Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JANETH M. MASABURI: Mheshimiwa Spika, pamoja na hatua nzuri zilizochukuliwa katika kutatua changamoto zilizoko katika sekta ya uvuvi na mifugo, kuna changamoto nyingi ambazo zinahitaji kupatiwa ufumbuzi wa haraka. Naomba nichangie changamoto chache kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, sekta ya uvuvi itaendelea iwapo itapata msukumo kwa kuwekeza kwa kiwango kikubwa kama kuwekeza kwa wataalam ambao wataendana na teknolojia ya uvuvi wa kisasa, ununuzi wa vifaa vya kisasa vya uvuvi na uhifadhi wa samaki, elimu, semina za mara kwa mara kwa wavuvi wadogo wadogo. Viongozi wa Serikali watumie lugha ya kuelimisha wavuvi kuliko kutumia nguvu zaidi, hali wakijua uelewa wa watu uko tofauti. Ndiyo maana Baba wa Taifa alitumia kampeni ya kuelimisha na kuhamasisha watu katika mambo mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali iweke mazingira ya kujenga mabwawa ya kufugia samaki kwa kila Halmashauri ili wananchi waweze kupata lishe na pia kufanya biashara na kuongeza ajira kwa vijana. Kwa kufanya hivyo kunaweza kupunguza malalamiko ya uvuvi. Pia Kanda ya Ziwa itumike kujenga mabwawa ya ufugaji wa samaki kando kando ya Ziwa Victoria, kwa kiwango kikubwa bila kusahau kuwaelimisha wavuvi wadogo wadogo. Uvuvi wa bahari kuu ndiyo mkombozi wa kuingiza fedha za kigeni. Vilevile nguvu iongezwe kupata makampuni makubwa ya kuvua samaki katika bahari ya kina kirefu (Deep Sea Fishing).
Mheshimiwa Spika, sekta ya mifugo ndiyo tegemeo la wanadamu karibu wote kwa maana ya kwamba kabla ya mtoto kuzaliwa, mama mjamzito hushauriwa kunywa maziwa, mtoto akizaliwa hunywa maziwa, mgonjwa hunywa maziwa, mzee chakula chake ni maziwa na sisi maziwa ndiyo chakula chetu cha kila siku. Serikali iangalie uwezekano wa kuwekeza katika sekta hii, kwa kuwa inawagusa wananchi wengi walio maskini sana, pia uelewa wao ni mdogo ingawa wana mifugo mingi. Ubora wa mifugo na unafuu wa kodi ambazo ni kikwazo kwa mazao ya mifugo kama nyama, maziwa, ngozi, jibini, mifupa, mbolea na kadhalika. Kupiga chapa ng’ombe kuangaliwe kwa kuweka alama eneo la masikioni kuliko kuweka pajani au tumboni. Hali hiyo huharibu ubora wa ngozi.
Mheshimiwa Spika, ombi langu ni kwamba Serikali ifanye uwekezaji mkubwa katika sekta ya mifugo na uvuvi ili kufanya mageuzi na mapinduzi katika sekta hizi bila kusahau sekta ya kilimo pia.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.