Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ENG. RAMO M. MAKANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana timu nzima ya Wizara ikiongozwa na Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu kwa kazi nzuri mnayoendelea kuitekeleza Wizarani ili sekta ya kilimo iendelee kuwa miongoni mwa sekta kiongozi katika kuchangia uchumi wa Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa zinaonesha kuwa kuna uhaba wa Maafisa Ugani kwa viwango vikubwa. Ni vema kwanza Serikali ikaandaa kanzidata (database) ili kujua idadi na ujuzi walionao wale wachache waliopo kwa madhumuni ya kuandaa mkakati kutatua tatizo, skills maalum kwa maeneo maalum, idadi kulingana na mahitaji ya kila eneo, kipaumbele kwa maeneo yenye umuhimu kimkakati; kwa mfano katika uzalishaji wa mahindi the big four regions, na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mifano ya uhaba mkubwa wa Maafisa Ugani (Sera ya Afisa mmoja kila kijiji), katika hotuba ya bajeti ukurasa 47 Mkoa mzima wa Kagera, licha ya kuwa mkoa wenye shughuli kubwa na nyingi za kilimo, inao Maafisa Ugani 548 tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Tunduru yenye mahitaji ya Maafisa Ugani 227 inao 72 tu, sawa na asilimia 32. Hali hii inasababisha changamoto nyingi kama wakulima kutojua viuatilifu sahihi, viwango na matumizi sahihi. Pia aina za udongo katika maeneo na mazao yanayofaa kustawishwa na kadhalika. Wananchi wengi wanapata mavuno wanayodhani ni mengi katika eneo la ukubwa ambao wangezalisha zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viwanda, Wilaya ya Tunduru imefikia uzalishaji wa tani 20,000 za korosho mwaka 2017/2018. Wilaya ina kiwanda kimoja tu cha kubangua korosho chenye uwezo wa kubangua tani 3400 tu sawa na asilimia 17 tu. Ili kuendana na mkakati wa Kitaifa wa uchumi wa viwanda na ili kuongeza thamani na kuongeza pato kwa mkulima, Halmashauri na Taifa kwa ujumla, lengo (ndoto) ni kubangua korosho zote. Ili tufikie katika lengo la ubanguaji kwa asilimia 100 au karibu na hiyo, tunahitaji viwanda vingi zaidi kama ilivyo kwa nchi kama ya India wanaofanya vizuri. Viwanda hivi ni vidogo na vya kati vyenye wamiliki wa uwezo mdogo hadi wa kati. Viwanda hivyo vinahitaji malighafi, lakini ununuzi wa korosho ghafi unasimamiwa na Sheria ya Tasnia ya Korosho. Kanuni zake na Mwongozo Na. 1 wa mwaka 2017/2018 wa mauzo ya korosho. Sheria, Kanuni na Mwongozo huo siyo rafiki kwa utekelezaji wa hitaji hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itathmini kwa kina jambo hili.