Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nachingwea
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kunipa nafasi niwe mchangiaji wa kwanza jioni hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeipitia na kuisoma vizuri hotuba ya Mheshimiwa Waziri na maombi ya fedha ambayo anaomba. Pamoja na yote ambayo yamewasilishwa nina mambo kadhaa ambayo napenda kwa niaba ya wananchi ambao tunawawakilisha hapa Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atupatie maelezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ni uendelezaji wa zao la korosho. Ziko jitihada kubwa sana ambazo zimefanywa na Serikali yetu lakini pia iko kazi kubwa sana ambayo sisi Wabunge pamoja na Serikali tumeifanya katika kutoa tozo zile ambazo zilikuwa kandamizi kwa wakulima wetu na hii imepelekea angalau kuona tija kidogo. Hata hivyo, yako mambo ambayo naona ni busara sasa tuweze kuelekezana na pia tupeane ufafanuzi ili tuweze kuona namna bora ambavyo tutaliendeleza zao hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na Mfuko wa Pembejeo ambao kazi yake kubwa ilikuwa ni kuendeleza zao la korosho. Kwa msimu wa 2016/2017, ziko fedha nyingi sana (export levy) ambazo wakulima wa korosho wamekatwa. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kusimama atueleze kwa mwaka nilioutaja 2016/2017 ni kiasi gani cha fedha zao la korosho limechangia lakini pia Serikali itueleze ni kiasi gani imerejesha kwa ajili ya uendelezaji wa zao hili la korosho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia tena Mheshimiwa Tizeba kila Mbunge aliyesimama kutoka Mkoa wa Lindi na Mtwara jambo hili amelizungumzia na mimi naomba kwa heshima na taadhima utakapokuja kusimama utuambie fedha ya export levy ambayo tulipaswa turudishiwe kwa ajili ya kununua pembejeo mpaka sasa hivi tunavyozungumza iko wapi na imetumika kufanya kazi gani? Kwa sababu utaratibu ambao sasa hivi unaendelea ni kinyume na makubaliano yetu ya awali na namna hata mfuko unavyotaka katika uendelezaji wa zao letu la korosho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo pia naomba ufafanuzi kutoka kwa Mheshimiwa Waziri ni nia haswa ambayo wenzetu wa Wizara wameanza kuionyesha. Kabla sijasema naomba kidogo niwakumbushe wale waliosoma historia. Kipindi cha ukoloni nchi hii iligawanywa katika kanda, yako maeneo ambayo yalikuwa yanalima mazao kutokana na hali ya hewa jinsi ilivyo. Leo hii ukienda Mwanza utakuta pamba, Kusini mwa Tanzania utakuta korosho na ndiko inakostawi na ndiko inakotoka korosho bora na ukienda Kaskazini huko utapata kahawa na chai. Leo hii sijajua ni tamaa kiasi gani imetuingia tunataka tulihamishe zao la korosho kutoka Kusini ambako lilikuwa linalimwa tulifanye kuwa zao la Tanzania nzima. Siyo jambo baya, kama tumeamua kuweka mkakati huo basi si vibaya Mheshimiwa Waziri atuambie ni kiasi gani cha fedha ya kahawa anaenda kutuletea watu wa Lindi na Mtwara ili na sisi tukaanze kulima mazao haya ya biashara ambayo yatakwenda kutusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki kinachofanyika nafahamu kina nia njema kwa wakulima na Watanzania na hii ni kwa sababu tayari tumeshaanza kuona faida kubwa ambayo inapatikana kwenye zao la korosho. Ukichukua mathalani Dodoma leo hii tunakuja kupanda korosho, mikorosho ambayo mmeisambaza mwaka uliopita mpaka sasa hivi iko majumbani inakauka tu, hamna mtu yeyote ambaye anaishughulikia na anaifanyia kazi. Wakati mikorosho hii tungeweza kuisambaza Tandahimba, Mauta, Nachingwea na Liwale ambako hali ya hewa inaruhusu ingeweza kuleta tija zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaomba Mheshimiwa Waziri atuambie hasa anachokusudia kukifanya ni nini. Kama lengo ni kutawanya keki hii basi si vibaya na sisi watuletee fedha za pamba, kahawa na chai ili na sisi tuweze kulima katika maeneo yetu kwa sababu ardhi yetu nayo pia inaweza kuhimili na kupokea mazao hayo kama ambavyo maeneo mengine wanafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kupata ufafanuzi kupitia watu wa Wizara. Ukisoma Ripoti ya CAG, ukurasa wa 148 – 151, umeeleza ubadhirifu mkubwa sana ambao umejitokeza katika uzalishaji wa zao la korosho. Ziko hatua ambazo tulitamani kuziona zinachukuliwa na zitatusaidia sana kuendeleza zao la korosho kama ambavyo Serikali na watu wa Wizara wamekusudia. Najua uko wakati ambao tutajadili ripoti ya CAG lakini ni vizuri wakati tunaenda kujadili bajeti ya Wizara hii lazima tuone hatua na dhamira gani watu wa Wizara wamekuwa nazo kwa ajili ya kuhakikisha ubadhirifu ambao umeendelea kujitokeza kwenye zao la korosho unadhibitiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ukisoma utaona kupitia Mfuko wa Hisani wa Kuendeleza Zao la Korosho iko fedha ambayo ilipaswa tayari iwe imeshakatwa kutoka kwa watu wa vyama Sh.4,085,000,000. Mpaka mwaka huu wa fedha ambao tunaenda kuumaliza fedha hii haieleweki ipo kwa watu wa vyama vya ushirika kwa maana kwenye akaunti zao au ilitakiwa iwe wapi kwa sababu wako watu ambao wamekatwa na hawa ni wakulima ambao sisi tunawawakilisha. