Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, pongezi kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na wataalam wote wa Wizara kwa kuandaa hotuba na kuwasilisha hapa Bungeni.

Mheshimiwa Spika, Tanzania ni nchi ya pili katika Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya mifugo, hata hivyo idadi hiyo haijaweza kuchangia kikamilifu katika pato la Taifa kutokana na changamoto nyingi zinazoikabili sekta ya mifugo. Wafugaji wa Taifa hili wamekuwa wanahangaika sana kwa kukosa malisho na huduma muhimu na hivyo kusababisha migongano ya wafugaji na wakulima na watumiaji wengine wa ardhi.

Mheshimiwa Spika, Sheria za Ardhi na Maliasili zinaelekeza Mawaziri watenge maeneo ya mifugo na kuyatangaza kwenye gazeti na kuyalinda. Sasa Serikali ieleze hapa ni maeneo gani yametengwa kwa ajili ya mifugo na malisho ya mifugo, yako mikoa na wilaya zipi?

Mheshimiwa Spika, wafugaji wamekuwa wanakamatiwa mifugo yao kwenye hifadhi za misitu, inapigwa mnada hata pale Mahakama inapotoa hukumu kwamba irudishwe kwa wenyewe. Waziri wa Mifugo anashughulikiaje suala hili ambalo limewafilisi wafugaji wengi na wamebaki maskini?

Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango gani kuhakikisha nyakati za mvua vyakula vya mifugo vinaandaliwa na kutunzwa kwa ajili ya matumizi ya nyakati za ukame, Kilenge’s Silage na kadhalika?

Mheshimiwa Spika, kuna mpango gani wa Serikali kutengeneza na kuendesha kampeni za unywaji maziwa mashuleni na katika jamii nzima? Sote tunafahamu umuhimu wa maziwa na kwa ng’ombe tulionao Tanzania inawezekana kabisa kila shule kupata maziwa kwa watoto wetu.

Mheshimiwa Spika, viwanda vingi vya kuchakata mazao ya mifugo vimekufa hali inayopelekea wafugaji kukosa masoko ya uhakika kwa mifugo yao. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha viwanda vyote vya ngozi, nyama na kadhalika vinafanya kazi? Naomba Waziri aje na majibu ya nini mkakati wa kufufua viwanda hivyo.