Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia Wizara hii muhimu kwa ustawi wa Taifa letu, Wizara ambayo Serikali ikiwekeza kimkakati na kuhakikisha inapeleka fedha za maendeleo kama zinavyopitishwa na Bunge basi Watanzania zaidi ya 10% ambao wamejiajiri moja kwa moja kwenye sekta hii wataweza kuinuliwa kuliko hali ilivyo sasa ambapo tumeendelea kushuhudia wafugaji wakihangaika vilevile wavuvi na wafanyabiashara wa samaki na dagaa wamekuwa wakinyanyasika sana.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya CCM ni kweli haina dhamira ya dhati kwenye maendeleo ya watu bali vitu ambavyo Watanzania chini ya 5% ndiyo wanatumia, mathalani ndege ambazo zimenunuliwa kwa fedha taslimu. Ikumbukwe mwaka 2017/2018 Bunge lilipitisha kiasi cha shilingi bilioni nne kama fedha za maendeleo lakini kwa taarifa za Waziri kwenye kitabu cha hotuba anasema hadi Aprili, 2018 Wizara haikupokea fedha yoyote kwa ajili ya maendeleo licha ya Wizara kukusanya zaidi ya shilingi bilioni nane kwenye tozo ya chapa za ng’ombe tu.

Mheshimiwa Spika, hivi kwa nini tunapoteza muda na fedha za Watanzania walipa kodi maskini kukaa vikao vya bajeti ambavyo hata asilimia moja ya utekelezaji inakosekana? Hii ni aibu kubwa sana kwenye mhimili huu muhimu sana katika kuisimamia na kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Spika, baada ya mchango huo, naomba kuongelea umuhimu wa kuufungua mnada wa mpakani wa Magena uliopo katika Halmashauri ya Mji wa Tarime. Naomba sasa kuikumbusha kwa mara ya nne Serikali juu ya umuhimu wa kuufungua Mnada wa Magena ambao ulifungwa bila sababu za msingi mwaka 1997 kwa kile kilichodaiwa kuwa ni wizi wa mifugo. Sababu hii ilitolewa tarehe 9/4/2018 wakati Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi akijibu swali langu nilipotaka kujua ni lini Serikali itaufungua mnada wa mpakani wa Magena. Kwa masikitiko Serikali ilirudia majibu ya ukaririsho kuwa mnada ulifungwa mwaka 1997 kwa ajili ya wizi wa mifugo. Ukweli ni kwamba kuna nia ovu na wananchi wa Tarime na nia hiyo imetawaliwa zaidi na utashi wa kisiasa badala ya maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, tangu mwaka 2011 nimekuwa nikiiomba Serikali kuufungua Mnada wa Magena nikitambua fika mnada ule upo kimkakati na ufunguaji wake ungeweza kutoa fursa nyingi sana kwa wananchi wa Tarime na kupelekea kukua kwa uchumi kwani sekta mbalimbali zingenufaika (mulitiplier effect). Majibu ya Serikali ya tarehe 9/4/2018 yalijaa fedheha kwa wananchi wangu wa Tarime kwani mnada kupelekwa Kirumi bado ng’ombe wanaonunuliwa Kirumi hupitishwa Tarime kwenda Kenya kwenye Mnada wa Maabara na kupelekea upotevu wa fedha za Tanzania kwani wanaopeleka ng’ombe Kenya hufanya manunuzi ya mahitaji huko huko na kutoa fursa za ajira Kenya.

Mheshimiwa Spika, lakini tujiulize zaidi hapa Tarime wanaposema tangu mwaka 1997 hadi 2018 yaani miaka 21 baadae bado wimbo ni sababu ya wizi wa ng’ombe? Serikali inasahau kuwa Tarime bado kuna Mnada wa Mtana na Randa mbona hao ng’ombe hawaibiwi? Serikali inasahau kuwa tuna Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya na kuwa Mnada wa Kirumi kwanza siyo wa mpakani, lakini pia upo Mkoa wa Kipolisi wa Mara.

Mheshimiwa Spika, Serikali hii hii haijui kwamba mwaka 2016 baada ya kuuliza swali Bungeni aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Uvuvi na Mifugo, Mheshimiwa Mwigulu aliweza kufika Tarime na watendaji wa Wizara ambapo tulikaa kikao na Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya pamoja na Katibu wa CCM Wilaya ya Tarime na maazimio ya kikao ilikuwa ni kuufungua Mnada wa Magena baada ya kujiridhisha na mazingira ya sasa na hivyo kupangwa siku za Mnada wa Kirumi uwe mara mbili kwa wiki na ule wa Magena nao mara mbili kwa wiki ila siku tofauti. Baada ya hapo tuliweza kutembelea eneo la mnada na kujionea miundombinu iliyopo kuwa inakidhi kuanza mnada mara moja. Mheshimiwa Waziri
pamoja na DC Luoga waliongea na wananchi na kuwahakikishia ufunguzi wa mnada huo.

Mheshimiwa Spika, nimeandika haya kuweka kumbukumbu sawa maana nilishtushwa na majibu ya mwaka 2018 wakirejea maamuzi ya mwaka1997 ilhali kuna maamuzi ya mwaka 2016 yanayosubiri utekelezaji tu. Naomba Serikali ione ni kiasi gani tunapoteza fursa kwa kutoufungua mnada ule kwani Mnada wa Kirumi kamwe hauwezi kuwa mbadala wa Mnada wa Magena badala yake tutaendelea kuifaidisha Kenya.

Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba ng’ombe zinazotoka Wilaya ya Serengeti haziendi Kirumi zinaenda moja kwa moja Kenya kupitia Tarime. Ng’ombe zinazotoka Rorya kwa asilimia kubwa zinaenda Kenya moja kwa moja kupitia Tarime. Ng’ombe zinazotoka Kirumi zinapita Tarime kwenda Kenya.

Mheshimiwa Spika, naendelea kuiomba Serikali hii ya CCM ifungue mnada huu wa kimkakati wa Magena ili uweze kuwa stop center ya minada hiyo mingine na uweze kuliingizia Taifa fedha ambazo sasa zinapotea kwa kupeleka ng’ombe kwenye mnada wa mpakani wa Kenya ilhali Tanzania tuna mnada wa mpakani lakini tumeufunga kwa sababu za kisiasa. Tunataka kuona watu wa Kenya wanakuja kufuata mifugo Tanzania na kuweza kuacha fedha za kigeni kwetu na siyo sisi kuwapelekea mifugo.

Mheshimiwa Spika, labda Serikali haijui Kenya wanategemea sana ng’ombe (mifugo) wa Tanzania na hivyo huu mnada ukifunguliwa utakuza uchumi wa wananchi wangu wa Tarime, Halmashauri tutapata mapato na Serikali Kuu pia itapata mapato na zaidi kasi ya ukuaji wa Mji wa Tarime itaongezeka na fursa za uwekezaji nazo zitaongezeka na hatimaye maendeleo. Zaidi ule usumbufu wanaoupata wafanyabiashara wa Tanzania wakati wanavusha mifugo kwenda Kenya utakuwa umepunguzwa. Naomba Wizara inipe majibu ni lini na kwa uharaka mnada ule utafunguliwa.