Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Masoud Abdalla Salim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtambile

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala aliyetujalia uzima na afya njema katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani, tuwatakie sote tunaofunga Mwenyezi Mungu a-taqabbal funga zetu, atulipe ujira mwema, na Insha Allah bi-idhinillah malipo ya kheri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mhehimiwa Waziri muhusika, tatizo la mahujaji waliosota, waliokaa muda mrefu wakati wanakwenda Hija mwaka uliopita tatizo hili lisirejee tena. Ilikuwa ni aibu kubwa, tatizo kubwa, lilileta taswira mbaya miongoni mwa watu mbalimbali. Wizara husika ni Wizara hii hii. Kwa watu wote wanaoshughulika na kwenda nje kwa vyovyote iwavyo bado Wizara ya Mambo ya Nje inahusika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu wazi wazi; tumekuwa tukipiga kelele kwamba wameiandikia BAKWATA tena kuwapa Mamlaka na madaraka ya kuwapeleka watu Mahujaji hawa kwenda kuhijji, tafadhali sana BAKWATA kama Taasisi nyingine kwa hiyo msiwape mamlaka, yakitokea mambo mengine hasa tutasema kwamba BAKWATA ni sehemu ya Serikali na ndivyo inavyonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunachosema ni kwamba waacheni taasisi nyingine za kidini ziandae utaratibu wake wa kupeleka mahujaji Makka, ndiyo nikasema sasa ni vyema tujitathmini na hili. Upungufu huu wa kupeleka Mahujaji Makka dosari hii isitokee tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, APRM (African Pear Review Mechanism), mpango wa kujitathmini wenyewe kiutawala bora, kisiasa, kiuchumi na mambo mengine. Nashukuru kwamba wameongeza fedha. Hata hivyo, nataka Mheshimiwa Waziri aniambie kisiasa wamejitathmini kiasi gani kwa wakati huu pale ambapo mwendelezo au wanakaa mahabusu muda mrefu Mahakamani, unaambiwa upelelezi haujakamilika. Masheikh wa Uamsho wamekaa muda mrefu, juzi tu Mheshimiwa Waziri alisema kwamba ushahidi umepatikana, wanasubiri e-mail kutoka nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi watu wanakaa mahabusu miaka minne, miaka mitano hili hawalioni, wanataka tafsiri nyingine zije tafsiri za aina gani? Masheikh wa Uamisho wamekaa muda mrefu sana. Kwa hiyo wanajitathmini kiasi gani? Amesema Mheshimiwa Bwege mpaka akatoka machozi. Watu wamepigwa risasi Msikitini kule Chumo, damu imemwagwa msikitini Chumo. Tafadhali sana, hakuna kitu kibaya katika mambo haya ya hisia za dini. Waliopigwa risasi kule Chumo msikitini liwe jambo la mwisho tafadhalini sana. Mheshimiwa Mahiga anifahamu na walionifahamu wanifahamu, wale Taasisi za Serikali za kiulinzi wanifahamu, risasi msikitini isilie tena maisha, tafadhalini sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina suala lingine ambalo ni juu ya mahusiano yetu ya mambo ya nje na Mataifa mbalimbali uko vizuri. Nafahamu uhusiano mzuri tulionao sisi na Msumbiji, nafahamu jinsi Tanzania ilivyoshiriki katika ukombozi ule wa Msumbiji, nafahamu mambo mengi mazuri yetu sisi na Msumbiji na mimi naunga mkono. Kuna Watanzania ambao wako gerezani kule Msumbiji katika Gereza la Beyo kule eneo la Pemba ambao wako gerezani hasa kwa muda wa miezi sita. Hawa ni wapiga kura na kwa mahusiano mazuri sisi na Msumbiji na nadhani nampongeza sana Balozi wetu Monica hapa leo yupo hongera, sana nampongeza sana Balozi Monica. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu hawa naomba sana niwataje kwa majina wapo Beyo hapo Msumbiji kwenye Gereza hilo. Kwanza kutoka Jimbo la Kiwani na Mtambile Jimboni kwangu na hawa wamefanya makosa madogo madogo tu, hawana yale makosa makubwa ukasema makosa yale labda ya madawa ya kulevya; nao ni Shahali Makame Omary wa Chole-Kiwani; Fadhili Khamisi Makame, Chole-Kiwani; Khamisi Fadhili Khamisi, Chole-Kiwani; Mussa Rare Mussa, Chole-Kiwani; Ally Zidini Ngali, Chole-Kiwani; Zahoro Ngwali Ally, Chole-Kiwani; Zaharani Fadhili Khamisi, Chole-Kiwani; Silima Yakoub Ally, Chole-Kiwani; Ally Shahali Makame, Chole-Kiwani; Mbarouk Hijja Silima, Chole-Kiwani; na Juma Tabu Mussa, Chole-Kiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Jimbo la Ziwani kuna Abdallah Khalfani, wa Wesha; na Hamza Fikira Sharif, wa Wesha. Kuna Jimbo la Mkoani nako