Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Dr. Immaculate Sware Semesi

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi, na mimi niweze kutoa maoni yangu katika hoja iliyopo mezani.

Mheshimiwa Spika, nitaanza kwa sekta ya uvuvi. Naanza na sekta ya uvuvi kwa masikitiko makubwa sana kwa sababu ni sekta ambayo inaweza ikalitoa Taifa hili katika hali ya uchumi uliodorora tulionao sasa hivi. Sekta hii Mwenyezi Mungu ametujalia rasilimali ambazo tunaweza tukazitumia, tuna maziwa makubwa matatu hapa nchini yenye kilometa za mraba zaidi ya 54,000; Victoria, Tanganyika na Nyasa.

Mheshimiwa Spika, tuna maziwa size ya kati na madogo zaidi ya 45; tuna mito mikubwa mingi, mizuri zaidi ya 20 na kitu; tuna Ukanda wa Pwani wa Bahari wa kilometa 1,420 na ukanda huu ndani ya maji ambayo wavuvi wetu wanavua zina kilometa za mraba 64,000 na ukanda wa uchumi EEZ wa zaidi ya kilometa za mraba laki mbili na kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, rasilimali zipo, viumbe ambavyo tunaweza tukavivuna au kuvifuga vipo, wavuvi na wanaofanya shughuli za uvuvi wako zaidi ya milioni nne, wavuvi wenyewe wako 200,000 na zaidi. Sasa ukiangalia rasilimali watu tulionayo na rasilimali zenyewe za uvuvi tulizonazo haziendani na tunachokipata. Maduhuli ya mwaka 2017 yaliyokusanywa na Wizara kwenye sekta ya uvuvi ni shilingi bilioni 21 tu. Nina uhakika pia kwamba shilingi bilioni hii 21 imeongezeka kwa sababu ya shilingi bilioni sita tuliyoipata kwenye operation sangara.

Mheshimiwa Spika, Wizara hii bajeti yake kubwa yote ni shilingi bilioni 14 tu, lakini iliyoenda hii bajeti inayoishia mwaka 2017/2018 ni asilimia 52 tu. Bajeti ya maendeleo iliyotengwa katika sekta hii ilikuwa ni shilingi bilioni mbili, lakini kwa miaka mitatu yote iliyopita inasomeka sifuri kwenye vyanzo vya ndani. Sekta ya uvuvi sasa hivi wakisema wanafanya chochote cha maendeleo, basi ni katika mikopo ya Benki ya Dunia kwenye Mradi wa Sio Fish, lakini kama Taifa hatujawekeza katika sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia mifugo na uvuvi kwa ujumla wake tunachangia katika pato la Taifa asilimia saba na kitu. Asilimia 5.6 inatoka kwenye sekta ya mifugo na asilimia 1.9 inatoka kwenye uvuvi, lakini ukiangalia hata hiyo mifugo yenyewe haijapewa kipaumbele japokuwa ina- contribute more hata kuliko kwenye sekta ya madini ambayo ina-contribute 4.5 nafikiri katika pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia uwekezaji jinsi ulivyo mdogo, tunasema kwamba kuna changamoto katika uvuvi, tunaenda kwenye ufugaji (aquaculture) lakini kitengo hiki kilitengewa shilingi milioni 800 tu katika kuhakiksha Aquaculture inakua nchini na imepata sifuri na haikuweza hata kukusanya maduhuli yoyote, inasomeka sifuri.

Mheshimiwa Spika, tangu miaka ya 1990 au 1980 tulikuwa tuna viwanda takribani 18 vya uchakataji wa mazao ya samaki. Tunapoongea sasa hivi, tuna viwanda nane tu, vingine vyote vimefungwa. By then katika viwanda 18 walikuwa wameajiri wafanyakazi 4,000 na zaidi na walikuwa wana-produce tani 1,000 na kitu za samaki. Sasa hivi viwanda vya samaki vimeajiri watu chini ya 1,000 na wana-produce tani chini ya 200, nafikiri ni tani 170 za samaki.

Mheshimiwa Spika, niende moja kwa moja kusema kwamba kumekuwepo na kilio kikubwa sana katika usimamizi wa rasilimali hizi za uvuvi ambazo tayari hatuzipi vipaumbele. Serikali ilianzisha mchakato mzuri kabisa kupitia sera yake ya 1997 ya uvuvi ya kutengeneza hivi vikundi vya usimamizi wa rasilimali za uvuvi yaani BMUs. Sasa hivi nchini nafikiri tuna BMUs 700 na kitu. Vikundi hivi katika upande wa Pwani pamoja na Ziwa Victoria, vimeterekezwa na Serikali. Kazi mahususi ya vikundi hivi ilikuwa ni kujisimamia wenyewe na kusimamia kazi za kulinda rasilimali hizi za uvuvi.

Mheshimiwa Spika, tumeshindwa kugatua madaraka kwamba Wizara husika iachie TAMISEMI isimamie BMUs kama ilivyo kwenye sheria tuliyojiwekea wenyewe namba 22 ya mwaka 2003 ya Uvuvi. Badala yake kumekuwa na mkanganyiko wa nani asimamie rasilimali za uvuvi wakati Halmashauri husika through TAMISEMI ndiyo walitakiwa wasimamie hao wavuvi wadogo wadogo wakiongozwa na BMUs?

