Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ulanga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa kwa namna ya pekee naomba niishukuru taasisi moja ya kidini ambayo inachimba visima bure katika Jimbo langu la Ulanga, taasisi inaitwa AlFayed Charitable Foundation chini ya usimamizi wake wa Ndugu Khadija Ahmad, nadhani unaifahamu hii taasisi, hapa ndiyo najua uwezo wa wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii taasisi kiongozi wake ni mwanamke na inafanya kazi vizuri, kwa hiyo hongera sana wanawake, imeshachimba visima 57 na wana utaratibu wa kuchimba visima 300. Kwa hiyo, Jimboni kwangu suala la maji mambo ni poa kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niweke katika record, katika Bunge lililopita wakati yupo Naibu Spika, Mbunge machachari kabisa kwa upande wa CCM alikuwa Mheshimiwa Luhaga Mpina, sasa hivi kwa bahati mbaya machachari tumeongezeka na bahati mbaya wewe upo huko, kwa hiyo, tuache tukushughulikie sehemu zile ambazo unakosea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninapongeza zoezi la kupinga uvuvi haramu, kwa mfano Mto Kilombero samaki wamekwisha kabisa, lakini zoezi hili linaloendelea lina ukatili mkubwa, lina dhuluma kubwa, lina filisi watu, lina rushwa kubwa na linaleta usumbufu kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sidhani kama watendaji wa Serikali wana nia nzuri kama ya wavuvi ambao wanaishi katika yale maeneo na sijawahi kuona mkakati wa Serikali, labda tuseme mnawawekea pumba hawa samaki au mnawalisha au mnafanya nini, kwa nini mnakuwa wakatili kiasi hiki? Sielewi! Tunawafanya Watanzania kama siyo wapiga kura wetu, humu ndani tumeingia kwa kupigiwa kura, kwa hiyo tuwathamini watu waliotupigia kura.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala langu la pili ni suala la nyavu na hii naomba niliseme wazi. Mheshimiwa Waziri Wizara yako imekithiri kwa rushwa, nasema hivyo kwa sababu viwanda vinavyotengeneza nyavu za samaki ni vichache na havina uwezo wa kukudhi soko, leo hii meli iko bandarini hawaruhusiwi kuingiza nyavu pale wanawekewa mlolongo mrefu na kwa taarifa nilizonazo wale wenye viwanda wamei–corrupt Wizara matokeo yake hamna mtu yeyote anayeruhusiwa kuingiza nyavu ili wao wauze, lazima tuseme ukweli. (Makofi)
Mheshimiwa spika, suala langu la tatu ni biashara ya samaki. Samaki wengi tunaokula wanatoka nje ya nchi, hata watu wanaoruhusiwa kuingiza wote ni watu weupe, wote ni Wahindi, watu weusi wote wamezuiliwa na hii ni kwa sababu ya rushwa. Mheshimiwa Rais wetu mweusi tangu wa kwanza, kwa nini hatuwaamini watu weusi? Viongozi, Mawaziri wote watu weusi kwa nini hatuwaamini? Akija muhindi, mwarabu tunamtetemekea, kwa nini tusiwaruhusu watu weusi ambao wana uwezo na wana uchungu wa nchi hii wasiweze kuingiza samaki?
Mheshimiwa Spika, suala lingine ni suala la malisho ya mifugo, katika jimbo langu la Ulanga tuna mapori mengi kweli …
T A A R I F A . . .
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa kaka yangu Mheshimiwa Murrad utaniwia radhi nimewagusa, lakini hili suala linaumiza sana, kwa sababu watu wote wanaoingiza samaki hamna mtu mweusi hata mmoja, akienda wanasema hana uwezo! Kweli watu weusi hatuna uwezo? Hakuna watu wenye hela? Mabasi mbona wapo watu weusi wanamiliki akina Kimbinyiko wote siyo watu weusi? Hata Shabiby yule ni mweusi umeona lakini hawaruhusiwi wanaambiwa hawana uwezo pamoja na Mheshimiwa Murrad. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, niongelee suala la malisho ya mifugo, kwa mfano Ulanga tuna maeneo mengi sana ya mapori, lakini wafugaji wanapotaka maeneo ya kulisha wanaambiwa maeneo hamna, kwa hiyo hawa watu wamekuwa wanahangaika. Naishauri Serikali tuwatengee maeneo ya malisho, tukishawatengea maeneo ya malisho sasa hivi ziko mbegu ambazo zinapandwa kwa muda mfupi zinaota nyasi nzuri kwa ajili ya malisho.
Mheshimiwa Spika, kuhusu majosho ninaishukuru Serikali imeniahidi kunijengea majosho na malambo kwa ajili ya mifugo, napendekeza hizi mbegu za mifugo za madume bora ziweze kuuzwa kwa bei nafuu ili wananchi wetu waweze kumudu.
Mheshimiwa Spika, kuna suala la watu wa maliasili kukamata mifugo na kuishikilia kwa muda mrefu na kuhitaji pesa kubwa, hii imekuwa unyanyasaji mkubwa sana kwa wafanyabiashara wetu wa mifugo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la masoko kwenye minada yetu wafugaji wanapopeleka mifugo sokoni wauze ama wasiuze wanatozwa ushuru, hili limekuwa linaleta usumbufu mkubwa, Serikali imeniahidi katika Jimbo langu la Ulanga litaweka utaratibu wa masoko mazuri ya mifugo, minada iwe ya kisasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la mwisho ni suala la upigaji chapa, suala hili siliungi mkono kabisa, kwanza ni unyanyasaji wa wanyama, pili ni gharama wafugaji ambao hatuwasaidii kitu tunaenda kupiga chapa tu kwao tunataka pesa, tatu ni usumbufu kwa wafugaji wenyewe na hata kwa wanyama. Sababu wanayosema wanapiga chapa kwa wanyama ni eti wasichanganyike na wanyama wengine ambao wanatoka nje ya nchi. Jamani mbona watu wa mipakani hatuwapigi chapa, kwa nini tupige chapa mifugo? (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, naona hili zoezi lifutwe kwa sababu kwanza lina haribu hata thamani ya ngozi, kwa sababu ngozi ukishaipiga chapa thamani yake inashuka. Leo hii tunasema Tanzania ya viwanda, viwanda vya ngozi vitakosa mazao ya ngozi kwa sababu ya ubora mdogo wa ngozi.
Mheshimiwa Spika, kwa hayo, machache mimi siungi mkono hoja, nataka huu mkazo wa kusitisha hii operation ya kuzuia uvuvi haramu, iundwe Tume ya Kibunge, litakapotolewa hilo ndipo nitaunga mkono hoja, la sivyo nitafanya kampeni ya Mbunge mmoja baada ya mwingine kuhakikisha bajeti hii haipiti na Mheshimiwa Waziri unajua uwezo wangu, nitafanya kampeni ya Mbunge kwa Mbunge kuhakikisha bajeti yako haipiti mpaka iundwe Kamati kwa ajili ya kuondoa hii operation haramu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.