kuna Makame Burhani Kombo, wa Chokocho; na Faki Shahali, wa Chokocho. Donge-Unguja yuko Mselem Khalfani Mohamed na Chumu Mshenga, hawa wako kwenye gereza la Beyo huko Pemba-Msumbiji. Tafadhali sana, kwa ujirani tulionao na ubora wa Balozi wetu Monica ninavyomwona yuko vizuri sana, hongera sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hili jambo walichukue, utaratibu wa nchi nyingine wanakuwa wanafahamiana, utaratibu wa kuwarudisha mahabusu au wafungwa kutoka nchi hizo sembuse hapo jirani tu. Naombeni sana hawa watu waandae mazingira mazuri waweze kuwarejesha. Nina imani kwa ujumbe huo Mheshimiwa ataweza kufanya jambo lolote la msingi la kuweza kufanya shughuli zinazohitajika.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye jambo lingine la tatu ambalo ni miradi ya maendeleo. Mara nyingi tunasema kwamba baadhi ya miradi ya maendeleo inataka itekelezwe kwa wakati wake. Kuna miradi inayopaswa kutekelezwa katika Visiwa vya Unguja na Pemba yaani Zanzibar. Mpiga duru yupo katika mikakati, naomba sana Mheshimiwa Waziri aliangalie suala la mpiga duru.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni miaka kadhaa wamekuwa wakisema kwamba wana mpango mkakati wa kuboresha uwanja wa ndege Pemba, lakini kila mara wanataja, wanataja katika mipango yao hii ya kiujumla katika bajeti hii ya Afrika mashariki. Ni kwa nini na ni sababu zipi za msingi zilizopelekea uwanja wa Ndege, Pemba haupewi kipaumbele ukapewa nafasi yake ili ile dhana ya uchumi unaohitajika ukaendelea, tatizo ni nini? Pemba ipo Tanzania nataka wafahamu haiko sehemu nyingine yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bandari ya Mkoani walisema muda mrefu kwamba nayo wataiboresha, watakwenda vizuri lakini hadi leo inaonekana bado ni danganya toto. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa aniambie habari ya mpiga duru, aniambie habari ya uwanja wa Ndege wa Pemba, anipe habari rasmi ya Bandari ya Mkoani na Bandari ya Wete. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, atumishi ambao wako katika Balozi inafika wakati Maafisa huwa hawapeleki kwa wakati na ile dhana ya diplomasia ya kiuchumi inakuwa inasuasua. Naomba waniambie sasa kwamba kwa nini wanakuwa na kigugumizi cha kupeleka Maafisa kwenye Balozi kwa haraka haraka pale ambapo wengine wameshamaliza muda wao. Anipe habari, nataka kujua kule Ankara, Uturuki, anipe habari ya Korea, Doha-Qatar, Brussels ambapo kuna vikao vingi ya European Union nako sasa hawapo au ni kidogo sana. Addis Ababa napo ni tatizo, New York nako vilevile.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hili tatizo ni lini wataweza kulisawazisha kwamba tunasema tuna economic diplomacy (diplomasia ya kiuchumi) lakini Maafisa wale wa Ubalozi ambao wanahitajika kwenda kule hawako, sasa hili nalo ni tatizo. Sasa Mheshimiwa Waziri aniambie jambo hili ni lini litakaa vizuri.

Mheshimiwa naibu Spika, la mwisho, tuepukane na aibu kubwa ambayo tunaipata kwenye vile viwanja ambavyo haviendelezwi. Majengo ambayo wanataka kuyakarabati hapa yapo, lakini kila wakati tunaweka bajeti tu lakini fedha zile hazipelekwi. Kwa hiyo atuambie sasa mkakati wa kuepukana na aibu ni upi. Leo tunaambiwa kwamba Tanzaia itashtakiwa katika nchi husika kwamba majengo yale ni machakavu, mabovu na viwanja haviendelezwi. Nimwambie Mheshimiwa Waziri, hii ni aibu kwa Taifa kama letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vyema sasa tujifunze, tuepukane na aibu kwa nchi za nje, tunajitia aibu sisi wenyewe kwa sababu hatupeleki zile fedha. Kama ingekuwa tunaona kwamba kuepuka aibu Mataifa ya wenzetu wasiweze kututafsiri vinginevyo, basi majengo hayo tungeyakarabati, tungepeleka fedha na vile viwanja ambavyo vilitaka kuchukuliwa ambavyo vimekuwa ni pori na tunataka kushtakiwa ile aibu sisi tungekuwa hatunayo. Naomba sana Mheshimiwa Waziri, kwa sababu Serikali ni moja waandae mazingira kuona kwamba majengo yetu yanakarabatiwa, fedha zinapelekwa na vile viwanja ambavyo vinatia aibu, aibu hiyo inaondoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie la mwisho, ni hati za utambulisho (Present Credential), wamepanga mara kadhaa Mheshimiwa Naibu Waziri, hizi hati za utambulisho katika maeneo ambayo tumepanga basi tufanye kweli.