Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa mchana huu kupata nafasi kuzungumza kidogo juu ya habari ya Wizara ya Uvuvi na Mifugo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kwanza kuzungumza juu ya habari ya mifugo ambayo Mwanza peke yake tuna kiwanda cha Tanneries. Moja ya viwanda vya mazao ya mifugo ambavyo kwa sasa havifanyi kazi na vipo ni pamoja na Kiwanda cha Nyama Shinyanga, Mwanza Tanneries na Kiwanda cha Maziwa Mara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nikuzungumza habari ya Mwanza Tanneries na nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mkuu wa Mkoa wangu wa Mwanza Comrade John Mongela kwa kazi kubwa aliyoifanya kuhakikisha kiwanda hiki kinarudi mikononi mwa Serikali. Miaka mingi kiwanda hiki watu wamekuwa wanapokezana tu hati na kuchukua fedha kwenye mabenki bila utaratibu wowote ili hali kiwanda kikiwa ni mali halali ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Mifugo kwa sababu yupo hapa wachukue jitihada na juhudi za haraka kuhakikisha viwanda hivi kwa kuwa vimerudi Serikalini vinapata wadau na vianze kufanya kazi haraka kwa sababu ndiyo malengo ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano kuhakikisha viwanda vinafanya kazi kwa maana ya Serikali ya viwanda na ajira zinapatikana kwa wingi. Pasi kufanya hivyo tutakuwa bado hatutimizi malengo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2015 - 2020 kuwasaidia Watanzania wengi na vijana kupata ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende sasa kwenye oparesheni Sangara. Operesheni Sangara, nitajikita hapo zaidi kwa sababu Sangara anapatikana katika Ziwa Viktoria peke yake. Ni ukweli usiopingika hakuna hata mtu mmoja miongoni mwetu anayepingana na zoezi zima la uvuvi haramu. Hata hivyo, nataka tu nijiulize mambo machache; tunapozungumzia uvuvi haramu leo lazima kuna watu ambao wanajulikana na shughuli yao kubwa ni uvuvi haramu peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka tu nijue na Wizara inisaidie kujua sana. Sangara hawa tunaowazungumza leo miaka ya nyuma ukija Dodoma hapa kwa kina Mzee Lubeleje walikuwa wanaletewa mapanki na vichwa. Leo Sangara huyu analiwa karibu nchi nzima akiwa nyama kama vile alivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tu kujua leo tunapozungumza uvuvi haramu na zana haramu tunazozizungumza ni zipi? Tunazungumzia kokoro, timba, baruti, sumu au nyavu za inchi nne, sita na kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana Mheshimiwa Waziri kuna vitu viwili hapa, kuna wizara na kila wizara inapokwenda kwenye operesheni aidha inapotoka liko kundi lingine la uvuvi wa operesheni kutoka kwenye Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wavuvi wamenyanyasika sana, wako watu wanatumia jina la operesheni Mpina kwa sababu tu wakisikia Mpina ameingia wanatetemeka na wanatumia nafasi hii kuwaumiza sana wavuvi hawa kupitia jina lako. Natambua kazi inayofanywa na Wizara lakini yapo maeneo inawezekana wameyaacha wazi sana, wavuvi hawa wananyanyasika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikupe mfano, nyavu ya macho 26, hii siyo haramu imeruhusiwa lakini wataalam wanajua na hata wao ukiwauliza nyavu hii tafsiri yake inavua kwenye maji madogo. Sasa kama inavua kwenye maji ya kina kifupi, nyavu hii ya macho ya macho 26 kwa nini isiende kutetekeza hicho kizazi tunachokitegemea, ombi langu turudi nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Waziri alituma timu ya utafiti kutoka TAFIRI ikafanya kazi kubwa sana na wavuvi hawa. Chama cha Wavuvi wamezunguka takribani siku 14, wamekaa ziwani, wameangalia madhara ya nyavu yenye matundu 78 na matundu 52 na kujua tatizo lipo wapi, wameleta ripoti.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri akiifanyia kazi vizuri ripoti hii itamsaidia na nyavu hizi zenye matundu 78 wanazoziita haramu na hapa mimi huwa najiuliza nyavu hii ina matundu 78, ukiipunguza mara mbili ukatoa moja ukatoa mbili inabaki 26 inakuwa siyo haramu, haramu haiwezi kuwa halali hata ukiigeuza vipi. Tuweke utaratibu mzuri ambao Wizara mnafanya na leo najikita sana kwenye kushauri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwanza tunayoiona leo nataka niwaambie haijajengwa na dhahabu na kitu kingine chochote, imejengwa na wavuvi hawa. Ukichukua ajira, ajira ya wavuvi wanaotega, wavuvi wamiliki wenye mitumbwi, ukachukua na ajira zilizopo kwenye viwanda, hawa wategaji na wavuvi wa kawaida ni wengi kuliko ajira za kwenye viwanda. Kwa hiyo, hii ni sehemu nyingine ya kiwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri tusimame sana, gharama za uvuvi zimepelekea wachuuzi wa bidhaa za uvuvi zimekwenda juu. Leo imeongelewa hapa boya moja la Sh.200 