Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Itilima
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia jioni ya leo. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake na Watendaji wote wakiongozwa na Katibu Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanya kwa kuteua Majaji ili kesi zisiwe na mlundikano kwenye Mahakama zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie suala la wafugaji. Wafugaji wetu wameteseka sana hususan wanaoishi maeneo ya kando kando ya hifadhi. Mheshimiwa Rais alipoteua Majaji na Majaji hawa wanafanya kazi nzuri sana na kiapo chao walichoapa watatoa hukumu kulingana na mazingira ya maeneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Wilaya yangu ya Itilima kuna wafugaji walikuwa wamehukumiwa na mifugo yao ikataifishwa; ng’ombe 339 lakini Mahakama Kuu ikaamuru ng’ombe wale waachiwe na wale watuhumiwa waachiwe, lakini cha ajabu mpaka leo wale ng’ombe hawajaachiwa lakini watuhumiwa walishaachiwa. Sasa Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana angetueleza yeye kama msimamizi wa wafugaji, anatusaidiaje wafugaji ambao tunaendelea kuhangaika, lakini kabisa azma ya Serikali Awamu ya Tano ni kuhakikisha inakomboa wanyonge na hususan mambo haya yapo kisheria na Kimahakama zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wakati anatoa hotuba yake alisema baada ya mamlaka kumruhusu vibali vya Kimahakama aliweza kuteketeza nyavu, lakini sasa baaadhi ya vyombo vyetu, Mahakama imeamuru ng’ombe warudishwe lakini bado wamezuiliwa na mpaka sasa na ng’ombe wanaendelea kufa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba katika majumuisho yake Mheshimiwa Waziri atusaidie, ni kwa nini mambo haya yanaendelea katika maeneo yetu hususan kwa wakulima na Serikali ya Awamu ya Tano ni ya wanyonge na wakumbuke ng’ombe hawa ni wa wafugaji maskini lakini ndio matajiri wakubwa ambao wanatuwezesha humu ndani sisi sote tukiamka asubuhi tunakunywa supu, tukiamka asubuhi tunataka nyama, maziwa na vitu vingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kulisema, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Mbunge aliyemaliza kuzungumza katika suala zima la ng’ombe. Mheshimiwa Waziri anaelewa kabisa kwamba maeneo yetu bado hatujawa na miundombinu mizuri katika minada yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na changamoto kubwa, mnunuzi amenunua ng’ombe wake watano na tunafahamu kabisa wafugaji wetu au wakulima wetu anaweza akauza mazao yake anaamua kwenda kununua ng’ombe au ametoka machimboni akanunua ng’ombe wake hata 10, 20. Akikutana na wale jamaa, anaambiwa huruhusiwi kuswaga ng’ombe zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hii wangetusaidia sana kuweka miundombinu katika maeneo yenu mazuri. Nia ni ya dhati na kazi zao wanazofanya ni nzuri sana, wanalinda rasilimali zetu za nchi lakini namwomba Mheshimiwa Waziri achukue huu ushauri akaufanyie kazi ili kusudi tuondokane na adha hizi ambazo zimejitokeza katika meneo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa mipango yake mizuri aliyoilekeza katika ukurasa wa 15 na 12 kuhakikisha Kiwanda cha Nyama cha Shinyanga, kinarudishwa na kinafanya kazi katika maeneo yetu. Hongera sana, hiyo akiifanya litakuwa jambo zuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambasamba na hilo, atusaidie katika eneo liliko Maswa Shishiu ekari 10,240 hazina kazi. Sasa hiyo ni sehemu mojawapo ya kutatua baadhi ya changamoto za wafugaji. Ikiwezekana maeneo haya basi tuwape wafugaji waweze kulifanyia kazi kuliko eneo lipo tangu tupate uhuru lakini halina kazi, yanazidi kupoteza muda. Tukiwapa Watanzania na wafugaji wataweza kutusaidia sana kuongeza kipato cha Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa ambayo ameifanya. Amebeba dhamana mpaka ya kuhakikisha analinda rasilimali na mapato ya nchi yaweze kuongezeka. Ushauri wangu ni kwamba wavuvi wamelalamika lakini wanatoa mchango kwa kuunga hoja zake anazozileta, lakini sasa kwenye suala zima la upatikanaji wa vitendea kazi, kiwanda cha Arusha kinaonekana kimezidiwa. Baada ya mwezi mmoja au miwili zile nyavu zinaharibika.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni jambo jema sana Mheshimiwa Waziri akalichukua na kulifanyia kazi. Kuna Kontena za watu ziko bandarini ambazo tayari zimeshaingia hapa nchini. wangetumia ule utaratibu wa kawaida wakazifanyia uchunguzi, hawa wavuvi wakapatiwa zana hizo wakaendelea kufanya kazi yao kubwa na nzuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka Mheshimiwa Rais alipokuwa akizindua kampeni yake Jangwani, alisema anataka nchi ya viwanda, lakini pia anataka Watanzania wasipate shida. Uzuri Mheshimiwa Waziri amepewa dhamana hii ya kusimamia. Naomba sana pamoja na waatalam waliangalie kwa mapana zaidi ili kusudi wakulima na wafugaji waendelee kufanikiwa katika kutimiza azma ya Serikali yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, nampongeza Katibu Mkuu. Tena bahati nzuri Mheshimiwa Waziri amepewa Katibu Mkuu mwanamama na mwanaume. Kwa hiyo, una sehemu kabisa nzuri za kulelewa vizuri na akafanya kazi yake vizuri sana na kuhakikisha Watanzania wanapiga hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, naunga mkono hoja. Ahsante sana.