Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bumbuli
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia bajeti hii na nianze kwa kukupongeza kwa jinsi unavyoongoza Bunge letu vizuri kwa busara na hekima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Mpango, Waziri wa Fedha, Naibu Waziri wa Fedha, Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote. Nimefuatilia mijadala ya bajeti hata kabla ya hapo, mijadala mbalimbali iliyohusu Wizara ya Fedha. Bahati mbaya sana katika baadhi ya mambo niliyobaini ni mashambulizi binafsi kwa Mheshimiwa Dkt. Mpango (personal attack), kwamba kuna wakati tabia yake, kwamba ana kiburi, ilikuwa inazungumzwa kuna wakati hata elimu yake inatiliwa mashaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati mwingi kilichopo mezani huwa ni hoja, lakini bahati mbaya, mimi bahati nzuri nimepata kumfahamu Mheshimiwa Dkt. Mpango miaka kumi tumekuwa wote, alikuwa msaidizi wa Rais, Uchumi mimi nilikuwa Msaidizi wa Rais, Hotuba, nimefanya nae kazi kwa karibu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukitaka kujua humility au humbleness ni Dkt. Mpango, hii habari ya kiburi, binafsi na wote ambao tuna-interact naye binafsi hiyo haipo. Kwa hiyo nadhani wakati mwingine humu ndani ya Bunge tupingane tu na ni haki na ni sahihi, kuwa na mawazo tofauti ya alicholeta mezani lakini tunapomwendea binafsi tunakuwa tunakosea. Wakati mwingine sio yeye tu hata humu ndani baina ya Wabunge na Wabunge, umebaini Mbunge anapotoa hoja kinachojibiwa sio alichosema bali ni yeye yukoje na anaishi wapi na anafanya shughuli gani na yote ambayo yamezungumzwa yanakuwa sio tena hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Bunge la namna hiyo nadhani sio Bunge unalolitaka na sio Bunge linalostahili hadhi na uzito wako kama wewe Spika. Kwa hiyo, nataka ni-vouch, nimtetee Dkt. Mpango kwamba namfahamu na pia ukiondoa tu tabia yake ya kusikiliza na kuheshimu kila mtu, pia ni msomi mzuri bila shaka yoyote. Amefanya kazi Benki ya Dunia, ameaminiwa na Marais wawili, amepitia kwenye mikono ya Profesa Ndulu ambaye tunamsifu ni gwiji wa uchumi hapa nchini, ameaminiwa nje ya nchi na ndani ya nchi na pia ni mcha Mungu, kaka yake ni Askofu anatoka huko katika familia ya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia Mheshimiwa Dkt. Ashatu wote ambao tunapishana naye kwenye corridor hatuwezi kusema kwamba, ana kiburi, tunamjua kwamba mtu ana heshima. Vilevile watalaam wa Wizara ya Fedha wakiongozwa na Bwana Dotto na wao pia ukimfuata bwana Dotto anakusikiliza na anafanya maamuzi akielewa jambo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niliona wakati tunaongelea bajeti hawa viongozi wetu wakuu ambao tumewapa kazi kubwa sana ya kuandaa bajeti na kuiwasilisha na kujibu siyo kazi ndogo wanaifanya kwa niaba yetu sisi Watanzania. Hivyo, tusiwapeleke kule ambapo tutazidi kuwatia msongo wa mawazo kwamba kazi wanayofanya hatuithamini. Kwa hiyo, nawapongeza kwa weledi wao lakini pia kwa hulka zao.
Mheshimiwa Spika, naomba nikuthibitishie kwamba sikukaa chemba na Mheshimiwa Dkt. Mpango kabla ya kuzungumza hapa siku ya leo. Kwa hiyo hizi ni hisia kabisa binafsi na zinawasilisha mawazo mengi hapa katika Baraza la Mawaziri na Wabunge wengi ambao tunafanya kazi na Mheshimiwa Dkt. Mpango. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna mambo kadhaa yamezungumzwa kuhusu muungano hasa kubwa ni hoja ya Mheshimiwa Dkt. Ally Yussuf Suleiman ambaye ametaja mambo matatu, ambayo napenda kuchukua nafasi hii kuyajibu harakaharaka.
Mheshimiwa Spika, la kwanza ni akaunti ya pamoja, amesema muda mrefu akaunti hii haijaanzishwa. Ni kweli na akaunti hii ya pamoja imewekwa ni hitaji la kikatiba kifungu cha 133 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinaelekeza kwamba kuwe na Mfuko wa Akaunti ya Pamoja ya Fedha ambayo itakuwa sehemu ya Mfuko Mkuu wa Hazina ambapo kutawekwa fedha yote itakayochangwa na Serikali mbili kwa kiasi kitakachoaamuliwa na Tume ya Pamoja ya Fedha. Hilo ndiyo neno la msingi, kwa kiasi kitakachoamuliwa na Tume ya Pamoja ya Fedha.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Akaunti hii ya Pamoja haijakuwepo kwa sababu mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha kuhusu kiwango cha mgawanyo ndiyo yanafanyiwa kazi na Serikali sasa hivi. Hili ni jambo kubwa linahitaji uamuzi wa Mabaraza yote mawili ya Mawaziri ya pande zote mbili na linahitaji input kubwa ya wataalam.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kinachoendelea sasa hivi ni kusubiri maamuzi baada ya wataalam kuwa wanamalizia kazi yao. Kwa hiyo, sisi kama Serikali azma ya kutimiza matakwa ya kikatiba bado ipo palepale, lakini kwa kuwa ni jambo kubwa lazima tuliendee kwa umakini na utaratibu ili liweze kufanikiwa kwa kiwango kikubwa.
