Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii nichangie Wizara hii ambayo kwa kweli tuna majonzi sana. Nashukuru sana leo umekaa hapo mbele, ni bahati. Kwa nini, nianzie na msemaji wa sasa hivi ambaye amepita.
Mheshimiwa Spika, kuunda Tume ya Bunge kwenda kuangalia matatizo na madhara yaliyowakuta wafugaji na wavuvi haiepukiki. Kwa nini? Wavuvi wa Tanzania leo wako kwenye utumwa, kwa sababu ni watu ambao wanaishi. Nataka kutoa mfano kidogo. Ukienda Ukerewe ni kisiwa, lakini kuna Kisiwa kidogo Kulazu, kuna Kisiwa kingine Kweru, kuna Irugwa, Liegoba, kuna Burara, ukienda Bukoba kuna Bumbile, kuna Gozba na Msira. Hawa watu wanaishi visiwani, maisha yao ni kuvua samaki tu. Wamelea watoto, wamesomesha watoto, wana ma-degree, ni samaki peke yake, hawana kitu wanachojua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hawa watu leo ni kilio siyo kidogo, ni kikubwa. Watu wamejinyonga na kupigwa risasi kwenye operation. Hii hatari ni kubwa. Wana-CCM wenzangu niwaambie, tutaenda kuomba kura sisi, tunaombaje kura hawa watu wanaoteswa hivi kwa operation ya ajabu hii? Operation zimeshafanyika nyingi, katika Bunge hili tunaona haiwezekani utu wa mtu ukaharibika kwa sababu Mheshimiwa Mpina ni Waziri. Huo Uwaziri hauwezi kuwa mtu mmoja halafu CCM ikashindwa kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika hili Tume haiepukiki. Nina imani Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi haijamwagiza Mheshimiwa Waziri afanye hivyo na haiwezi kumwagiza hivyo. Chama cha Mapinduzi ni chama cha watu, Rais wetu anajinafsisha, anaongelea wanyonge, wanyonge wa Kanda ya Ziwa, wa Pangani, Mtwara, Mafia wanaenda kuhudumiwa na nani kama sio sisi Wabunge tuliomo humu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, bado miezi tisa mnaenda kuomba kura kwenye Serikali za Mitaa, mnaenda kusema nini kwa hali hii? Mnaendaji kuongea na watu hawa? Mtanzania anakuwaje mtumwa kwenye nchi yake? Wafanyakazi wanalia, wafanyabiashara wanalia, watu wote wanalia, inawezekanaje? Hapana, Mheshimiwa Mpina huwatendei haki Watanzania! Huwatendei haki! Hii kuna siku Mungu atahukumu. Haiwezekani watu wamekuwa watumwa katika nchi yao kwa sababu ya kuvua. Ziwa lipo, tumelikuta, maeneo haya tumeyakuta, watu wanaishi hivyo, leo ni mateso. Haikubaliki hata siku moja, haikubaliki! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, neno hili ni gumu sana kulisema. Wafugaji wana dhambi gani? Kufuga ni dhambi? Mtu kuwa na ng’ombe ni dhambi? Mheshimiwa Waziri anafuatwa mpaka kwenye viwanja vya Bunge hataki kuwasikiliza watu, wewe ni Waziri wa nani? Waziri wa Wizara ya kufanya nini? Kama huhudumii watu, Uwaziri wako ni wa nini? Kama huwezi kusikiliza sekta, ni nini hiki? Wako hapo nje, kila mtu anagawa karatasi, nimeumizwa, ng’ombe wangu wameuzwa wamefanya nini, kwa nini? Hii haiko ndani Ilani ya CCM, kwamba utakuwa Waziri, badala kumsaidia Mheshimiwa Rais, unamsababishia matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumefanya semina ya uvuvi, ilikuwa nzuri kiasi chake, lakini yule mseminishaji anasema Mheshimiwa Rais amempongeza Waziri kwa jukumu analofanya. Nilisema pale pale na ninasema hapa, niliwaambia msimchanganye Mheshimiwa Rais na hilo, Rais hawezi kushangilia wananchi wanateswa, hawezi kushangilia wananchi wake wanaumizwa.Rais amepigiwa kura, anatakiwa kurudi kuomba kura kule. Kwa nini mnamchanganya Mheshimiwa Rais na matatizo ya mtu mmoja ambaye ni Waziri? Kwani Mheshimiwa Waziri kwenye sekta hii ana muda gani? Si miezi tisa! Miezi tisa tu nchi inavurugika, amani inakosa, watu hawalali, hapana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tupe Tume, ije na majibu. Simamisha operation zako. Mheshimiwa Waziri juzi ameenda Mwanza, amesema shughuli hii itaendelea, yale mambo ni ya wanasiasa. Wewe umetoka mbinguni? Wewe hujapigiwa kura? Hatujaja kwako kuomba kura wewe? Wewe umetoka mbinguni? Wanasiasa ni wapi? Haiwezekani, lazima tuwalinde wananchi wetu, lazima