Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii inachangia zaidi ya asilimia 30 ya pato la Taifa na inaajiri zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania na inachangia asilimia 65 ya malighafi viwandani. Cha kushangaza ni asilimia 0.52 ya bajeti kuu ya Serikali na imekuwa ikishuka kila mwaka wa bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mbunge wa Mkoa wa Tanga na Mkoa wa Tanga tunalima mazao mbalimbali lakini mazao makuu ni mahindi, mihogo, machungwa, viungo na michikichi. Naomba Waziri atakapokuja atoe maelezo katika mambo yafuatayo:-
(i) Zao la machungwa limeingiliwa na wadudu. Wakulima wanalima kwa gharama kubwa, mfano mzuri wakulima wa Wilaya ya Muheza wanauza machungwa kwa bei ya hasara ya shilingi 40. Je, Waziri ana mkakati gani wa kusimamia soko la machungwa na dawa kwa ajili ya magonjwa yanayokumba zao hili?
(ii) Zao la minazi (Pangani) linasumbuliwa na wadudu, hivyo kufanya wakulima kupata hasara sokoni na mazao kukosa ubora unaotakiwa sokoni.
(iii) Katika Mkoa wa Tanga, Serikali ya Mkoa na Wilaya zake tulikubaliana kuwezesha wakulima wa zao la mihogo. Je, Serikali ina mkakati gani kuandaa soko kwa wakulima hawa pindi inapofika kipindi cha mavuno? Je, ni mpango gani wameuandaa kuhusu dawa ili kunusuru zao hili?
(iv) Zao la michikichi Tanga (Muheza), Kata ya Magoroto kuna estate kubwa ya shamba la michikichi lakini shamba hili halina faida kwa wakulima na viwanda vya kukamulia vimekufa. Je, Serikali ina mkakati gani wa kufufua zao la michikichi ili kukabiliana na upungufu wa mafuta ya kupikia nchini, hasa kuhamasisha wakulima wadogo wadogo kuendelea kulima michikichi na kufufua kiwanda?
(v) Chuo cha Kilimo cha Utafiti Mlingano kilikuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima wa Mkoa wa Tanga na Tanzania kwa ujumla. Chuo hiki kimesahaulika, wakulima wanapambana na magonjwa kwenye mazao mbalimbali hasa michungwa, viungo, mihogo na michikichi. Naomba
Waziri aje atuambie mpango mkakati wa Wizara katika chuo hiki hasa wataalam na vitendea kazi.