Mheshimiwa Spika, suala la pili lililozungumzwa kuhusu Muungano ni suala la mchakato wa sasa hivi unaoendelea wa usajili wa meli. Kama unavyofahamu Tanzania ina aina mbili ya usajili wa meli; kuna usajili wa meli za ndani na usajili wa meli za nje zinazopeperusha Bendera ya Tanzania. Kwamba mtu yuko nje ya Tanzania ana meli yake, lakini anataka atumie Bendera ya Tanzania. Usajili huo unafanywa na Mamlaka Zanzibar ndiyo tulivyokubaliana, usajili wa meli za ndani unafanywa na SUMATRA. Sasa kulitokea changamoto ya kutokuwepo na uangalifu na umakini katika usajili wa meli za nje zinazopeperusha Bendera ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kilichojitokeza ni kwamba meli zinazopeperusha Bendera za Tanzania zilikutwa nje ya nchi zinafanya makosa makubwa, kubeba silaha, magendo, madawa ya kulevya na kupaki kwenye Bandari zisizoruhusiwa. Kwa hiyo, Serikali ambacho tumeamua kufanya siyo kuinyang’anya Zanzibar mamlaka ya usajili hapana, kwamba hili jambo la usajili tushiriki wote. Kwamba asiwe mtu Dubai ana muhuri tu yeye anagonga tu na kukabidhi bendera, lazima vyombo vya Usalama vya nchi vishiriki, kwa sababu tunapotoa bendera yetu, ni alama ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tulikubaliana kwamba wenzetu watafanya lakini wasifanye peke yao kuwe na input ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama na due diligence wa meli zote zinazoomba kutumia Bendera ya Tanzania. Kwa hiyo, hicho ndicho kinachofanyika na wala wenzetu Wazanzibari wasione tunawapora na kwa kweli ni muhimu haya mambo kuyajua kabla ya kuyasema, kwa sababu yanaamsha hisia ambazo si sahihi.
Mheshimiwa Spika, la mwisho ni Kisiwa cha Fungu Mbaraka au Latham; kwamba Mheshimiwa Dkt. Ally Yussuf Suleiman alisema kwamba Tanzania Bara inataka kupora Kisiwa hiki kwa sababu kuna rasilimali. Labda niseme kwamba nchi yetu ni moja hatujafikia mahali pa kugombea eneo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, kinaitwa Fungu Mbaraka au Latham kipo katikati hapa Bahari ya Hindi. Kwa hiyo, kuna dhana inajengeka kwamba kuna mgogoro kati ya Bara na Zanzibar kuhusu umiliki wa Kisiwa hicho.
Mheshimiwa Spika, chanzo cha mgogoro ni kwamba inawezekana eneo lile lina mafuta. Sasa hii dhana inaenea na inaamsha hisia. Sasa niseme tu kwamba huko nyuma wakati suala la mafuta ni la Muungano na TPDC ndiyo ilikuwa inatoa leseni ni kweli pale mahali palitolewa blocks za kuchimba, kutafuta mafuta.
Mheshimiwa Spika, bahati mbaya wale waliyotafuta mafuta hawakuyapata, kwa hiyo wakarudisha zile block, kwa hiyo, mpaka leo lile eneo halina mtu anayetafuta mafuta. Kwa hiyo dhana kwamba tunagombea eneo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siyo sahihi, Katiba zetu ziko wazi kuhusu maeneo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na nchi yetu hii ni moja, Zanzibar ikinufaika Tanzania imenufaika, Bara ikinufaika Tanzania imenufaika.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba kwa wenzetu Wanzazibari na Watanzania kwa ujumla kusijengeke dhana kwamba tunagombana kuhusu eneo lolote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho, umezungumza kuhusu lugha humu ndani za ukabila na ukanda na mengineyo. Hata hivyo, kuna moja ambalo ni muhimu kulizungumza lugha zinazohusu Muungano wetu. Namna ambavyo tunauchangia na kuuelezea Muungano wetu ni kana kwamba bado hatujakubaliana kuhusu umuhimu wake na kwamba tumeamua kuungana. Kuna lugha kali sana ambazo zinafadhaisha watu wa upande mmoja na kudhalilisha upande mmoja au mwingine.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ningependa utumie rungu lako na kiti chako na joho lako na busara zako kukemea hizi lugha ambazo zina-condemn kwa ujumla watu wa upande mmoja au mwingine kuhusu Muungano. Muungano wetu sisi tumeamua kuwa nchi moja, tumeamua kuwa jeuri na kutengeneza mipaka yetu ya Tanzania. Kwa hiyo, naomba urithi huo tuulinde na Bunge lako lichukue uongozi katika kuulinda urithi huo.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.