Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo

Hon. Ignas Aloyce Malocha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo

MHE. IGNAS A MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nitangulie kusema moja kwa moja siungi mkono hoja. Siungi mkono kwa sababu nitakazozieleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkulima wa mahindi katika nchi hii amekuwa kama mfungwa au kuku ambaye mama yake amekufa. Toka mwaka jana Waheshimiwa Wabunge wengi wamekuwa wakizungumzia shida ya mkulima wa mahindi katika nchi hii na mpaka sasa hivi shida hiyo inaendelea. Nilitarajia kwenye bajeti hii kutakuwa labda na maelezo ya kuwakosha wakulima wa mahindi lakini ndiyo inazidi kuwaumiza zaidi. Kwa kweli hii si haki hata kidogo.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkulima wa mahindi anauza gunia Sh.15,000, huyu mtu nadhani yuko mbioni kujinyonga, hakika. Kwa kweli kitendo hiki hakiridhishi na hakifurahishi mtu yeyote. Wakulima wa mahindi katika nchi wanateseka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi Waziri katika hotuba yake anasema kuuza mahindi nje mpaka apewe kibali, apewe kibali ulimsaidia kulima? Amelima kwa jitihada zake mwenyewe, mkulima wa kijijini kule aanze kushughulika na kibali? Jamani, tufike mahali tuwaonee huruma wakulima yaani mkulima wa kijijini aanze kuangalia na kibali, amelima kwa shida aanze kutafuta kibali cha nini? Kama unaona kuna shida si ununue mazao hayo uyahifadhi mwenyewe kwenye ghala lako? Nunua uhifadhi kwenye ghala si kazi ya mkulima kutunza chakula cha nchi hii, mkulima analima kwa ajili ya kujikimu maisha yake yeye mwenyewe. Mimi nadhani tufike mahali tulione jambo hili, si sahihi hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza hili kwa niaba ya wananchi. Mimi wananchi wangu wa Jimbo wako karibu 450,000, wamenituma nizungumze kwa nguvu zote jambo hili na linawauma kwelikweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kutotenga fedha za kutosha katika kilimo cha umwagiliaji, hii ni ajabu sana. Duniani kote kilimo cha umwagiliaji ndiyo chenye tija. Bahati nzuri katika takwimu zetu zinaonyesha karibu hekta milioni 29.4 tunazo fursa za kulima kilimo cha umwagiliaji lakini katika utekelezaji zilizoshughulikiwa ni hekta 461 sawa na asilimia 1.6. Hivi kweli tuko serious katika kilimo? Hatuko serious katika kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nashangaa, maendeleo ya viwanda duniani kote yalianza na mapinduzi ya kilimo. Mapinduzi ya kilimo ndiyo yanaleta viwanda. Sasa ni ajabu sana kilimo kinakuwa pembeni. Hivi vipaumbele mnavyoweka mnamuuliza nani? Mtuulize sisi tunaotoka kwa wananchi, ndiyo, mtuulize sisi ambao tunatoka kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wakati wa uchaguzi alisema wazi kwamba hatambughudhi mkulima, mkulima awe uhuru kuuza kokote anakotaka, sasa haya maneno mnayatoa wapi? Mimi nashangaa Ndugu yangu Mheshimiwa Tizeba siwezi kukulaumu kwa sababu bajeti hii hupangi nyumbani kwako, hivi hawa wataalamu ambao wamesomeshwa na nchi hii wanafanya kazi gani kusaidia wananchi hawa? Kwa sababu hii bajeti Waziri hupangi nyumbani kwako, unakaa na wataalam mnashauriana sasa wanashauri kitu gani, hayo ma-degree waliyonayo ni ya kumuumiza mkulima? Mimi nashindwa kuelewa. Kwa kweli tufike mahali tuangalie jitihada anazofanya mkulima kwa kukimu maisha yake tusimtese kwa kiasi hiki. