Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Sadifa Juma Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Donge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. SADIFA JUMA KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri na Watendaji wake wote, akianza Mkuu wa Majeshi na Watendaji wengine wote, tunawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunawapongeza maana wengine huwa hatupongezi tu hivi hivi. Viongozi ninyi tunawaamini kwamba mna vission, mission na capacity mpaka jeshi letu hili limekuwa imara mpaka hivi sasa na ni wasikivu pia, tunasema hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usipingika kwamba Jeshi la Ulinzi Wananchi wa Tanzania linafanya kazi kubwa sana na kwa weledi wa hali ya juu katika kutekeleza majukumu yake. Jeshi katika jukumu lake moja ni kulinda amani na mipaka ya nchi yetu, hilo ni jukumu lao moja. Kwa hiyo, wanafanya kazi vizuri sana, Mheshimiwa Yussuf Mjomba wangu aliyesema kwamba Tanzania hakuna amani kwa sababu kuna mtu anasema aliuawa akiwa anatetea ardhi yake au mali yake, Mheshimiwa Yussuf alisema hivyo! Alisema anakataa kabisa kwamba Tanzania hakuna amani eti kwa sababu mtu mmoja alifariki kwa sababu kutetea haki yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwuambie kwamba atofautishe baina ya majukumu ya Jeshi la Polisi na majukumu ya JWTZ. Jeshi la Polisi jukumu lake moja ni kulinda raia na mali zao. Sasa anapokufa mtu mmoja huko akisema kwamba anatetea haki yake ina maana unapozungumzia suala la amani hakuna tafsiri halisi kwamba hii hakuna amani, hata ndani ya nyumba yako ukigombana na mkeo unaweza ukasema katika nchi hii hakuna amani kwa sababu wewe huna amani ndani ya nyumba yako? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka nimwambie Mheshimiwa Yussuf atenganishe majukumu ya Jeshi la Polisi na majukumu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania wanafanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na pongezi ambazo nimempa Mheshimiwa Waziri, pamoja na pongezi nilizompa Mkuu wa Majeshi kuna problem ndani ya Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania na Mheshimiwa Waziri naomba anisikilize vizuri sana katika hili pamoja na CDF. Muda wa kuingia kazini na kutoka kazini Jeshini siyo mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana 2017, Wapinzani walilisema na CCM tunasema, CDF tunaomba sana hebu angalia muda mzuri Wanajeshi wetu watoke na kuingia kazini vizuri. Kwa mfano, watu wa Dar es Salaam anatoka nyumbani kwake saa 12.00 asubuhi anarudi saa 5.00 usiku nyumbani kwake, kila mmoja anajua Dar es Salaam kuna foleni. Kisaikolojia inawaumiza pamoja na kwamba ni Wanajeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakwenda kwa ufupi sana, niombe tena Jeshini kuna kozi ya Junior kwa kwa wale ma- Captain, Captain anatakiwa afanye course ile ya Junior Staff College kama sikosei, lakini leo hii inafanya course ile akiwa Meja na bahati mbaya sana Meja hawa wamekuwa wengi mno wanakaribia kuwa Luteni Kanali muda wao umefika, lakini hawavai vile vyeo vya Luteni Kanali mmoja huyo hapo Dafa Msaidizi wako, katika hawa wanaosubiri muda huo na yeye yumo, mimi alinifundisha huyo course.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana hii course hii kwa nini wasiifanye kule wakiwa Captain? Kwa hiyo wanarundika sana wanashindwa kupanda kuwa Mameja. Nasema wanafanya kazi nzuri na tunawapenda sana tunawatakia kila la kheri katika majukumu yenu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni Wizara ya Fedha, kila anayesimama hapa anazungumzia Wizara ya Fedha, tunawaomba sana Wizara ya Fedha, tunajua kwamba tuna upungufu wa fedha Tanzania ni maskini, lakini pamoja na umaskini tulionao hebu tunaomba tusaidie sana ili Wizara hii ya Ulinzi wasishindwe kutekeleza majukumu yao. Kuna madeni kuna pesa huko za likizo hazijalipwa, 2015 waliambiwa watalipwa mpaka leo hawajalipwa lakini tunajua ni kwa sababu fedha ni kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika eneo lingine, kuna mtu hapa alisimama akasema Mheshimiwa Rais ile issue ya Arusha pale sijui alichemka. Tukumbuke tusome Katiba nani Rais katika Katiba yetu. Rais ni Amiri Jeshi Mkuu, Rais ni Head of the State, Rais ni Head of the Government, naomba sana tusichanganye, Rais ni Amiri Jeshi Mkuu; kama ni Amiri Jeshi Mkuu maana yake ana mamlaka ya kuliamrisha Jeshi hili kufanya lolote atakaloona inafaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais alikwenda pale akatekeleza vema jukumu lile, alitekeleza vema jukumu ya Kamisheni kwa Officer’s na Maafisa walitunukiwa, kazi yake aliyoiendea pale ilikamilika, baada ya kukamilika ndipo akasema sasa anafanya kazi iliyobaki akiwa ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, hakuna amabaye anaweza akazuia Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi asifanye kazi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani fimbo itakuwa imewakaa, mimi sikutaka kuchangia mengi nilisema nichangie hayo. Niwaombe sana Wizara ya Fedha, wawape fedha Wizara ya Ulinzi, ili hata Askari wetu hawa nazungumzia maeneo yote, ukienda Mambo ya Ndani kule unakuta kwa mfano, Mheshimiwa Mwigulu nisikilizeni vizuri na ninyi, mishahara yao hii ni kwa Askari wote Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania na Mambo ya Ndani, Wizara ya Fedha wakiwapa fedha maana yake watalipwa mishahara vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hii migogoro mingine inayozungumziwa, baadhi wanashindwa kupima kwa sababu hawana fedha. Kwa hiyo, niwaombe sana Wizara ya Fedha watekeleze majukumu yao, wajitahidi kwa mujibu wa uwezo wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo machache, mimi sikutaka kuzungumza sana nina imani ujumbe umefika. Nashukuru na naunga mkono hoja.