Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii ili niweze kuzungumza kiasi, nadhani hata dakika 10 hazitofika kwa sababu mambo mengi yamekwisha kuzungumzwa ambayo nilikuwa nimeyaandaa kuyazungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kutoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa moyo wa dhati aliounesha kwa majeshi yetu ya Tanzania kuhakikisha ya kwamba wanaboreshewa nafasi zao za kufanyia kazi hali kadhalika na makazi yao. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na tunaunga mkono kazi kubwa anayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Wakuu wote wa Majeshi wa JWTZ na JKT kwa kazi nzuri wanayoifanya ya uzalendo. Nasema ya uzalendo kwa sababu hawa ndugu zetu kwa kweli maisha yao katika mazingira yao na wanapoishi kwa kweli majumba yao siyo mazuri na hata maeneo yao ya kazi siyo mazuri na makazi siyo mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali iweze kuwaongezea mfuko katika fungu la maendeleo kwani hawa watu wameonyesha uzuri wao wa ujenzi katika uzio wa Tanzanite. Wameonekana kwamba ni watu bora na wanaoweza kusimamia kitu katika muda mfupi na kuweza kukamilisha. Ni vema ndugu zetu wakaongezewa fedha za mafungu ya maendeleo ili waweze kukarabati, waweze kujenga miundombinu yote inayowahusu katika upande wa Jeshi kwa ukamilifu wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali au Wizara ya Fedha katika suala zima la kuweka ukomo wa bajeti ya Wizara ya Ulinzi kwa kweli ukomo ule siyo mzuri. Kwa mfano, mwaka huu walikuwa wamewekewa ukomo wa trilioni 1.9 lakini bajeti ya ulinzi bajeti ya Wizara ni trilioni 2.8. Nawaomba Wizara ya Fedha, kabla hawajafanya jambo lolote lile katika makusanyo yao ya fedha na kuzigawa fedha hizo, katika
kuziweka kwenye ukomo, waangalie kwa jicho la pekee Wizara ya Ulinzi. Ulinzi ni kila jambo, ulinzi ni kila kitu, bila ulinzi mengine yote hayawezi kuyafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza hivyo hata katika Wizara ya Mambo ya Ndani, nilizungumzia suala la Wanajeshi, tusiweke ukomo jamani, wanafanya kazi ngumu ni ngumu sana. Wanajeshi wana hali ngumu sana bila wao tusingekuwepo hapa. Mimi leo asubuhi nilipokuwa nakuja Bungeni nilipowaona wenzangu wa Jeshi nikasema leo ni usalama mtupu katika Bunge letu. Kwa hiyo, wanajeshi tunawapongeza na tunawatakia kila la heri katika maisha yenu katika kazi ngumu mnayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara waone umuhimu kabisa katika bajeti hii waliyoiomba Wizara ya Ulinzi kwanza ni ndogo. Wamefanya hivyo kwa sababu ya ukomo, naomba hii bajeti waliyokuwa wameiandika itolewe yote asilimia mia kwa mia, wala pasiwe na mjadala wa kuiacha hii sehemu fulani, kwa sababu mwaka jana wametoa asilimia takribani 80, lakini hii asilimia 20 iliyobaki pia nayo tunaomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha kabla ya tarehe 30 Juni, fedha hii iweze kupelekwa katika Wizara ya Ulinzi ili waweze kukamilisha malengo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuzungumzia suala la maendeleo. Katika suala la maendeleo mwaka 2017/2018, katika Mashirika yetu Mzinga tulipata asilimia 38 na Nyumbu tulipata asilimia saba ni aibu. Nasema ni aibu kwa sababu hawa watu wanachokifanya wanafanya kitu ambacho kina maslahi kwetu. Wanapunguza gharama ya utengenezaji wa vifaa mbalimbali kwa Taifa na kupunguza gharama ambayo inatoka nchi za nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo basi ni vema tukawapa fedha zao kamili ili waweze kukamilisha malengo yao. Kwa maana hiyo Wizara katika Fungu Namba 38, mwaka 2017/2018 tulipata asilimia 41. Sasa naomba hizi bilioni nane za 2018/2019, zitoke zote. JKT - Fungu 39, bilioni sita na pia Wizara bilioni 220, naomba zitoke zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli naomba Wizara ya Fedha, sijui kwa sababu Mheshimiwa Waziri Mwinyi ni mtu mtaratibu, mkarimu ambaye hataki vurugu ndiyo maana labda wanambana hizi fedha hazitoki zote. Naomba ndugu zangu msimchukulie ukimya wake na upole wake kutoweza kumpa katika ukamilifu, naomba mumpatie kwa asilimia 100 fedha zake za mafungu yake aliyoomba kwa maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuzungumzia suala la JKT. Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha elimu bure. Baada ya kupitishwa elimu bure vijana wetu wengi ambao wanamaliza darasa la saba, wanamaliza darasa la 12 wanakuwa wako mitaani na hawana mahali pa kwenda. Tunaomba vijana hawa waweze kuchukuliwa kwenda kujiunga na JKT ili waweze kupata uzalendo wa nchi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, idadi ya wanaochukuliwa kutoka kwenye Mkoa hawazidi vijana 100, kila wanapokuwa wanafanya reshuffle ya kusaili vijana wa JKT wanachukua chini ya 100. Naomba hii idadi iweze kuongezwa kwa kila mkoa, idadi iwe ni kubwa kwa sababu tumeamua kuongeza Kambi za JKT, kwa hiyo, tunaomba tuongeze idadi ya watoto wanaochukuliwa kwenda JKT.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kutoa shukrani za dhati, nilipoingia Bungeni niliulizia suala la Kambi ya Luwa na Kambi ya Milundikwa kwamba yawe ni Kambi za Jeshi. Nashukuru kwamba sasa zimerejeshwa kuwa ni kambi za JKT, kwa maana hiyo nawashukuru sana kwa maamuzi hayo ili vijana wengi wa Mkoa wa Rukwa nao watapata nafasi ya kujiunga na JKT. Ahsanteni sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine naomba kutoa pongezi za dhati kwa Wanajeshi wetu kwa kazi nzito wanayoifanya. Naiomba Serikali yangu sikivu, kwa heshima na taadhima kubwa, tujaribu kusukuma yale mashirika na zile taasisi na zile Wizara ambazo zinadaiwa na SUMA JKT, naomba walipe madeni hayo. Walipe madeni hayo kuhakikisha kwamba ndugu zetu wa SUMA waweze kuendeleza shughuli wanazoziendeleza za maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa sijawahi kununua trekta kwa sababu matrekta yalikuwa na bei kubwa, lakini leo baada ya JKT SUMA kutoa matrekta nimeweza kununua trekta na wamewasaidia sana wakulima wadogowadogo wenye kipato kidogo kuweza kulipa by installment na kuweza kukamilisha matrekta yale na sasa hivi wanalima kwa tija inayokubalika kwa hivi sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana kama tunavyosukuma madeni ya TANESCO, kama tunavyosukuma madeni ya maji, basi naomba tusukume na madeni ya SUMA JKT ili waweze kujiendeleza na waweze kuleta maendeleo kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, kwa heshima na taadhima napongeza Jeshi langu la Tanzania kwa kazi nzuri wanayoifanya nasema kwamba Aluta Continua na big up, hamna matatizo tuko pamoja na ninyi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.