sasa hivi linauzwa Sh.400, lakini ukizungumza kamba iliyokuwa inauzwa laki moja na nusu, leo ipo mpaka laki mbili na themanini. Ni kwa sababu watu wajanja wachache wanatumia mwanya huo wa operesheni kujinufaisha wao na kuumiza wavuvi. Lawama zote zinazopigwa leo zinarudi kwenye Serikali ya Mheshimiwa Waziri. Kwa hiyo, nataka niombe Mheshimiwa Waziri ashughulike na watu ambao hawataki kututendea mema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utafiti uliofanywa unaonesha kabisa kwamba ziko aina ya nyavu hazina madhara kama zitatumika kuanzia kwenye maji ya kina kirefu na maeneo mengine kwa sababu nyavu hizo zinaonekana zinawasaidia watu hawa. Ukirudi leo ukizungumzia masuala ya faini ambayo watu wengi kweli wamepigwa faini na nimekuwa najiuliza, akitoka Mheshimiwa Waziri, kinaenda chombo kingine kinakwenda kufanya operesheni ya Wilaya na hiki ndicho kinachokwenda na ubabe wa hali ya juu, haujawahi kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nitoe mfano, mtu ameenda kwenye kisiwa kimoja Goziba au Ilubwa kule akaenda kuvua amekaa kule siku 16 anasubiri samaki, ameondoka na barafu kutoka kwenye kiwanda Mwanza, amesafiri siku nzima kesho yake amefika ameanza kusubiri kununua samaki. Siku anarudi na samaki wake ameweka barafu, ile barafu kwa pale juu kadri ya siku alivyokaa inaanza kuyeyuka kushuka chini polepole, akikutana na Afisa Uvuvi kule ziwani anamwambia mbona barafu hakuna samaki ameonekana mgongo, anapigwa faini na anapewa masaa 24. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa watu hawamtakii mema Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya. Naamini kazi hii ikifanywa kwa weledi mzuri na style nzuri baada ya miezi michache ijayo Mwanza tunazungumza dhahabu ya pamba itakuwa Ziwa Viktoria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi unawezaje kumpiga faini mtu ambaye unaona tu mgogo wa samaki umeelea juu, kwa sababu barafu imeyeyuka. Mtu huyu akifika kiwandani hakuna Sangara anayeoza, akifika kwa mwenye kiwanda, mwenye kiwanda atachukua samaki anaowataka. Wale wengine ndiyo maana wanatengeneza kayabo, wanakwenda kuuzwa nchi za jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niwaombe sana Maafisa wa Uvuvi wawe wanaangalia na wao ni wataalam wanajua misingi thabiti ya jambo hili kubwa wanalolifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ninalotaka kuchangia, Mji wa Mwanza biashara zake zote, kwa mfano leo dizeli haiuzwi, petroli haiuzwi kwa kiwango hicho kwa sababu wenye mahitaji haya ni hawa hawa. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri na jambo lingine kubwa tufanye mkakati kama Wizara na Serikali, tumekuwa tukifanya sana huko na tumesikia asubuhi hapa masuala ya bahari kuu vinatafutwa vifaa vya uvuvi na kadha wa kadha kwenye bahari kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri hapa amejibu vizuri, lakini hebu tujiulize wavuvi wa Kanda ya Ziwa wanapokwenda ziwani kuvua wanatumia fikra zao, wanabuni, wanahisi sehemu fulani leo kunaweza kuwa na samaki wengine wanaweza kuwa wanafuata mwezi, wanahisi au wanaweza kuwa wanabashiri ni wapi samaki watapatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yake Waziri, Mheshimiwa Mpina itengeneze sasa utaratibu, ifikirie mpango thabiti wa kuwasaidia wavuvi wa Kanda ya Ziwa ili na wao wawe na vifaa; wanapokwenda kule kwenye maji wawe na uhakika nakwenda na nyavu yenye matundu kadhaa, ninapokwenda kutupa nyavu ndani ya masaa sita nitakuwa nimepata samaki ninaowahitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wavuvi hawa anaweza kuwasha boti kutoka kwenye kisiwa akafika mpaka ziwani, akaishia kilo mbili amechoma mafuta ya gharama akarudi akakutana na operesheni hata zile kilo mbili akanyang’anywa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, yeye bado kijana ana uwezo mkubwa wa kufanya kazi hii na akabaki kwenye historia kukumbukwa kwenye Taifa hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Hivi tunavyokwenda Wizara inaweza ikatusaidia sana kuhakikisha wavuvi na wafugaji katika Taifa hili wanabaki salama, lakini anaanzsiha vitu ambavyo vitakuwa na historia kubwa, vitamjenga ataacha legacy kwa wavuvi hawa. Mheshimiwa Waziri asimamie watendaji wasiokuwa waaminifu wanaendelea mpaka kesho. Leo wanasema ukifika kwenda kukamata operesheni kabla hujakamatwa umeona boti, unatupa kwanza bomu na hii imetokea na taarifa ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, tusimame kwenye misingi ya kulisaidia Taifa hili. Narudia tena miezi michache ijayo Ziwa Viktoria itakuwa na dhahabu ya pamba kama hatutawanyanyasa watu hawa na kupora mitaji yao kwa namna ambavyo inatupelekea kubaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.