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni pembejeo. Kila mwaka pembejeo zinachelewa, sijawahi kuona mwaka pembejeo zikawahi au zikakidhi, ni stori isiyo na mwisho, hii stori itaisha lini? Kwa sababu ni mazoea, mimi tangia nimeingia Bunge hili hiki ni kipindi cha pili sijawahi kuona pembejeo zikatosheleza au zikawahi. Pembejeo za kupandia zinakuja wakati wa kupalilia mahindi na za kukuzia zinakuja karibu watu wavune mahindi, huu ni utaratibu wa wapi? Tunaomba Mheshimiwa Tizeba anapokuja kujibu afafanue mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la mawakala. Mawakala hawa ni binadamu kama binadamu wengine, ni wafanyabiashara kama wafanyabiashara wengine. Kama lilitokea tatizo la wizi si mmeshachambua basi tangazeni kwamba idadi ya watu fulani ni wezi hamlipwi. Hivi wote ni wezi kweli jamani, hivi mawakala wote ni wezi? Hii ni dhuluma na Mwenyezi Mungu hapendi dhuluma ya namna hii. Lazima mfike mahali mchambue wezi muwapeleke Mahakamani wenye haki wapate, siyo kwamba mawakala wote walikuwa wezi, hamna kitu cha namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mawakala hawa ndiyo wanaoishi na wananchi na ndiyo wanaosaidia nchi hii katika kuleta maendeleo, sasa leo hii mnawatema kiasi hiki ndugu zangu? Hapana, hii si haki hata kidogo. Jaribuni kuchambua wale waliofanya kazi kwa uaminifu wapate kilicho chao. Kama wengine walivyochangia, wengine wamekufa, wengine nyumba zao zimeuzwa, hii siyo haki hata kidogo. Tunaomba Serikali mjaribu kuliangalia suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilitaka kuzungumzia ni suala la mbolea. Tunajua Serikali inataka kuleta mfumo wa mbolea inayotengezwa ndani ya nchi tunakubali na kwa jina mnasema Minjingu, hii Minjingu mmeifanyia utafiti wa kutosha? Kwa sababu kipindi kilichopita wananchi walilalamika sana na wengine walipata hasara, hatukatai kama imeboreshwa mtueleze imeboreshwa kwa kiasi gani lakini hata kama imeboreshwa uwezo wa kukidhi nchi hii kwa Minjingu sidhani kama itaweza. Kwa hiyo, lazima hilo nalo Serikali mliangalie, nia ni njema mnataka tuchukue mbolea ndani ya nchi lakini mtueleze Minjingu imeboreshwa kiasi gani na uzalishaji wake uko kiasi gani kama unaweza ukakidhi mahitaji ya wananchi. Kwa hiyo, jambo hili mnapaswa kuliangalia kwa macho mawili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kushuka kwa bajeti ya kilimo. Bajeti ya kilimo inashuka mwaka hadi mwaka. Mimi nashindwa kuelewa, kwa mfano mwaka jana bajeti ya kilimo ilikuwa ni Sh.150,253,000,000 zilizotolewa ni Sh.27,231,305,232 sawa na asilimia 18, hapa ndipo unaweza ukaona hivi kuna u-serious katika kilimo? Yaani mmetenga bajeti halafu kiasi mnachotoa ni asilimia 18 na mbaya zaidi kwa mwaka huu imeshuka tena hata ile bajeti, kama bajeti imeshuka hivi asilimia itakayokuja ni asilimia 3, hakika. Kwa sababu unaangalia hata bajeti iliyotolewa imeshuka badala ya bajeti ya kile kiwango kilichopita. Jamani msaidie Rais huyu, tunaona kazi nyingi zinaleta ufanisi pale Rais au Waziri Mkuu wanapoingilia kati ninyi wasaidizi wake msaidieni Rais huyu wa wanyonge. Sasa wanyonge wenyewe hawa wakulima ndiyo wanaanza kuteseka, mnaenda kinyume na matamko ya Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni Maafisa Ugani. Tunaomba Serikali iwasimamie hawa Maafisa Ugani. Maafisa Ugani wanafanya kazi wanavyotaka, hakuna anayewasimamia kuleta tija katika kilimo, wanafanya kazi kama wanavyotaka. Tunaomba hawa watu muwasimamie kila Afisa Ugani kwenye eneo lake aeleze ameleta tija kiasi gani na uzalishaji umeongezeka kiasi gani kwa eneo dogo. Wapimwe kwa vigezo vya uzalishaji katika eneo dogo, maana tunaona tu wanakaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine wapeni mafunzo rejea, mmewapeleka tu hawana mafunzo rejea. Juzi tumeelezwa juu ya wadudu wanaoshambulia mazao mbalimbali sina hakika kama Maafisa Ugani wanapewa elimu hiyo, hawapewi. Tunafanya kazi kwa mikupuo, tungeomba Maafisa Ugani wasimamiwe kwanza lakini wapewe elimu rejea na vilevile wapewe malengo kwamba wewe umepewa eneo hili tunataka kiwango cha uzalishaji kiongezeke kutoka mahali hapa kwenda mahali hapa na anafuatiliwa kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ongezeni idadi ya Maafisa Ugani kwa sababu utaalam unasema Afisa Ugani anatakiwa kuhudumia wakulima 1,600. Sasa unaweza ukakuta Afisa Ugani ni wa kata nzima yenye vijiji vitano ataweza kweli na hana usafiri? Kwa hiyo, hili nalo tungeomba Serikali iweze kuliona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siungi mkono hoja mpaka nitakapopata maelezo.