Mheshimiwa Spika, sasa tumeona kumekuwa na matukio ya kutokujipanga vizuri kwa Serikali na kuanzisha hizi operation za papo kwa hapo ambazo zinaleta gharama kubwa sana katika utekelezaji wake na kuwaumiza wale wananchi, wakati tungekuwa na zile BMUs tungeziwezesha na kutoa elimu, basi hawa BMUs wangeweza kuzilinda hizo rasilimali na kuleta tija katika sekta hii ya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano mzuri tu ni katika Halmashauri ya Pangani, walikuwa wanatumia mawakala kukusanya mapato ya uvuvi. Walikuwa wanakusanya takribani milioni 25,000, lakini Halmashauri hii ya Pangani ilihusisha BMUs na wakawatumia hao BMUs kama mawakala na sasa hivi wameweza kukusanya mapato ya shilingi bilioni 140 na kitu, yaani ime-triple the amount.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tukiwawezesha, siyo tu wanaweza kuingiza fedha za Halmashauri husika na kujiwezesha na wenyewe pia kujifanyia shughuli zao, lakini pia wanalinda zile rasilimali za uvuvi. Sasa kwa nini hatuwi na hii mikakati ambayo tumejiwekea ambayo ni endelevu na iko tangible? Badala yake tunakurupuka na operesheni ambazo zinaleta vilio. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini nimesema tunakurupuka? Mbele yangu hapa, hii barua nafikiri nakala imekufikia, ni kutoka kwenye Chama cha Wavuvi wakiomba Bunge liingilie kati kwenye Operation Sangara na nina-quote machache waliyoyaandika. Wanasema ili kupata uhalisia wa mambo tunaomba kukutana na Kamati husika tuzungumze nayo, lengo likiwa ni pamoja na kuundwa Tume ya kutembelea na kuzungumza na wavuvi kwenye maeneo husika, hivyo kubaini hali halisi ya matokeo ya operation hizi.

Mheshimiwa Spika, ni kama ilivyokuwa kwenye Operation Tokomeza, yaani ya majangili, miaka ya nyuma Bunge na Umma walipata kujua uhalisia wa matokeo ya operesheni hiyo na matukio mengine baada ya Bunge kuunda Tume na kurejesha ripoti zake Bungeni.

Mheshimiwa Spika, sidhani kama wavuvi wamejitungia, ndiyo maana wamekuwa na uwezo wa kuja hapa Bungeni kutoa kilio chao kwamba hiyo operation ilivyoendeshwa imeleta madhara makubwa sana, kwa sababu baadhi ya maeneo wametumia nguvu za ziada, risasi za moto, mapanga na mabomu. Wameleta madhara makubwa sana.

Mheshimiwa Spika, hatukatai, mimi kama mwana mazingira sikatai kuhusu kutunza mazingira au kuleta operation special kwenye maeneo ambayo ni sugu ya uharibifu wa mazingira. Ila ni njia na mikakati gani tunayoitumia ili zilete uharibifu?

Mheshimiwa Spika, mfano tu mzuri ili tuweze kwenda sawa, traffic akikamata gari au basi lenye abiria akamkuta dereva hana leseni au amebeba mzigo siyo au amezidisha idadi ya abiria, nini kinafanyika? Anampa faini au anaenda mahakamani.

Mheshimiwa Spika, sasa kwenye uvuvi, mvuvi anapokamatwa kama ametenda kosa, labla hana leseni au amevua samaki kwa kutumia nyavu sizo, basi huyu mvuvi atatozwa faini, watataifisha zile mali na wanachoma moto mtumbwi au boti. Traffic ana uwezo wa kuchoma gari moja kwa sababu umevunja sheria? Traffic anataifisha gari kama umevunja sheria? Basi haya ndiyo yaliyotokea katika Operation Sangara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nia na lengo la Wizara inaweza ikawa nzuri lakini utekelezaji wake umeleta maafa makubwa zaidi kwa wavuvi hawa. (Makofi)

Kwa hiyo, naliomba Bunge lako liunde Tume kama walivyoomba hawa wavuvi, waangaliwe kwa jicho cha ziada ni nini kimetokea ili tupate kujifunza kwa operesheni zijazo, kwa sababu najua wanaenda operation namba mbili sijui au ni namba tatu, liangaliwe hivyo hivyo katika operesheni nyingine zitakazokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kumeletwa mbele yangu kilio kutoka kwa wavuvi, Chama cha Wavuvi vilevile wakihusisha operation hii na upatikanaji wa nyenzo za kuvulia. Sasa hivi nyenzo hizi kama vile nyavu na maboya yamekuwa ya bei juu sana kwa sababu ya kutokuingizwa au na baadhi ya hizi nyenzo zimezuiwa kuingizwa katika border ya Sirali. Kwa hiyo, wanaomba nyavu hizi ziwe available na ziweze kupatikana na kwa bei ile ambayo inaleta tija katika Taifa.

Mheshimiwa Spika, niliongelee jambo lingine lililoletwa mbele yangu ambalo ni Sheria ya Uvuvi. Wadau wakuu wa Sheria ya Uvuvi ambao ni wavuvi wenyewe, wanalalamika kwamba hawajahusishwa katika kuirekebisha sheria hii mpya ambayo inakuja soon mezani kwako, wapate kuzingatiwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache, nashukuru na mengine nitaandika kwa maandishi.