Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Madaba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mimi naomba nijielekeze moja kwa moja kwenye hoja na mchango wangu utajikita kwenye eneo la soko la mazao ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kupata mapinduzi ya kilimo Tanzania kama hakutakuwa na mfumo madhubuti wa soko la mazao. Kinachomfanya mwananchi wa Madaba, mwananchi wa Njombe, Songea Mkoa wa Ruvuma, mwananchi wa Katavi, mwananchi wa Rukwa, mwananchi wa Sumbawanga, Songwe na Mbeya aamke asubuhi, aweke jembe begani akalime ni kwa sababu anataka kupata pesa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkulima haendi kulima kwa ajili ya kutatua tatizo la food security ya nchi, ile ndiyo ofisi yake. Mwananchi wa Madaba, mwananchi wa Katavi anakwenda kulima mahindi kwa sababu anataka ajenge nyumba bora, kwa sababu anataka asomeshe mtoto wake katika shule zenye sifa, kwa sababu anataka amudu mahitaji ya afya katika hospitali zenye ubora, anataka kuishi maisha bora huyu Mtanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaongelea asilimia 70 ya Watanzania ambao kipato chao kinatokana moja kwa moja na shughuli za kilimo, lakini tunaongelea asilimia karibu 90 ya Watanzania ambao kwa namna moja au nyingine wanategemea kilimo. Huwezi kupata mapinduzi ya kilimo bila mfumo madhubuti wa soko la mazao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Madaba wameumia sana na mfumo wa masoko, pia wananchi wa Mikoa yote niliyoitaja ukiwemo na Morogoro wameumia sana juu ya ukosefu wa soko la mahindi. Wakulima hawa kama ambavyo Wabunge tunataka tuwasomeshe watoto wetu katika shule zenye sifa, tujitibu vizuri, tujenge nyumba bora, tuvae nguo safi, nao pia wana ndoto hiyo. Hatuwezi kuipata Tanzania yenye mapinduzi ya kilimo kama hatutaki kuwekeza kwenye masoko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe ushahidi, ukuaji wa sekta ya kilimo mwaka 2014/2015 ulikuwa asilimia 3.4 na ukuaji wa sekta hiyo mwaka jana 2016/2017 ilikuwa asilimia 2.1, kwa nini? Kwa nini ukuaji umeshuka ni kwa sababu incentive ya mkulima ni soko. Hawezi kwenda kununua mbolea, hawezi kujikita kwenye mbegu bora, hawezi kutafuta mbinu bora za kilimo kama kilimo hakimlipi. Kwani ni nani ameenda kuwaambia vijana wanunue bodaboda, wafanye biashara Mjini, si kwa sababu inalipa? Hivi leo tunahitaji kuwambia wakulima wakalime? Tuwape soko wakulima watakwenda kulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkulima yeyote akishajua tangawizi inamlipa, mahindi yanamlipa, kahawa inamlipa huhitaji kwenda kumfundisha kulima atakutafuta mwenyewe, atakuambia nifundishe namna ya kulima mahindi, atakutafuta mwenyewe atakuuliza umwambie mbolea iko wapi. Leo tunawaweka wananchi wetu wakulima katika mazingira magumu sana, Madaba na maeneo mengine masikitiko ni makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea na hoja yangu nimshukuru sana Waziri na Ofisi yake Wizara ya Kilimo wamenisaidia sana, mwaka huu nilikuwa napoteza Ubunge Mabada kama suala la mbolea lisingezingatiwa. Ucheleweshaji ulikuwa mkubwa, wananchi wamelalamika lakini nakushukuru Waziri ulinisaidia na timu yako ya Katibu Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la soko la mahindi Serikali inajaribu kulitatua lakini bado halijapatiwa ufumbuzi. Mwaka 2015/2016 tulikuwa na ziada ya tani milioni 2.6 Serikali ilinunua tani 22,000 tu, mwaka uliofuata tani milioni tatu ziada Serikali ilinumnua tani 62,000 tu za mahindi. Mkoa wa Ruvuma hapa nina taarifa aliyopewa Waziri Mkuu alipokuja, tulizalisha ziada ya mahindi/nafaka tani milioni 1.4, ilinunuliwa tani 10,000 tu, tunakwenda wapi? Wakulima hawa wote mahindi haya wameyapeleka wapi? yameharibika, wameendelea kuwa maskini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya kuzingatia muda nitakwenda moja kwa moja kwenye ushauri. Mheshimiwa Waziri azingatie mambo yafuatayo:-
Moja, sera ya kilimo inataka mambo manne nchi yoyote, nenda Marekani, nenda nchi zozote za Kusini mwa Afrika, Kenya na kokote sera yoyote ya kilimo ina mambo manne ambayo ni safety, security, sufficiency na quality ya maisha ya mkulima. Mheshimiwa Dkt. Tizeba hili naamini unalizingatia na tunaomba sana ulizingatie. (Makofi)
Pili, sera yoyote ya agricultural trade, sheria zote za mipakani zilenge kulinda maslahi na maendeleo ya wakulima ndani ya nchi yako ndipo utapata haya yote unayotaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaenda haraka haraka. Ilani ya Chama cha Mapinduzi imetoa mapendekezo juu ya ufumbuzi wa tatizo la soko la mahindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja imesema katika ukurasa wa 12, tuanzishe soko la mazao sasa commodity exchange kwa maana ya kwamba wakulima wetu wanapoingia shambani wawe na uhakika wa soko. Leo Sudan hawana chakula, Uganda na Tanzania tunapishana misimu ya kulima, Kenya wanahitaji mahindi ya Tanzania leo tunasema tunawanyima mahindi wakati mahindi yanaoza Madaba. Ilani ya Chama cha Mapinduzi imetoa muongozo kwenye eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili imependekeza NFRA iwe na kitengo cha kununua mahindi, inunue mahindi ya hifadhi lakini inunue mahindi ya kutosha kwa ajili ya kutafuta soko la nje. Kama tunataka ku-control inflation, kama tunataka tu-control food security basi NFRA apewe hayo majukumu, leo amepewa bilioni 15 badala ya kupewa shilingi bilioni 86, shilingi bilioni 15…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)