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba sana, haya siyo maneno yangu ni ripoti ya CAG ukiisoma vizuri inabainisha na inataka watu wanaohusika na eneo hili watueleze fedha hii shilingi bilioni 4 iko wapi mpaka sasa hivi ili tuweze kuwarudishia wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine katika ripoti hii ya CAG ukiiangalia vizuri utaona wako watu ambao wamepewa fedha kwa ajili ya ubanguaji wa korosho. Iko Kampuni moja inaitwa Jumbo Cashewnuts na kikundi cha akina mama wanaonekana wamechukua fedha zaidi ya shilingi milioni 500, fedha hii haijarejeshwa mpaka leo tunavyozungumza. Wako viongozi wa Bodi ya Korosho wamechukuliwa hatua lakini hatuamini kwamba wale wachache waliochukuliwa hatua ndiyo pekee ambao wamehusika na upotevu wa fedha za wakulima. Tunaomba Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana na timu yake watuambie wote wanaowasaidia viongozi wote wa Bodi ya Korosho ni hatua gani watakwenda kuchukuliwa kwa usumbufu na hasara kubwa ambayo wamewasababishia wakulima wetu ambao kimsingi mpaka sasa uendelezaji wake unasuasua. Wale wanaopaswa kukopeshwa hizi fedha bado hawajakopeshwa kwa sababu tu kuna watu ambao makampuni yao yamechukua fedha na hawajazirejesha kwa wakulima ili tuweze kuingiza katika mzunguko ambao utatusaidia kuwakomboa wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nilitaka nilizungumze ni suala zima la uchelewaji wa malipo. Yako makampuni leo tunazungumza mwezi wa tano takribani miezi sita imepita toka tumefunga minada bado hawajalipa wakulima fedha zao. Hili ni jambo la hatari na la kukatisha tamaa sana. Wakulima wetu walio wengi sasa hivi wanapata shida ya kuendesha maisha yao kwa sababu fedha zao kuna makampuni wamezikalia. Ziko sheria ambazo zinataka wale waliochukua fedha hizi kuchukuliwa hatua lakini mpaka sasa hivi kesi nyingi ziko polisi na wakulima wanaopaswa kulipwa hawajalipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Mheshimiwa Naibu Waziri alishafika katika maeneo yetu na hasa aliishia Masasi lakini naomba niwape taarifa, walichokiona Masasi ni sehemu tu bado maeneo ya Nachingwea ukienda Liwale kuna wananchi mpaka leo napozungumza, mkihitaji ushahidi wa haya nitakuja niwaambie hawajalipwa fedha zao na wanaendelea kuzungushwa. Kesi zinaenda polisi hazifikishwi Mahakamani, hatujui sababu za kesi hizi kutofikishwa Mahakamani ni nini wakati wakulima walishatoa korosho zao kwenye makampuni haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishauri makampuni yanayoshindwa kulipa yaondolewe katika ununuzi wa korosho za wakulima. Jambo hili huu sasa mwaka wa pili halijafanyika na makampuni haya yanaendelea kushiriki kwenye ununuzi wa korosho. Sasa hii kidogo inatupa shida kujua dhamira yetu haswa ipo katika eneo gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nilitaka nichangie ni zao la mbaazi. Mheshimiwa Waziri Mzee Tizeba kila tunaposimama hapa tunazungumza suala la mbaazi, uchungu wake ni kama bado haujawafikia lakini kwa sisi tunaokaa na hawa wakulima hili jambo tutapaza sauti kila tutakapopata nafasi ya kusimama hapa mpaka Serikali itakaposhtuka. Wakulima wetu bado wanaendelea kuzalisha mbaazi lakini hakuna mikakati yoyote ambayo itaenda kumkomboa mkulima anayelima mbaazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako majibu hapa tumepewa kwamba tulime mbaazi na ikiwezekana tule kama mboga haina shida, hizo sisi tunakula kama mboga lakini bado tunaomba majibu ya kina. Nimeisoma hotuba vizuri sana inaeleza kwamba Serikali itaendelea kuimarisha soko la ndani lakini pia itaendelea kuhamasisha viwanda ambavyo vitafunguliwa kwa ajili ya kuendeleza au kununua zao hili. Tunaomba kupitia Kitengo cha Utafiti watuambie bado tuna mahitaji ya mbaazi? Kama hatuna mahitaji tuwaambie wakulima wetu wasiingie hasara ya kulima mashamba makubwa ambayo tija yake mpaka sasa hivi bado haijaonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha naomba jambo hili alipe kipaumbele, tunaomba statement, tunaomba kauli yake vinginevyo mwezi wa saba, wa nane tutakuja hapa kumlaumu kwamba kwa nini mbaazi haijanunuliwa wakati hili jambo siyo lake yeye.