Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi ya kuchangia kwenye eneo hili muhimu. Jambo langu la kwanza ni huduma mbalimbali ambazo zilikuwa zinatolewa Jeshini. Jeshini walikuwa wanauza vifaa vya ujenzi ambayo ilikuwa inaleta unafuu kwa Wanajeshi, walikuwa wanapata huduma mbalimbali za vinywaji, hivi vitu vikaondolewa kule Jeshini, nataka tupate kauli ya Mheshimiwa Waziri kwamba, baada ya kuondoa hizi huduma Jeshini nini mbadala wake sasa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa ni watu ambao wanakuwa maeneo yao ya kazi kwa muda mwingi, kwa hiyo ile kupunguza bei ina maana na wenyewe hawafanyi biashara zingine za kuingiza kipato ilikuwa inawasaidia sana, nasikia malalamiko mtaani huko. Kwa hiyo, nadhani Waziri atupe maelezo nini kitu mbadala wa hiyo huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka kuliongelea ni fedha kutotosha, lakini fedha ambazo zinapangwa kwenye Wizara hii pia ambayo ni muhimu sana kwa bahati mbaya sana baadhi ya Mafungu hazipelekwi kabisa. Nimejaribu kuangalia kumbukumbu kwa mfano 2015 kuna fedha hazikwenda, maeneo mengine wamepeleka mpaka asilimia tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano specifically Ngombe Fungu la 38 mwaka 2016 zilitengwa shilingi bilioni nane ambazo zilipaswa kufanya miradi kwa mfano kujenga Uwanja wa Ndege wa Tanga, kujenga maghala ya mlipuko ili kuepuka mambo kama yale ya Mbagala na Gongo la Mboto ambayo yalituathiri, lakini kwa bahati mbaya Fungu hili mwaka 2016 hawakupelekewa hata senti moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unaweza ukaona hali ilivyo katika hili na ni sehemu zipo nyingi sana ambazo zimetajwa, asilimia 1.3, asilimia nane, asilimia 12 na asilimia 13. Kwa hiyo, fedha zinatengwa pamoja na kwamba ni pungufu lakini pia hazipelekwi katika maeneo haya. Tunaomba hiyo fedha iliyotengwa hata kama ni kidogo kiasi gani ipelekwe ili miradi iliyopangwa na Jeshi hili katika maeneo mbalimbali iweze kuzipata fedha kwa wakati ili miradi hiyo ambayo imekusudiwa kufanywa itekelezwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, wenzangu wamependekeza suala la utafiti. Ukienda kwa mfano kama kile kituo cha NASA kule Marekani, nilipata fursa siku moja kukitembelea, wale watu asilimia 95 ni Wanajeshi na ndiyo wagunduzi wakubwa. Sasa kwetu hapa tuna Sheria ya Jeshi tangu mwaka 1966, nadhani sasa ni wakati muafaka hii sheria iletwe hapa Bungeni ibadilishwe ili Jeshi letu liendane na Jeshi la kisasa la sayansi na teknolojia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vyovyote vile hata kibinadamu tangu mwaka 1966 mambo ambayo yamepangwa kwenye hiyo ya sheria kwa kweli yamepitwa na wakati. Kwanza ulikuwa ni wakati wa ukoloni, nchi nyingi zilikuwa hazijapata uhuru, teknolojia haijakua na watu wengi hawajasoma, sasa tunataka Jeshi la kisasa, lenye wataalam waliobobea na wapanue wigo, lakini hawawezi kupanua wigo kama sheria haijafanyiwa marekebisho. Kwa hiyo, tungeomba hiyo sheria iletwe Bungeni, ifanyiwe marekebisho iendane na wakati kwa maana ya Jeshi la kisasa na la kukidhi mahitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo tulizungumza hapa, Jeshi la Wananchi kwa sasa ni chombo ambacho kimebaki Watanzania tunakitegemea wote bila vyama vyetu, lakini tunawashauri Serikali na Mheshimiwa Waziri ni muhimu sana wakati wa uchaguzi 2010 na 2015 kule Zanzibar Jeshi lilihusika kusimamia uchaguzi, kazi ambayo ni ya Mambo ya Ndani. Tunaomba jambo hili lisirudiwe tena kwani ni jambo baya kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji chombo ambacho ni very independent, kifanye kazi iliyokusudiwa, kama kuna mahali kuna hali ya hatari imetangazwa, waingie sababu inaeleweka, haya mambo ya uchaguzi ya siasa humu ndani acha tupambane na Polisi ambao tumezoeana Mheshimiwa Mwigulu anajua hilo, lakini Jeshi wafanye kazi yao, tutawapa ushirikiano, tunawaheshimu sana wabaki. Tusiwe kila mahali tunayogusa tunaingiza siasa kitu ambacho kwa kweli sio sawasawa, itafika mahali tuanze kulalamikiana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine limeulizwa hapa jambo la kuhusu mipaka, nadhani ni muhimu tukapata majibu. Imetajwa kwamba kwa mfano Tarime ambako ni kwetu, kule kuna beacon ziliondolewa maeneo ya Migori na ni muda mrefu, mazungumzo yamefanyika hayajakamilika. Kwa hiyo, tungeomba mambo haya na yenyewe pia yafanyiwe kazi yaishe kwa sababu ni mambo ambayo yana maswali ambayo yanazungumzwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo madai mbalimbali ya Wanajeshi. Mimi ni Mbunge wa Jimbo la Ukonga, tuna Kambi ya Jeshi pale na lile Jimbo vilevile lina wastaafu wengi. Kwa kweli Mheshimiwa Waziri ni aibu, mtu ambaye amekuwa mstari wa mbele aliyeapa kwamba yeye anakufa kwanza ndiyo nchi yake ibaki salama, ana-sacrifice maisha yake, halafu amefanya kazi muda mrefu sana, amestaafu, anaganga njaa mtaani na mkongojo anadai fedha yake ya kustaafu, siyo jambo jema kwa kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwanajeshi anadai uhamisho, kwanza wenzetu hapo ni amri, mnaamrisha nenda kituo, eneo au kambi fulani, anafunga mizigo hata familia hakuiaga, ameacha mke na watoto wanadai fedha za uhamisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu bima za afya. Wanajeshi hawana bima kwa hiyo wakienda kwenye duka la Jeshi akikosa dawa naye hana pesa, mke au mtoto wake, atakufa. Hivi akiwa vitani umemtuma kazi maalum ya nchi atafikiria familia au atafanya mapambano. Kwa hiyo, nadhani wapewe huduma zao, wapewe bima, hii siyo sawa sawa, hawa watu wanasafiri sana ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, JKT wapewe miradi ya ujenzi, wamefanya kazi kubwa sana, tulikwenda juzi kule Nyakato - Bukoba, JKT wanafanya kazi nzuri. Wapewe kazi ya miradi wana uzalendo wana-save hela ya Serikali ili watimize azma, wanafanya kazi nzuri sana nami nawapongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.