wananchi wetu wapate haki yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, bahati mbaya huko nyuma nilikuwa kwenye CCM naongoza kitu fulani, nilitembea nchi nzima hii. Pili, nilipata bahati ya Mheshimiwa Rais kutembea naye. Watanzania ni wanyonge, watu wanaishi kwa mlo wa siku moja, watu wanajishughulisha na mambo yao, mtu anapewa Uwaziri anaona kazi ni hiyo. Haipo hivyo! CCM haitakubali, Serikali haitakubali, kila mtu abebe mzigo wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Ulega nakuhurumia, ukiwa Naibu Waziri huna mamlaka, mwenye mamlaka ni Waziri wako. Kwa nini mnataabisha watu? Kwa nini tunatesa Watanzania? Au niseme, inawezekana Mheshimiwa Mpina unataka Wapinzani watushinde? Ni nini hii? Inawezekana ni style hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaomba Tume kutoka ndani ya Bunge hili na operation zisimame. Hakuna operation haina muda. Kila operation ina muda wake. Bunge hili lituambie operation moja ni miezi mingapi? Operation mbili ni miezi mingapi? Leo unaambiwa inaenda operation three. Unamchukua Hakimu wa Mahakama ya Kutembea, unachukua watu wa operation, anakamatwa mvuvi, watu wanasema faini isiyokwenda benki, tunataka pesa cash. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hawa wanalala guest house, haki ya mvuvi iko wapi? Atapewaje haki yake wakati hawa watu wanakaa kwenye hoteli? Kwa nini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jana Mbunge wangu wa Musoma Mjini pale anasema vizuri samaki wanaongezeka. Wanaongezekaje samaki? Nyavu hazipo. Walikuwa wanavua watu 1000, leo wanavua watu 200, utaona samaki kama zipo, hazipo. Wasafirisha samaki wanaambiwa lazima muwe na mambo ya cold room sijui nini, watayatoa wapi? Lazima samaki wote waende viwanda ili viwanda vipate faida, ndiyo mtu asafirishe. Kwa nini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala hili ni gumu kuliko kuwa kwenye ugumu. Tunasema suala hili ni gumu kwa sababu Wabunge wa CCM mtaenda kuomba kura. Maswali haya mtakutana nayo, lazima muwe na majibu. Haiwezekani watu wakawa wananyanyasika katika nchi yao na sisi tunaangalia, tunakubali. Wana-CCM iteteeni CCM, kesho kutwa kuna kura hapa, tutashindaje? Tutashinda kwa style gani? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kura zinapigwa na watu, hakuna Mbunge anayeingia humu kwa kupewa, ni sisi wachache, tumekuja kwa bahati mbaya huku labda au nzuri, muda wetu umeshaisha, mimi ni mstaafu wala siwazi chochote, sigombei popote, lakini kuisemea CCM, nitasema wakati wowote na mahali popote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mpina umeingiaje kwenye mtego huu? Kuna mtego mmoja umeingia, nakusikitikia sana na ninakuhurumia sana. Nimesema mara mbili ndani ya Bunge hili.
Mheshimiwa Spika, nilishasema mtu anaitwa Vediga, jana umemkaribisha hapa Bungeni mfanyakazi mzuri, ana viwanda na nini, lakini huyu ndio analeta Wahindi peke yake wanafungua butchery kuanzia Mtwara mpaka Singida, hakuna hata Mswahili anayefanya kazi hiyo. Wewe nawe umeingia kwenye mtego huo? Umeingia mtego huo tayari? Nakupongeza. Kwa sababu kama mtego mzuri umekunasa, acha ukunase. Haiwezekani mtu anayetesa Watanzania, anayenyanyasa Watanzania wetu, leo wewe ndio umemleta kwenye gallery kwamba ni mfanyakazi mzuri. Viwanda viko vingapi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasema hili najua kuna wadogo zangu wengi inawagusa kwa sababu huyu ni mwenzenu. Nasema yuko kwa Mheshimiwa Mama Jenista, yuko kwa Mambo ya Ndani, kuna jibu siku litarudi hapa ndani. Haki ya Watanzania itapatikana na haki ya weupe mnaowatanguliza mbele itapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sina zaidi, naomba kwenye majibu ya Mheshimiwa Waziri na Serikali mniambie mnaunda Tume, mniambie operation inasimama na kama operesheni haiwezi kusisimama, shilingi mimi sina. Leo nasema siungi mkono hoja katika hoja iliyopo mbele yako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nawakilisha.