Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkuranga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. Awali ya yote napenda kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha hapa nilipo leo nikiwa na afya njema. Nianze mchango wangu kwa kutamka kwamba naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kujibu hoja mbalimbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge, naomba kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi. Napenda kutumia nafasi hii kumuahidi Mheshimiwa Rais kwamba nitafanya kazi yangu kwa uadilifu na uaminifu mkubwa sana ili kuhakikisha kwamba Tanzania sekta hizi za mifugo na uvuvi zinachangia kikamilifu katika kuinua pato la mfugaji na mvuvi na kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa kipato cha kati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia napenda nichukue fursa hii nimshukuru tena Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa kwa uongozi wao mahiri na makini kabisa ambao unaipeleka nchi yetu katika uelekeo wake ule ule wa amani, utulivu na maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda pia kumshukuru Waziri wangu Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, Mbunge wa Kisesa kwa kunishirikisha kwa karibu sana katika majukumu ya kuongoza Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Spika, pia nikushukuru sana wewe mwenyewe, Naibu Spika, Wenyeviti wote wa Bunge, Wabunge wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushirikiano wao kwa ujumla wanaonipa katika utendaji wangu wa kazi za ndani na nje ya Bunge letu tukufu. Nawaahidi ushirikiano na nasema ahsanteni sana kwa ushirikiano mnaonipa kila mara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba pia vilevile nichukue fursa hii niwashukuru watendaji wetu katika Wizara, Katibu Mkuu Dkt. Mary Mashingo anayeshughulika na mifugo, vilevile Katibu Mkuu Dkt. Yohana Budeba anayeshughulika na uvuvi na Wakuu wa Idara zote na taasisi zote zilizoko katika wizara yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba pia nichukue fursa hii kuwashukuru sana wapiga kura wangu katika Jimbo la Mkuranga na nataka niwahakikishie kwamba mimi kijana wao niko makini na timamu kabisa kuendelea kuitumikia kazi hii ya Ubunge wa Jimbo la Mkuranga bila ya kuchoka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee, naomba uniruhusu pia nimshukuru mke wangu na familia yangu kwa namna ambavyo wamekuwa wakinipa ushirikiano wa hali na mali wakati wote wa kutumikia kazi hizi za nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema haya, naomba sasa uniruhusu niweze kujibu hoja ambazo zimeletwa na Waheshimiwa Wabunge wakati wakichangia mjadala wa bajeti yetu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Kwanza, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote, sisi katika Wizara tumeyachukua mawazo, maoni na maelekezo yao mbalimbali waliyotupatia. Nataka niwahakikishie kwamba vitu vyote hivi walivyotushauri tutavifanyia kazi ili kuweza kupata uendelevu wa sekta zetu hizi za mifugo na uvuvi kwa manufaa mapana sana ya nchi yetu ya Tanzania. Mimi nitazungumza kwa uchache lakini baadae Mheshimiwa Waziri wangu atakuja kueleza kwa upana zaidi ili kuweza kujibu hoja zote bila mashaka yoyote yale.
Mheshimiwa Spika, la kwanza ambalo limezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge wengi ni namna ambavyo sisi kama Serikali tulivyojipanga kuhusiana na sekta hii inayochipukia ya ufugaji wa samaki. Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge sisi tunaelewa namna ambavyo Wabunge wengi wamekuwa wakivutiwa na suala hili la ufugaji wa samaki kwa maana ya aquaculture. Mpango mkakati wetu ni kuhakikisha kwamba Watanzania walio wengi wanaingia katika ufugaji wa samaki kwa sababu ufugaji wa samaki umekuwa ni wenye kuleta matumaini.
