Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Haya majina ya Waheshimiwa haya yanatuvimbisha vichwa wakati mwingine, kuna watu wakiitwa jina inawezekana ukapata ujumbe vizuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri alikuja Ukonga katika mnada wa Pugu na akajionea hali ya shida iliyopo na ugomvi wa mnada ule na wananchi wanaozunguka eneo lile Mtaa wa Banguro. Nimeona kwenye ukurasa wa 40 amelizungumzia hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri anisikilize. Eneo la Banguro ni kweli kwamba Wizara yake ina hati ya mwaka 1939, lakini vilevile wananchi wenyewe walipewa hati ya Kijiji na Mheshimiwa Rais wa Kwanza wa nchi hii, Julius Kambarage Nyerere ya mwaka 1976 na wamejenga shule, wana zahanati, shughuli za maendeleo zinaendelea katika eneo lile. Kuna hekari 4,800 na wameshachukua hekari hizo zote karibu 4,162 anazo 108. Alipozunguka alikuwa anaoneshwa beacons ambazo ziko kwenye Miji ya watu na huduma za Kijamii.
Mheshimiwa N aibu Spika, ushari wangu ni kwamba, kwa kuwa wananchi walipewa hati na Serikali na hati ya kwanza ni ya mwaka 1939, hati ya pili ya mwaka 1976, automatically hii hati ya mwisho imefuta ile ya kwanza na ndiyo maana wamefanya shughuli za kimaendeleo, kuna zahanati pale wanajenga, shule ipo na watu wanaishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ningeshauri kwa sababu kuna hekari zilizobaki 108, kama alivyosema abaki na hizi kwa maana ya kuimarisha, lakini ikimpendeza sasa hivi ule mnada uko mjini, kuna maeneo hata hapa Ruvu makubwa tu, mapori makubwa ng’ombe wanahitaji maji, wanahitaji majosho, wanahitaji mabwawa, wanahitaji huduma mbalimbali katika eneo hilo, kule Dar es Salaam anapaswa alete tu nyama, hawa ng’ombe wanaweza wakatoka kwingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mheshimiwa Waziri hataki kwenda Ruvu, pale Zingiziwa tuna hekari 70, ni nje ya Mji, anaweza akapeleka hiyo huduma katika eneo lile. Kwa sasa wananchi wale kwa kweli wamepata sintofahamu, hawafanyi shughuli za kimaendeleo, wanaambiwa watafukuzwa kesho, watabomolewa kesho, kwa hiyo, natarajia katika mazungumzo yake na kwa sababu aliunda timu itakuwa imemshauri vizuri kwamba wale wananchi kwa sababu walipewa na Serikali na wana leseni za makazi, wengine wana hati miliki kama alivyojionea. Kwa hiyo, ningeshauri kwamba kauli yake itoke ili wapate amani katika maisha yao, waweze kujiendeleza, wasikae kwa wasiwasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pale Pugu Station wananchi wamevunjiwa nyumba kutoka Gongo la Mboto, kuja Ukonga, kuja Pugu mpaka Pugu Station. Tena sasa inakuja hofu tena ya mnada wa Pugu, kwa kweli hawawatendei haki wale wananchi. Ni muhimu ili watu wafanye shughuli za kimaendeleo na za kiuchumi wapate fursa na kauli ya Serikali ili waweze ku-settle na wajiendeleze. Hilo ni jambo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri mradi ule aliuona, katika eneo lile hakuna hata uzio, ndiyo maana kuna ugomvi kati ya wananchi na Wizara ya Mifugo na kuna malalamiko. Pale wanahitaji maji, wanahitaji uzio, ng’ombe wanaokufa juzi ameona wamekamatwa. Nilimwambia siku ile ng’ombe wanaokufa kwanza kuna tundu la kuchomwa ile mifugo ili wateketezwe, lile limeharibika na ile ya kuchimbia ile mifugo haipo, hivyo wanatupwa kule bondeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakitupwa kule bondeni, watu wanazunguka, wanachukua mizoga, wanachinja, wanaingia mtaani, watu wanakula mizoga iliyokufa, ile ambayo wamekamata juzi ni michache. Ukweli ni kwamba ng’ombe wanakufa na watu wanakula vibudu pale kwa sababu hiyo. Kwa hiyo nadhani hilo nalo Mheshimiwa Waziri alishughulikie.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kule Dar es Salaam tuna machinjio mbili, ile ya Vingunguti lakini na ile ya Mazizini. Mazizini ni machinjio ya mtu binafsi kwa hiyo hata Halmashauri inashindwa kuiboresha. Kwa hiyo, wananchi wa Mazizini wanapata shida, kuna maji machafu nilishamwambia na Mheshimiwa Naibu Waziri anajua. Maji yote ya ng’ombe wanaochinjwa pale, damu zote zinaingia mtaani. Kwa hiyo, ile sehemu wakati wote wa majira ya mwaka ni kipindupindu na magonjwa ya kuhara. Tumewaambia, tumelalamika mara nyingi walishughulikie, kama wanachukua kodi, waboreshe maeneo ya kufanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyabiashara hawa wa ng’ombe wanalalamika wana leseni mbili; kuna leseni ya kutoka kwenye mnada na akifika tena machinjioni analipa tena leseni nyingine. Bahati mbaya wale wafanyabiashara wanazuiliwa kuonana na viongozi yaani umoja wao, viongozi hawakutani nao ili wawaambie kero zao. Wanazuia hata ng’ombe ambao wanachinjwa hawajui idadi, wanadhulumiwa. Wanasema wale Madaktari, machinjio yote hata hii ya Kizota hapa Dodoma na nyingine Dar es Salaam, ng’ombe wanaochinjwa wale jamaa wanasema wanaibiwa nyama kwa sababu hawawezi kuhakiki. Kwa hiyo, hili nalo naomba Mheshimiwa Waziri alishughulikie lipate ufumbuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kumekuwa na shida mwenzangu amezungumza hapa asubuhi kwamba, ukihamisha mfugo kutoka eneo moja kwenda lingine unalipa kodi, hizi kodi si ndiyo Rais alisema kwamba ni Rais wa wanyonge ataziondoa, kulipwe kodi moja ambayo inaeleweka, leseni iwe moja, waiunganishe ili kuondoa usumbufu na kuondoa mianya ya rushwa na kuwasumbuasumbua watu. Vikodi kodi vingi vingi hivi kila mahali watu kwa kuwa wajanja wameingiza mikono yao na wafanyabiashara kimsingi hawanufaiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri kwa kweli ni mtu wa Kanda ya Ziwa na mimi nimeolea kule Nyakabindi kule Bariadi, yeye ni mfugaji, ni mkulima, kwa kweli siyo haki wakulima wa nchi hii, yaani mkulima analia, mvuvi analia na nyama tunaitaka. Haiwezekani wameendesha operesheni nyingi zimewaumiza watu sana. Operesheni Tokomeza walikuwa wanachukua ng’ombe, wanachukua miti wanawachomeka kule nyuma mpaka mtu anatoka utumbo, ni very unfair Mheshimiwa Waziri, siyo sawasawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, wafugaji hawa wanazunguka nchi nzima yaani Mmasai akionekana mahali ni kama mnyama, Msukuma watu wanatuchukia. Wameleta ugomvi kati ya wafugaji na wakulima. Watenge maeneo, ng’ombe apewe heshima yake, watengewe maeneo ya wafugaji ili tuondoe ugomvi kati ya wakulima na wafugaji. Nilitarajia Waziri aje na hiyo suluhu.