Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Zainab Mndolwa Amir

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nawapongeza Mheshimiwa Luhaga J. Mpina (Mb) Waziri wa Mifugo na Uvuvi pamoja na Naibu Mheshimiwa Abdallah H. Ulega (Mb) kwa kazi nzuri mnayoifanya katika Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali itilie mkazo katika sekta ya ufugaji wa nyuki, maana katika bajeti hii ya mwaka 2018/2019 Serikali haijaonesha mkakati wowote katika kuwasaidia wafugaji wa nyuki nchini mwetu.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali iwasaidie wavuvi wa Mkoa wa Dar es Salaam kupata vyombo vya uvuvi vya kisasa ili waweze kuvua samaki wengi ambao watakidhi matumizi ya wananchi na viwanda vyetu maana kuna wakati mwingine katika Soko la Kimataifa lililopo Ferry (Kivukoni) Mkoa wa Dar es Salaam kunakuwa na uhaba mkubwa wa samaki.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali inunue meli kubwa ya uvuvi ambayo itakuwa na uwezo wa kwenda katika maeneo ya maji yenye kina kirefu na kuvua samaki wengi ambao watatumika na wananchi wa Dar es Salaam pamoja na viwanda vyetu hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, asilimia kubwa ya wananchi waishio Mkoa wa Dar es Salaam hutumia kuku waliofugwa kisasa na hukua kwa wiki tatu hadi nne, pia hutumia na mayai ya kisasa. Kuna sintofahamu inayosemwa na baadhi ya watu kuwa nyama ya kuku hao pamoja na mayai yanayofugwa kisasa yana madhara kwa afya ya binadamu. Naishauri Serikali itoe kauli ili kuondoa sintofahamu ya kuwa kuku wa kisasa na mayai yana madhara kwa mlaji ili mfugaji aweze kutumia mbinu mbadala, ikibainika kuwa kuku hao na mayai yana madhara kwa afya ya binadamu.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali iongeze ufadhili kwa wanafunzi wanaosomea kozi (fani) za mifugo na uvuvi ili kuweza kupata wataalam wengi ambao watasaidia kutoa elimu kwa wafugaji na wavuvi wetu hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iwamilikishe wafugaji ardhi ya kutosha kwa ajili ya malisho na kuweza kuchimba mabwawa kwa ajili ya wanyama (mifugo yao) ili kuondoa migogoro baina ya wafugaji na wakulima ambao inaendelea kuwepo hapa nchini kwetu.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali pindi mfugaji akilisha mifugo yake katika shamba la mkulima, Serikali isimamie (mfugaji)) aweze kulipa fidia kwa mkulima maana mazao hulimwa kufuata hali ya mvua. Hivyo fidia hiyo ilingane na mazao yaliyoliwa ili mkulima awe na uwezo wa kutumia fidia hiyo kuweza kununua mazao (nafaka) hiyo ili kumsaidia kwa matumizi ya familia yake.

Mheshimiwa Spika, mwisho namuomba Mwenyezi Mungu awape afya njema na umri mrefu Mheshimiwa Waziri Luhaga J. Mpina (Mb) na Naibu Waziri Abdallah H. Ulega (Mb) ili muweze kuyaendea majukumu yenu ya kila siku.