Mheshimiwa Spika, namna gani Wizara tumejipanga? Nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge, sheria na kanuni zetu wakati fulani unaweza ukaziona kwamba, mathalani samaki ambao wanafugwa katika mabwawa yetu hawaruhusiwi kuchakatwa na hata kuuzwa nje. Hivi ni vitu ambavyo vimesababisha wakati mwingine sekta zetu zisisonge mbele kwa sababu zinakuwa si sekta shindani, watu hawavutiki kwenda kuwekeza pesa zao katika aquaculture.
Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie baada ya mazungumzo ya muda mrefu chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Waziri Luhaga Joelson Mpina, tumekubaliana kufanya mapinduzi katika eneo hili la aquaculture. Moja, hatuoni sababu ya kwa nini samaki wanaozalishwa katika mabwawa yetu wasiuzwe kibiashara. Kwa hiyo, nataka niwaahidi Waheshimiwa Wabunge kwamba eneo hili tunakwenda kulifanyia marekebisho. Tuchakate samaki wetu wanaotoka katika mabwawa (ponds) lakini turuhusu pia vilevile hata wauzwe ili tuweze kuvutia uwekezaji zaidi kwenye eneo hili.
Mheshimiwa Spika, kama hilo halitoshi tumeona juu ya kodi na tozo mbalimbali ambazo zinafanya sekta hii isiweze kuvutia hasa katika eneo la uingizaji wa vifaa mbalimbali. Tumekuwa tukiendelea na mashauriano na wenzetu wa Wizara ya Fedha, tunaamini kwamba watalifanyia consideration ambayo itakwenda kuwasaidia Watanzania wavutike katika kuwekeza kwenye eneo hili.
Mheshimiwa Spika, lakini pia tumejiwekeza zaidi katika kwenda kuviimarisha vituo vyetu, tunavyo vituo nchi nzima vinavyofanya kazi hii ya aquaculture. Vituo vyote hivi tumejielekeza katika kwenda kuviimarisha ili kuzalisha vifaranga vya kutosha, tuvigawe kwa wananchi lakini vilevile kuhakikisha tunapata chakula bora kwa ajili ya ufugaji wa samaki. Maana tatizo kubwa lililopo katika eneo hili ni upatikanaji wa chakula kizuri na upatikanaji wa vifaranga. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba vyote hivi tunaenda kuvitatua.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo limezungumzwa na Wabunge wengi ni eneo la nyavu, je, hizi nyavu mbona zimekuwa na mjadala mkubwa sana, ni nini tatizo? Pia vilevile imezungumzwa ya kwamba sisi tumetoa monopoly ya kiwanda kimoja tu katika nchi ambacho ndiyo kinaingiza nyavu kwa wavuvi, lakini Waheshimiwa Wabunge wakafika hatua ya kusema tumezuia uingizaji wa nyavu.
Mheshimiwa Spika, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Bunge lako tukufu hili, Wizara yetu haijazuia hata kidogo uingizaji wa nyavu nchini isipokuwa lazima tukubaliane kazi tuliyoifanya ya kuondoa zile nyavu ambazo zinasemwa na sheria kwamba ni nyavu haramu ni kubwa mno. Ukitazama anayeathirika ni yule mvuvi wa chini kule, tulipokwenda kuzichoma na kuziteketeza kwa mujibu wa sheria, waathirika wakubwa ni wale wavuvi wetu wa kule chini. Mara zote Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakiuliza kwa nini Serikali inajielekeza zaidi kwenda kushughulika na wavuvi wale wa kule chini hawashughuliki na wazalishaji na wasambazaji.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia maoni hayo ya Waheshimiwa Wabunge ndiyo maana sisi hatukukubali kwanza moja kwa moja kufungua mipaka yetu kuziingiza nyavu zile. Tulisema ni lazima turatibu zoezi hili ili tusiende kurudia makosa yale yale kila siku ya kwenda kumchomea mvuvi wetu, mvuvi mnyonge kwa sababu sisi tunaamini sekta hii ya mifugo na uvuvi haiwezi kuwepo bila ya kuwepo kwa hawa wavuvi wetu. Kwa hiyo, nataka niwahakikishieni baada ya kukubaliana na kufanya tathmini hii tutakuwa tuko tayari hata kufungua.
