Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, JWTZ kupora ardhi ya wananchi wa Kenyambi, Kata ya Nkende na Bugosi, Kata ya Nyamisangura, zilizopo Halmashauri ya Mji wa Tarime. Napenda kuchangia kwa kifupi sana kwenye Wizara hii hasa katika suala zima la Jeshi la Wananchi la Tanzania kuchukua ardhi ya wananchi kinyume cha Sheria ya Ardhi na kulipa fidia stahiki na kwa muda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Igaga Mike kuwa JWTZ wana eneo lao ambalo ni kambi lililopo Kata ya Nyandoto ambayo lipo nje ya Mji, lakini kwa makusudi kabisa waliamua kujitwalia kwa nguvu eneo walilokaribishwa kwa muda kupisha uharibifu wa miundombinu ya daraja iliyosababisha kukatika kwa mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa miundombinu hiyo ilishakamilika, lakini JWTZ wamegoma kuhama badala yake wameendelea kuongeza maeneo ya wananchi na hii inaleta sintofahamu na inaweza kusababisha uvunjifu wa amani, maana wananchi wangu wamezuiwa kufanya shughuli zozote za maendeleo kwa miaka yote hii. Nimekuwa nalizungumzia hili tangu 2010 na kupangwa kwenye kila fedha za bajeti ya maendeleo kwamba watalipa fidia, lakini hamna hatua zozote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wangu waliweza kuunda Kamati na kufika hadi kwa Waziri kuelezea matatizo yanayowakumba kwa ardhi yao kuchukuliwa na wanajeshi bila kufanyika malipo ya fidia ili waweza kwenda kutafuta makazi mengine ama kama fidia imeshindikana kulipwa, basi Wanajeshi warudishe ardhi ya wananchi wangu ambayo wameendelea kujitwalia kila kukicha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Tarime wangependa kujua ni kwa nini Serikali ya CCM kwa makusudi imeshindwa kurudisha ardhi ya wananchi hawa na ikizingatiwa Halmashauri ya Mji wa Tarime ina changamoto kubwa ya ardhi na hawa Wanajeshi wamekuja katikati ya Mji kuchukua maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi kwa mila za Wakurya ni kitu kinachothaminiwa, Serikali itakumbuka vita nyingi za koo hutokana na migogoro ya ardhi. Hivyo, tunaomba ardhi yetu irudishwe na kwa kweli, wanajeshi warudi kambini kwao ambalo ni eneo kubwa waliloshindwa kulipia ada ya ardhi kwa miaka yote hiyo na kulitelekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, kuwepo kwa Wanajeshi kwenye hizi Kata za uvamizi kumesababisha matatizo mengi kama vile kunyanyasa wananchi wanaotumia barabara inayopita kwenye mitaa ya Bugosi na Kenyambi eneo walilochukua. Vilevile kuna kipindi wananchi wakifuatilia nyagabona za ng’ombe Wanajeshi huwazuia na kuruhusu mwanya wa wizi wa ng’ombe na hili hufanywa na baadhi ya Maafisa wasio waaminifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa vyombo vya moto hasa bodaboda ambao hupewa adhabu kali bila kuzingatia kuwa yale ni maeneo ya umma na si Kambi ya Jeshi na ndiyo maana tunashauri warudi kwenye kambi yao Nyandoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.