Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema mwingi wa utukufu kwa kunipa uzima ili niweze kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Kilimo na Uvuvi.
Pia nichukue nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya katika nchi yetu ya Tanzania. Ni ukweli usiopingika kwamba nchi ya Tanzania sasa inakwenda kupaa kiuchumi, kila baada ya wiki moja tunashuhudia uzinduzi wa miradi mbalimbali, hongera sana kwako Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nichukue nafasi hii kumpongeza sana Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, niwapongeze sana Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Luhaga Mpina na Naibu wako. Nitakuwa sijatenda haki kama sijakupongeza sana Spika kwa namna ambavyo unachapa kazi, kwa namna ambavyo unasimamia Bunge hili, sasa hivi Bunge limetulia, ukiona chombo kimetulia basi ujue kwamba msimamizi wa chombo hicho yuko makini na mambo yanakwenda bara bara, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie suala la uvuvi wa samaki kwa maana ya sekta ya uvuvi. Katika sekta ya uvuvi nitajikita moja kwa moja Ziwa Nyasa. Nimesoma katika hotuba hii ya Waziri wa Mifugo, hotuba yake katika ukurasa wa 82 na 83 kwenye kipengele kila cha utafiti inaonesha kwamba katika utafiti ambao wameufanya katika maziwa yote pamoja na bahari kuna samaki tani 2,736,247 na mchanganuo wake ni kama ifuatavyo; Ziwa Victoria lina tani 2,148,248; Ziwa Tanganyika tani 295,000; Ziwa Nyasa tani 168,000 na Bahari ya Hindi tani 100,000.
Mheshimiwa Spika, katika utafiti huu ambao wameufanya naomba niende kwenye Ziwa Nyasa. Ziwa Nyasa inaoneshwa kwamba pana tani 168,000 lakini naomba nimuambie Mheshimiwa Waziri kwa maana ya utafiti huo naona kwamba tani hizi ni chache. Je, Serikali au Wizara ina mpango gani wa kuinua au wa kuweka mikakati ambayo itaweka uzalishaji mzuri kwenye hilo ziwa ili ziwa hili liweze kuweka samaki wengi zaidi, ukizingatia kwamba Ziwa Nyasa ni ziwa la pili kwa wingi wa maji, kwa hiyo lina uwezo mkubwa sana wa kuweza kutunza samaki wengi.
Mheshimiwa Spika, pia jirani zetu wa nchi ya Malawi wamekuwa wakifanya uhifadhi wa samaki kwa maana ya fish cage, kwa hiyo kwa uzalishaji na utunzaji huo wa samaki umepelekea samaki wetu kutoka huku upande wa Tanzania wanakimbilia kule kwa ajili ya kwenda kupata chakula, kwa hiyo inaonekana kwamba kwenye Ziwa Nyasa upande wa Tanzania hatuna samaki wengi.
Ninaiomba Serikali yangu ifanye mkakati wa maksudi na ninaamini kabisa Wizara hii ina Mawaziri vijana ambao tumeona wanafanya kazi na wanakwenda maeneo mbalimbali. Ninaamini kabisa wana uwezo mkubwa wa kuweka mikakati mizuri ambayo itakwenda kuzalisha na kwa kuwa, namuona Mheshimiwa Mpina amedhamiria kabisa kukuza sekta hii ya uvuvi hebu nenda kafanye utafiti mzuri zaidi na uone namna gani mnaweza kuinua uzalishaji huu katika Ziwa Nyasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mpina toka umepata madaraka haya ya Uwaziri hujaenda kule Ziwa Nyasa ni lini utaenda Ziwa Nyasa ukatembelee ukaone namna ambavyo ziwa lile lilivyo na ni ziwa ambalo lina vivutio vizuri sana vya utalii, kuna samaki wengi wa mapambo, kuna dagaa wazuri watamu kweli na siku moja hapa nilimtolea mfano dada yangu Mheshimiwa Jenista nikasema angalia hiyo brand ya Mheshimiwa Jenista namna alivyokuwa mzuri ni kwa sababu ya samaki wazuri watamu ambao wanatoka Ziwa Nyasa. Lakini pia nenda kamuangalie dada yangu Mheshimiwa Manyanya muda wote yuko vizuri kwa sababu ya samaki wazuri na mimi mwenyewe je?(Kicheko)
Mheshimiwa Spika, karibu sana Mkoa wa Ruvuma katika Ziwa Nyasa uone aina ya samaki watamu na wazuri ambao wana virutubisho vizuri na ukishakula wale samaki hata magonjwa yanakaa mbali.
Mheshimiwa Spika, napata shida sana, nilidhani kwamba unapokuwa na Bahari ya Hindi maana yake kwa ukubwa wake tunaweza tukawa tunapata tani nyingi za samaki kule, kumbe hii methali inayosema ukubwa wa pua siyo wingi wa..., samahani. Nashangazwa na tani chache hizi ambazo zimeainishwa hapa kwa maana ya utafiti uliofanyika kwenye Bahari ya Hindi. Wizara mna mkakati gani wa kuweka mpango mzuri ambao utakwenda kuhakikisha kwamba Bahari ya Hindi tunaitumia vizuri ili tuweze kupata pato kubwa.
Mimi siyo mtaalam wa mambo ya uvuvi lakini naona niongelee, halafu ninyi kama Wizara mtaona namna ya kuweka vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba pia Wizara iwezeshwe kwa pesa, kama tunazungumzia kwamba waweze kuinua uchumi, waweze kufanya mambo mbalimbali kwenye sekta hii, basi tuhakikishe kwamba hii Wizara inapewa pesa ili iweze kutekeleza majukumu yote ambayo tunadhani kwamba yanafaa kwa Wizara hiyo.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho naomba nirudie tena kumshukuru sana Mheshimiwa Rais aendelee kufanya kazi na kwamba wenzetu sasa Wapinzani wetu wamekuwa kama vile wamepanda basi ambalo wanaendesha gizani na wanatembelea taa za parking, Mheshimiwa Rais endelea kuchapa kazi, tuko nyuma yako, tunakuunga mkono sana.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.