Mheshimiwa Spika, niwaambie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba nyavu hizi nyingi zinazalishwa katika nchi jirani mojawapo ambayo haina hata ziwa lenyewe. Sisi hapa hiki kiwanda kinachosemwa cha hapo Arusha tumekipa kweli leseni baada ya kutuomba. Mimi mwenyewe kama Naibu Waziri nimekipitia kiwanda hiki, kina marobota ya nyavu za kuvulia dagaa mengi sana hayana mnunuzi. Tumeelewa concern ya Wabunge ya kwamba inawezekana wale mabwana nyavu zao hazina ubora. Tumekubaliana na wenzetu wa Wizara ya Viwanda na Biashara wanaohusika na masuala ya ubora tuweze kwenda kuhakikisha kwamba nyavu zile zinakwenda kuzalishwa zenye ubora zaidi.
Waheshimiwa Wabunge tunaomba mtuamini ya kwamba jambo hili tunalizingatia ili kusudi sekta yetu ya uvuvi na wavuvi wetu wasiweze kuweza kwenda kuharibikiwa.
Mheshimiwa Spika, vilevile kuna contradictions za sheria ambazo zimejadiliwa hapa na baadhi ya wavuvi wenzangu kwamba sasa inakuwaje juu ya hizi nyavu za dagaa lakini wakati huo huo zinakwenda na zinakamatwa tena. Unafahamu wavuvi nao vilevile ni binadamu na ni wajanja, kule Kanda ya Ziwa kuna uvuvi maarufu unaitwa gizagiza. Zilezile nyavu za dagaa kwa mujibu wa sheria na utaratibu wetu zile huenda kuvua kwa kutumia karabai, lakini watu wamezigeuza, hawatumii tena karabai wamefungia zile karabai zao, usiku wanakwenda kuvua bila ya zile karabai. Wanapokwenda kuvua bila ya zile karabai ndiyo wanaita gizagiza.
Sasa wakati ule wanapokuwa hawatumii karabai wanampata sangara mchanga, wanapata sato na mazao mengine ya uvuvi, ukitumia karabai haupati matatizo hayo.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya ufinyu wa muda, naomba niende katika upigaji chapa. Waheshimiwa Wabunge wengi sana wameeleza juu ya upigaji chapa na tena babu yangu Mzee Ndassa pale ameenda na kuniambia mimi kwamba tena wewe Ulega mwenyewe hata hii shughuli ya ufugaji hujawahi kuifanya.
Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishieni Waheshimiwa Wabunge mawazo na ushauri wenu wote mlioutoa katika kulinda sekta ya ngozi kwenye eneo hili la upigaji chapa tumeyachukua na sasa timu yetu inafanya tathmini. Kwa sababu hili eneo ni endelevu kwa maana ya kwamba upigaji chapa si kitu cha kusema kwamba kinaisha leo au kesho, ni kitu ambacho kipo kwa mujibu wa Sheria ya Utambuzi wa Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kile ambacho ninyi mmekiomba ni kuhakikisha kwamba tunaboresha, tumeyachukua yale mawazo kwamba tusichome tena ng’ombe badala yake tuwavalishe hereni ama tutafute mbinu nyingine zozote ambazo zitakwenda kuifanya ngozi yetu na mifugo yetu iendelee kuwa na thamani. Mimi nataka niwahakikishieni kwamba jambo mlilotushauri ni jema na tumelichukua na tunakwenda kulifanyia kazi mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, imezungumzwa pia vilevile hoja na jirani yangu Mheshimiwa Dau iliyohusu MPRU kwa maana ya hifadhi ya bahari. Nataka nimhakikishie kwamba kama nilivyokuwa nikijibu kila mara kwamba hifadhi ya bahari ipo kwa mujibu wa sheria lakini yeye concern yake ni juu ya mapato na amezungumzia kwamba kwa nini tusichukue MPRU kwa maana ya Hifadhi wachukue asilimia 50 na Halmashauri wachukue asilimia 50. Kwa sasa hivi asilimia 30 zinakwenda katika Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kwa maana ya 10 zinakwenda katika Halmashauri yenyewe na 20 inakwenda katika vijiji ambavyo vimezungukwa na ile hifadhi ya bahari. Ushauri wake wote aliotupatia wa kwamba tunataka twende katika usawa tunauchukua. Haya ni mambo ambayo tuna uwezo wa kuyazungumza, tukakaa kwa pamoja, tukashauriana na kuona ni namna gani bora zaidi ya kuweza kuwasaidia watu wetu.
