Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sumve
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamba ni siasa lakini pamba ni uchumi. Nitamke wazi kuwa siungi mkono bajeti hii kwa sababu moja kubwa. Mheshimiwa Waziri Mkuu alihamasisha sana Wakuu wa Mikoa, mikoa 10 na wilaya 46 zinazolima pamba, wananchi wakajitokeza kwa wingi wakalima kweli, kitu cha kushangaza ni kwamba matarajio ya wakulima hawa kwa bei ya mwaka jana kwa kilo moja ilikuwa Sh.1,200, lakini bila aibu mkulima huyu amejitolea kweli kweli, bei ya sasa kwa kilo moja ni Sh.1,100. Hivi mkulima huyu tunamsaidia namna gani? Kila mwaka msimu unapoanza, kelele ya bei ni kwa zao la pamba peke yake, hivi tatizo huwa ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kupitia bei ya soko. Bei ya soko ni senti 76, ukikokotoa utakuta thamani ya pamba nyuzi ni Sh.1,357 thamani ya mbegu ni Sh.281, ukijumlisha kwa kilo moja unapata Sh.1,638. Gharama za uendeshaji na uchambuaji kwa yote hayo ni Sh.405, ukitoa kwenye hiyo Sh.1,600 utabaki na Sh.1,233. Ni bora basi huyu mkulima ambaye amehangaika usiku na mchana kulima mngemuachia bei yake iwe kwa kilo Sh.1,200, Sh.100 mnamnyang’anya, kwa nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, eti wanasema hiyo ni kwa sababu mkulima huyu anatakiwa kulipia deni la viuadudu la shilingi bilioni 29, mkulima huyu alipie mabomba ya kupulizia shilingi milioni 525 lakini mkulima huyu alipie deni la mbegu shilingi bilioni 1.2, mkulima huyu alipie deni la shilingi bilioni 27.7, mkulima huyu huyu, lakini alipie na deni la miaka ya nyuma shilingi bilioni 3. Hivi wakati haya madeni mnayatengeneza mkulima huyu alikuwepo? Hakuwepo! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi jinsi mkulima huyu wa pamba anavyoonewa, analazimishwa kukatwa ile Sh.100 ili kusudi alipie mbegu kabla hata ya kulima, akatwe shilingi bilioni 16 lakini anunue chupa milioni tano shilingi bilioni 20, pia alipie mabomba shilingi bilioni 2. Hivi mkulima huyu hata kabla hajalima mnaanza kumkata kwenye hii Sh.100, huyu mkulima amekosea nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri, kwenye kitabu chake ukurasa wa 148, kwenye pamba, unasema kwamba mchango kwa ajili ya maendeleo ya zao la pamba fedha ambazo huwekwa kwenye Mfuko wa Pembejeo wa Zao la Pamba kwa ajili ya kusaidia kutoa mbegu na dawa za pamba, Sh.30 kwa kilo zinaondolewa. Unasema unaondoa Sh.30, unamuongezea Sh.100 utakuwa umepunguza au umeongeza? Kwa sababu huku unasema umeondoa Sh.30 lakini unakwenda unamuongezea Sh.100 huko, utakuwa umepunguza au umeongeza matatizo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mfuko kwa jinsi ulivyo, tunaiomba Serikali ukafanyiwe ukaguzi na CAG kwa sababu hiki ni kichaka cha watu kupata fedha za wakulima. Siku zote mifuko hii imekuwa ikiwanufaisha wao wala siyo wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina ugomvi hata kidogo na Mheshimiwa Waziri Tizeba, hata kidogo, ni mdogo wangu, ugomvi wangu uko kwa wakulima wa bei ya Sh.1,200, hii Sh.100 irudisheni kwa wakulima. Mnataka tutoke tani 122,000 twende kwenye tani 1,000,000 za pamba, mtafikaje huko kama mnawanyima incentive hawa wakulima? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wale wote wanaotoka kwenye mikoa wanayolima pamba, tusiunge mkono mpaka tupate maelezo ya kina kuhusu hii Sh.100. Sisi tunakubali kama ni Sh.1,200 lakini siyo kwa Sh.1,100. Mheshimiwa Tizeba mwakani kuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa, tutawaambia nini wale wananchi? Kama nilivyosema, pamba ni uchumi, pamba ni siasa, lazima tufike mahali tuwasaidie wananchi wetu, wamejitolea mno kulima na Waziri anafahamu jinsi walivyohangaika, kuna wadudu na matatizo mengine yamejitokeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi na hili naomba Waziri aje alifafanue vizuri zaidi, anasema ushirika kazi yake ni kukusanya, sijui unakusanya kutoka kwa nani? Yaani huyu mkulima achukue pamba yake ampelekee huyu ushirika, ushirika ambao tunaujua sote pamoja na Waziri, hii pamba yangu au yake? Halafu baada ya hapo aje mnunuzi, pamba yangu iende ikakae siku tatu, nimezoea nikuchukua pamba yangu naipeleka sokoni, napima kilo shilingi ngapi, nachukua hela yangu, sasa mkulima huyu aende akakopwe? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo jema kuimarisha ushirika lakini twende basi taratibu. Ukishasema kwamba kazi yao hawa ni kukusanya, je, anakusanya kwa siku ngapi? Kwa siku nne au tano yaani huyu mkulima apeleke pamba yake ikasubirie pale, Mheshimiwa Tizeba mdogo wangu nawe unatoka kwenye pamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siungi mkono hoja.