Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kigoma Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Spika, na mimi nianze kuchangia Wizara hii muhimu sana tena sana kwa mustakabali wa nchi yetu na wananchi wetu kwa jumla. Jimbo la Kigoma Kusini lina vijiji 61, kati ya hivyo vijiji 34 viko kwenye Ziwa Tanganyika, wavuvi wanategemea uvuvi ndio wamudu maisha yao. Lakini tuna tatizo kubwa sana tena sana, Idara ya Uvuvi Mkoa wa Kigoma tuna mwanamama pale ambaye ni Afisa Uvuvi Mkoa amekuwa kikwazo kikubwa sana kwa wavuvi. Kwanza hatoi ushirikiano wowote kwa wavuvi, pili amekuwa ni mtu wa kuwakwamisha wavuvi kwa kuwatoza pesa ili wamtetemekee, wanaokataa wanachukuliwa hatua kwa visingizio vya kukosea sheria za uvuvi.
Mheshimiwa Spika, ninao mfano wa Taasisi ya Tuungane iliyopo Kata ya Buhingu, Kijiji cha Mgambo. Taasisi hii haijulikani ina vibali gani kwa kusimamia masuala ya uvuvi ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza wamekuwa ni kero kubwa kwa wananchi maeneo yote yenye dagaa na samaki wa kutosha, wao ndio wanayachukua na kuvua, lakini ukiwauliza wanadai wanalinda samaki wadogo ili wasivuliwe mapema.
Mheshimiwa Spika, tunae mdau namba moja anaitwa Amadi Saidi, ni Mtanzania wa kuzaliwa. Yeye na wazazi wake pale Buhingu na mimi pia nina undugu naye, lakini alichukua uraia wa Abu Dhabi, lakini ni mvuvi mkubwa. Tuombe Wizara imsaidie kumpatia vibali vya uvuvi vyote kwani kufanya kwake kazi ya uvuvi katika Kata ya Buhingu kuna manufaa makubwa sana, amejenga Kituo cha Polisi, amejenga madarasa, amenunua madawati ya shule za Kata ya Buhingu.
Mheshimiwa Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri aliangalie hili. Mheshimiwa Naibu Waziri alikuja/alitembelea na kuona kazi kubwa anayofanya Ndugu Amadi Said. Naomba pia Wizara itupatie nyavu za ruzuku, mashine za maboti za ruzuku na ikiwezekana tupatiwe na maboti ya kuvulia samaki au kama Wizara inatoa mikopo ya wavuvi basi, sisi tupatiwe.
Mheshimiwa Spika, mwisho, tunao mwalo umejengwa Kata ya Mwakizega, Kitongoji cha Muyobozi ili wavuvi waongeze thamani ya mazao yao ya uvuvi, nimuombe Mheshimiwa Waziri amshawishi Mheshimiwa Waziri Mkuu ili atakapokuja kufanya ziara Mkoa wa Kigoma mwezi wa Julai, 2018 basi huu mradi wa mwalo ufunguliwe rasmi kwani mwaka umekamilika.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja.