Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibaha Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kumshukuru Mungu kwa kunifikisha mahali hapa salama ili na mimi nichangie hotuba hii muhimu ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya mwaka wa fedha 2018/2019. Ninaipongeza Wizara pamoja na wataalam wake kwa kuandaa bajeti nzuri. Bajeti hii inakwenda kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya maliasili na utalii.
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii pia kwa kuanza kuipongeza Serikali hii ya Awamu ya Tano kwa jitihada zake za dhati kabisa katika kukuza utalii na kuhakikisha sekta hiyo inaimarika na kuliingizia Taifa pato. Tanzania ni nchi ya pili duniani kwa kuwa na vivutio vya kihistoria, nafasi hiyo ni muhimu sana kwa Taifa na hatuna budi kuitumia ipasavyo kuandaa mikakati mbalimbali ya kimapinduzi katika sekta hii ya utalii ili ilete matokeo chanya.
Mheshimiwa Spika, Tanzania tumebarikiwa kuwa na vivutio hivyo ambavyo havipatikani mahali pengine popote duniani ila ni hapa nchini kwetu. Mikakakati ya kuvitangaza kwa kutumia njia mbalimbali ndiyo njia pekee itakayotusaidia kusikika duniani kote na kupata wageni watakaokuja kutembelea vivutio vyetu na kuliingizia Taifa letu fedha za kigeni pamoja na kutoa ajira kwa watu wetu ambao watahudumu kwa wageni hao. Serikali imejitahidi sana kuliangalia hilo, lakini tukiwa kama sehemu ya Serikali hatuna budi kuishauri pale tunapoona changamoto zinajitokeza hasa ambazo zinarudisha juhudi hizi muhimu.
Mheshimiwa Spika, naomba kuishauri Serikali kuzidisha matangazo mbalimbali katika maeneo mbalimbali duniani hasa kuvitangaza vivutio vyetu ipasavyo. Tukiwatumia mabalozi wetu katika mataifa mbalimbali wanayotuwakilisha itatusaidia sana kuvitangaza vivutio hivyo na kupata watalii wengi. Aidha, Serikali ije na mkakati wa kuvitangaza vivutio vyote vilivyosahaulika kwani tuna vivutio vya kitalii katika maeneo mbalimbali nchini. Vivutio vya kihistoria ambavyo vimesahaulika sasa ni wakati muafaka kwa Serikali kuvitangaza ili tuweze kupata wageni wa kuvitembelea.
Mheshimiwa Spika, aidha, ninaipongeza Serikali kwa juhudi kubwa ilizoweka na kufanikisha ongezeko la watalii kuja nchini kwetu kwa mwaka 2017 ambapo idadi imefikia milioni 1.33 ikilinganishwa na watalii milioni 1.28 mwaka 2016. Hii imepelekea mapato kuongezeka na kufika dola za Marekani bilioni 2.19 mwaka 2017 ikilinganishwa na dola za Marekani bilioni 2.13 kwa mwaka 2016. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia sita, ni hatua muhimu na zinaonesha kuwa sekta hii ya utalii ikijengewa mikakati madhubuti basi italiingizia Taifa letu pato kubwa na kuwezesha maendeleo kuja kwa haraka na hivyo uchumi kukua.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu imebarikiwa kwa kuwa na misitu pamoja na maliasili mbalimbali na Serikali imekuwa ikifanya juhudi kubwa kuyalinda maeneo hayo ya misitu, wanyamapori, malikale, uvuvi, ufugaji nyuki, pamoja na kuhakikisha kwamba rasilimali hizo zinanufaisha vizazi vya sasa na vya baadae.
Napenda kuipongeza Serikali kwa kuchukua hatua za kuimarisha mifumo ya kukusanya mapato katika sekta hizo, kupambana na ujangiri, kuzuia upotevu wa mazao yatokanayo na misitu na kutatua migogoro ya mipaka kati ya hifadhi na vijiji. Hizi ni hatua nzuri na za kupongezwa zinazoendelea kufanywa na Serikali yetu katika mikakati endelevu.
Mheshimiwa Spika, lakini bado kuna changamoto katika maeneo mbalimbali ya uchomwaji wa misitu, uvunaji wa magogo kiholela na kutokutolewa kwa elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya upandaji miti.
Mheshimiwa Spika, tukianzia suala zima la uchomaji wa misitu kiholela limepungua kwa kiasi kikubwa, lakini kuna baadhi ya maeneo changamoto bado inajitokeza. Wizara ichukue hatua mbalimbali za kukomesha majanga haya yanapotokea kwani huharibu mazingira hasa kwa baadhi ya maeneo ambayo yana viumbe hai na kwamba hupelekea viumbe hao kuhama.
Mheshimiwa Spika, ni wajibu wa Serikali na taasisi zake za kichunguzi zinazohusika na masuala mbalimbali yanayohusiana na Wizara hii, kuchukua hatua za haraka. Pale kwenye taarifa ama namna yoyote itakayoonesha au kudhihirisha kuna watu wanahujumu sekta yetu hii basi wachukuliwe hatua kali za kisheria na si kuachwa, watu hawa wakiachwa watalipeleka taifa letu katika mgogoro wa kimataifa ama kwa kuharibu mazingira, kuua wanyama wa mwituni na mengineyo yanayofanana na hayo.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.