Mheshimiwa Spika, mwisho nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wengi waliozungumzia ufugaji wa kuku kwamba Wizara yetu inao mradi mkubwa sana wa kuhamasisha ufugaji wa kuku. Kwa hivi sasa tumeshazifikia halmashauri 20 katika nchi nzima. Tunagawa bure kabisa mbegu ambazo ni za Kitanzania zenye kuhimili matatizo na ugonjwa kama vile ugonjwa wa mdondo na mengineo.
Kwa kusema ukweli tutahakikisha kwamba tunafikia Halmasharuri zote nchini. Mradi huu umefadhiliwa na wenzetu wa Bill & Melinda Gates ambapo tunahakikisha mpaka kufika mwaka 2019, Halmashauri zetu nyingi ziwe zimepata mradi huu wa ufugaji wa kuku. Nia na madhumuni yetu ni kuhakikisha tunainua kipato cha wafugaji wetu lakini pia tuwe na uhakika wa chakula vilevile.
Mheshimiwa Spika, yapo magonjwa ya mifugo vilevile yamezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge wengi. Nataka niwahakikishie kwamba sisi katika Wizara tumeweka mkakati madhubuti kabisa wa kupambana na magonjwa ya mifugo. Tumeweka magonjwa ya kipaumbele, yapo magonjwa kama kumi ambayo tumeona kwamba haya tuyafanye kuwa magonjwa ya kipaumbele katika ng’ombe kwa mfano ugonjwa wa kuangusha mimba na magonjwa ya miguu na midomo na katika kuku magonjwa kama vile ya mdondo, yote tumeyapa kipaumbele.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi maabara yetu ya pale Temeke Veterinary tuna chanjo takribani nne. Tunaamini kabla ya mwaka huu haujaisha tutakuwa tumeipata chanjo ya ugonjwa unaowasumbua ng’ombe wetu wengi sana, chanjo ya ugonjwa wa homa ya mapafu. Mpaka mwisho wa mwaka huu tunahakikisha kwamba tumeipata chanjo ile. Baada ya hapo ni lazima niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwamba kama tunataka kweli kabisa sekta yetu ya mifugo isonge mbele ni lazima upigaji wa chanjo yaani uchanjaji wa mifugo yetu uwe wa lazima ili kuweza kuifanya sekta hii iweze kukua vizuri na hatimaye tuweze kushindana katika masoko ya kimataifa, tuuze nyama yetu na watu waikubali nyama yetu.
Mheshimiwa Spika, naomba sana Waheshimiwa Wabunge tutakapofika katika hatua za namna hii nanyi muendelee kutuunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema haya, naomba tena nichukue fursa hii kusema kwamba naunga mkono hoja kwa asilimia moa moja kabisa. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge yale yote ambayo leo mmetuambia katika Bunge hili na kututaka tuweze kurekebisha ili hali iweze kuwa nzuri zaidi katika sekta zetu hizi za mifugo na uvuvi, tumeyachukua na tunakwenda kuyafanyia kazi. Ninaamini kwamba baada ya muda mfupi mtakuja hapa kutushangilia kwa namna ambavyo tumefanya vyema katika kazi mliyotutuma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsanteni sana.