Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

Hon. Dr. Mary Machuche Mwanjelwa

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mbeya Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naomba niseme kabisa kwamba ninaunga mkono hoja hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninamshukuru sana Jehova kwa kunifanya hivi nilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili kwa sababu hii ni mara yangu ya kwanza kwenye hotuba hii, napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mbeba maono wa Taifa hili, kwa imani yake kwangu na kuniteua ili nihudumu kwenye Serikali yake ya Awamu ya Tano katika nafasi ya Naibu Waziri, Wizara ya Kilimo. Naomba kumhakikishia Mheshimiwa Rais kuwa naendelea kumuomba Mungu azidi kunipa macho ya rohoni na kamwe nisimuangushe yeye na Taifa letu kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa napenda niwashukuru ndugu na wanafamilia yangu, hususani watoto wangu, marafiki zangu wapendwa Joseph and David kwa kuniombea na watumishi wa Mungu wote kuniinua mbele za Bwana katika kutekeleza majukumu yangu haya mapya. Aidha, napenda kuwashukuru wapiga kura wangu, Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya ambao wapo mahali hapa ukumbini na ninapenda kuwathibitishia kuwa ni ahsante, tuko pamoja na A luta continua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kumshukuru Waziri wangu Mheshimiwa Engineer Dkt. Charles Tizeba, Mbunge, kwa ushirikiano na miongozo anayonipa katika kutimiza majukumu yangu kwenye utumishi wangu wa kila siku kama Naibu Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuwashukuru watendaji Wakuu wa Wizara Engineer Mathew Mtigumwe - Katibu Mkuu Kilimo; Dkt. Thomas Kashililah, Naibu Katibu Mkuu, Watendaji wote katika Wizara, Taasisi na Mashirika yaliyo chini ya Wizara kwa ushirikiano wao katika kufanikisha uwasilishaji wa hotuba hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia nikushukuru wewe na Wabunge wenzangu wote kwa ushirikiano na ushauri mwema ambao mmekuwa mkinipa na kunitia moyo, pia bila kumsahau Mheshimiwa Spika, Naibu Spika, Mungu awabariki nyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia hoja kwa kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizochangiwa na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza naomba nitoe ufafanuzi wa baadhi ya Wabunge kuhusu TANECU. Kama inavyofahamika kwamba TANECU ina vyama vya ushirika vya mazao kwa maana ya AMCOS vipatavyo 186 vinavyojumuisha AMCOS za Wilaya ya Newala na Tandahimba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilieleze Bunge lako tukufu kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu alifanya ziara Wilaya na nilipata maombi ya kuigawa TANECU kutokana na ukubwa wa chama hicho. Aidha, msingi mwingine wa kuigawa TANECU ni ukweli kuwa viongozi wa chama hicho walihusishwa na ubadhilifu na uzembe. Hali hiyo ilibainika pia baada ya uchunguzi uliokuwa umefanywa na tume iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo Serikali kuanzia leo inaagiza kuwa Chama Kikuu cha TANECU kigawanywe ili kukinusuru chama hicho na pia katika kuimarisha ushirika. Kutokana na hatua hiyo Newala itabaki kuwa na AMCOS 53 na Tandahimba itakuwa na AMCOS 133 na Serikali inasisitiza kabisa kwamba utekelezaji wa maamuzi haya ufanyike kabla ya msimu huu kuanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali inatoa maelekezo kwa Wakuu wa Wilaya wote nchini na Wakuu wa Mikoa wote nchini kwa kushirikiana na Maafisa Ushirika wa Wilaya na Warajisi Wasaidizi wa Mikoa kusimamia mwenendo wa ushirika kwa ukaribu na kuwa ikidhihirika kuwepo uzembe wa aina yoyote katika utekelezaji wa maagizo hayo basi hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao. Ikumbuke kabisa kuwa kwamba katika utelezaji wa suala hilo Serikali haipo tayari kabisa kulipa madeni yoyote ya nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili naomba nifafanue hoja chache za Kamati na mengine Waziri wangu atayatolea ufafanuzi kwa mapana.

Katika hizo hoja za Kamati walisema kwamba hakuna bajeti ya maendeleo iliyotengwa kwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika. Naomba niwaeleze Wabunge wenzangu kwamba baada ya kukamilika kwa programu ya mageuzi na modernization ya ushirika ile ya mwaka 2015 kwa maana ya Cooperative Reform and Modernization Program, Wizara imekuwa ikiandaa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) ambapo kuna miradi kadhaa ya kuendeleza ushirika ambayo itaratibiwa na kusimamiwa na tume ya maendeleo ya ushirika lile Fungu 24.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara inaiongoza Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuandika maandiko mapya ya miradi na kuyasajili katika Wizara ya Fedha na Mipango. Kuanzia mwaka ule wa 2019/2020 tunatarajia Tume hii ya Maendeleo itaweza kujisimamia yenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, Kamati imeshauri Serikali kuchukua hatua kwa mawakala waothibitika kuwa ni wadanganyifu pamoja na maafisa wa Serikali walioshiriki kwenye udanganyifu huu. Naomba nilieleze Bunge lako tukufu kwamba katika zile hatua za awali watumishi wa Serikali wote waliohusika wameshakamatwa pamoja na vile vyombo vya dola vimeshawakamata na wamechukuliwa hatua kali sana. Kuhusu mawakala hawa uhakiki unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo Kamati imeishauri ni kwamba ni vyema midada ya zao la kahawa ikaongeza ili kuwa na wigo wa kutosha na hivyo kuwezesha upatikaji wa soko la uhakika. Naomba nilieleze Bunge lako tukufu kwamba kwa sasa minada ya kahawa inafanyika mara moja kwa wiki Mjini Moshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kahawa ikishakuwa tayari kwa mauzo katika maeneo ya uzalishaji nchini hutoa sampuli na kupelekwa Moshi kwa ajili ya mauzo kwa ushindani. Suala la kuongeza minada halileti tija kwa kuwa litaongeza gharama za uendeshaji na kupunguza ushindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya nimeongea kwa ufupi sana ili nisigongewe kengele, lakini Mheshimiwa Waziri wangu ataeleza kwa mapana na marefu na naomba niseme tena, naunga mkono hoja, ahsanteni sana.