Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibiti
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia kwa maandishi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika zao la korosho lipo tatizo kubwa sana kama ifuatavyo:-
(i) Upatikanaji wa pembejeo za sulphur. Hapa lipo tatizo kubwa kwani pembejeo hazipatikani kwa wakati;
(ii) Mfumo huu siyo rafiki kwa mkulima, haumletei tija mkulima, kumekuwa na udanganyifu sana katika mfumo huu wa pembejeo za ruzuku;
(iii) Naomba mfumo huu uboreshwe kwa kutoa kodi ambazo siyo za lazima ili pembejeo ziuzwe kama Coca-Cola katika maduka yote ya pembejeo;
(iii) Mfumo wa Stakabadhi Ghalani nao una changamoto kubwa, hasa katika Jimbo langu la Kibiti, kwani wakulima mpaka leo wanadai malipo yao ya mauzo ya korosho zao kama shilingi bilioni sita hivi msimu wa mwaka 2012/2013. Jamani kwa nini mkulima anakopwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto za zao la korosho:-
(i) Maghala ya kuhifadhia;
(ii) Pembejeo za uhakika na wakati;
(iii) Wataalam;
(iv) Viwanda vya kubangulia korosho;
(v) Ukosefu wa soko la uhakika; na
(vi) Miche bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto hizi zote zinaweza kutatuliwa kama kila mmoja atafuata wajibu wake kama Bodi ya Korosho. Bodi hii ya Korosho inakusanya pesa nyingi kwa kila msimu wa mauzo ya korosho, lakini cha kushangaza haimsaidii kabisa mkulima na zao la korosho.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wangu wa Jimbo la Kibiti kama vile Kibiti, Mtawanya, Bungu, Jaribu, wanalima sana mazao ya matunda kama mananasi, pasheni, embe, papai, machungwa, machenza, ndimu, limao na parachichi. Tatizo la kilimo hiki ni soko la uhakika, kwani mpaka sasa soko lipo moja tu, la Bakhresa, Azam. Soko hili halina tija kwa wakulima wa matunda kwani yupo peke yake, hata bei ya kununua mazao hayo hupanga yeye mwenyewe tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuishauri Serikali yangu sikivu ya Awamu ya Tano ya Hapa Kazi Tu, ili kupata soko la mazao ya wakulima wa matunda ni kujenga viwanda vya kusindika matunda katika maeneo ambayo matunda yanalimwa kwa wingi, kama Jaribu, Kibiti, Mtawanya, Bungu na Mlanzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, zao la minazi katika Jimbo langu linapotea kwa kiasi kikubwa kwani kumeibuka ugonjwa mbaya wa minazi ambapo hakuna anayejali. Hatujaona Extension Officers wanaojali kuhusu zao hili la biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Uvuvi ina umuhimu sana katika uzalishaji mali kwa vijana wetu ambao wanakumbwa na tatizo kubwa la ajira kwa vijana. Katika Jimbo langu la Kibiti, kuna maeneo ya Delta ambayo yamezunguka kando kando ya Bahari ya Hindi. Sekta hii ni muhimu sana kwa pato la Taifa letu la Tanzania kwani vipo vikundi vingi vya uvuvi katika maeneo hayo ambayo vinasimamiwa na BMU.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuishauri Serikali yangu sikivu kuwapa vijana vifaa vya kisasa vya uvuvi kama vile boti za kisasa, nyavu ambavyo vinawezesha uvuvi bora na endelevu. Kuchimba mabwawa ya kufugia samaki badala ya kutegemea mabonde.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Kibiti mifugo ipo mingi na mpaka inaleta migogoro ya wakulima na wafugaji kama vile Muyuyu, Makima, Maporoni. Napenda kushauri Serikali yangu sikivu kutenga maeneo ya kulima na ufugaji ili kutoa au kukomesha kabisa migogoro hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri katika Wizara yenye dhamana, hasa ndugu yangu Mheshimiwa Mwiguli Lameck Nchemba, sasa ana kazi ya kufanya kuhakikisha tunashirikiana naye kwa pamoja, sisi sote kwa kuboresha mazingira ya wafugaji kwa kuwajengea miundombinu kama:-
Kujenga machinjio ya kisasa;
Kujenga majosho;
Kujenga malambo;
Kuwapelekea Afisa Mifugo kuwa karibu nao;
Kujenga vituo vya minada;
Kuunda Kamati ya watu 10 kila Sekta tano za wakulima na wafugaji ili kutatua migogoro hiyo kabla hawajapelekana mbele ya sheria;
Wafugaji wawe tayari kulipa ushuru wa minada. Hii inawafanya wakulima waone umuhimu wa ufugaji katika maeneo yao; na
Kujenga viwanda vya bidhaa ambazo zinatokana na mifugo kama maziwa, ngozi na nyama.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ng‟ombe kila kitu mali.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho napenda kumuuliza swali ndugu yangu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba; kwa nini mazao yote ambayo yameundiwa Bodi za Mazao, mazao hayo hayafanyi vizuri?
Mheshimiwa Naibu Spika, mazao yenye Bodi ni matatizo. Korosho hoi, pamba hoi, chai hoi, pareto hoi, kahawa hoi, tumbaku hoi. Hii inaonesha kwamba hizi bodi hazimsaidii mkulima na badala yake zinamnyonya mkulima kwa asilimia kubwa sana na kumwachia maumivu makali.
Mheshimiwa Naibu Spika, mazao ambayo hayana bodi ni ufuta ambao uko hai, mbaazi hai, kunde hai, njugumawe hai, mihogo hai, mahindi hai, m punga hai. Mazao haya yanafanya vizuri katika Sekta ya Kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kauli Mbiu, Ukitaka Mali Utaipata Shambani.