Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Rhoda Edward Kunchela

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Katavi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kuna changamoto nyingi, lakini ningeomba haya machache Serikali iyashughulikie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi lipewe hati za Kambi na maeneo yao kwani mpaka sasa wananchi wanaendelea kuwa na migogoro na jeshi na migogoro hii ni ya muda mrefu. Je, Serikali kupitia Wizara hii ni lini itaondoa unyanyasaji huu unaoendelea kufanyika kwa wananchi kuzuia kufanya shughuli za kiuchumi na wakati maeneo hayo bado yana migogoro? Je, Wizara haioni kuwa kuendelea kushindwa kutatua kero hizi ni kuwaongeza umaskini wananchi? Wananchi wanapigwa na wanajeshi wanapata vilema kwa sababu ya kuingia kwenye maeneo hayo ambayo mpaka sasa hatma yao haijulikani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Misunkumilo, Jimbo la Mpanda Mjini, Katavi mpaka sasa wananchi pale hawajalipwa fidia zao kwa sababu jeshi ndiyo lililoingilia mipaka ya wananchi. Je, Wizara inawafikiriaje wananchi hawa kwa kuwalipa fidia zao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wa ziada wa utumishi hauko katika sheria za utumishi. Wanajeshi wanaingia saa 12.00 asubuhi wanatoka saa 12.00 jioni. Ni sheria gani inawafanya wanajeshi kufanya kazi saa nyingi tofauti na watumishi wa umma? Sheria inasemaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba za askari ni chache na zimechoka. Tangu kipindi cha Mwalimu Nyerere mpaka sasa nyumba zilizojengwa ni chache mno na hii imepelekea wanajeshi kuishi pamoja na wananchi kitu ambacho kinaondoa dhima ya jeshi. Serikali wanaona jambo hili ni sahihi kama siyo sahihi kupitia bajeti hii wamejipangaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna malalamiko ya uonevu kutoka kwa wananchi kuwa baadhi ya wanajeshi wasio na maadili ya kazi wamekua wakionea wananchi kwa kuwapiga bila sababu kwa sababu tu ya vyeo vyao. Je, Serikali haioni kukaa kimya kwa matendo haya ambayo hayaendi na maadili ya kazi na vitendo hivi vinavyoendelea vinalichafua jeshi?