Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kutoa maelezo yangu kwa Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi. Nina masikitiko makubwa kwamba huenda kama nchi yetu isingekuwa na maziwa makubwa kuzungukwa na bahari basi tusingekuwa na sekta hii ya uvuvi. Hii ni kwa sababu Wizara haioneshi kujali na kuthamini kusambaza huduma za uanzishaji wa mabwawa ya samaki kwenye maeneo ambayo hayana maziwa na mito mikubwa. Hivyo kutokuwa na tija inayokusudiwa kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Tanga wenye Wilaya nane ni Wilaya nne zilizoko pembezoni mwa Bahari ya Hindi ndio zinazopata samaki, Wilaya hizo ni Mkinga, Tanga, Pangani na sehemu ndogo ya Wilaya ya Muheza. Aidha, Wilaya ya Lushoto, Korogwe, Handeni na Korogwe hazina mito mikubwa wala mabwawa ya kuwezesha wananchi kupata kitoweo cha samaki.
Mheshimiwa Spika, jambo hili limekuwa likileta madhara makubwa ya kiafya kwa wananchi hasa wa Lushoto kutokana na upungufu wa madini ya chuma (iron) ambayo yanapatikana katika jamii ya samaki. Naomba kuishauri Serikali itujengee mabwawa ya samaki ili iweze kutibu madhara makubwa ya kiafya ya wananchi wa Lushoto.
Mheshimiwa Spika, ili kuwa na afya bora kwa wananchi wetu wa Tanzania na hata kupunguza bajeti ya Wizara ya Afya, Serikali ni lazima ichukue jukumu lake la kujengea uwezo watu wa Lushoto wapate mabwawa lakini pia na nchi nzima kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Spika, mifugo katika nchi yetu imekuwa haina faida zaidi ya kuonekana kama laana. Tunaomba sana mifugo ijengewe malambo, majosho ili kuongeza thamani ya mazao ya mifugo. Katika Jimbo la Mlalo, Kata za Mnazi na Mng’aro zina wafugaji wengi hasa ikizingatiwa zipo jirani na Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi ambalo ni eneo rafiki kwa ustawishaji wa mifugo. Nitoe rai kwa Serikali kupitia Wizara hii ili kusaidia wananchi wa maeneo haya ili waweze kuboresha mifugo yao. Nashauri pia Serikali iangalie kwa kina sekta ya maziwa hasa eneo la kodi kwa maziwa yanayoingizwa kutoka nje ya nchi. Nawasilisha.