Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima kubwa kupitia Bunge hili Tukufu naomba nitoe shukurani za dhati kwa Mheshimiwa David Silinde, Mbunge wa Momba mwanatimu ya mapambano kwa mashirikiano na juhudi zake amefanya kazi kwa moyo wa kijasiri na kwa kujitolea mpaka kuhakikisha ushindi wa Mheshimiwa Mboni Mhita, Rais wa Caucus ya vijana, Mheshimiwa Stephen Masele, Makamu wa Rais wa Bunge la Afrika wamepata ushindi na kuIletea nchi yetu heshima kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa taarifa yako kamanda wa jeshi hilo la ushindi si mwingine isipokuwa ni mimi mwenyewe Asha Mshuwa na nampelekea salamu Mheshimiwa Dkt. Magufuli japokuwa mimi hakunialika mimi na Mheshimiwa Silinde lakini sisi ndio tuliofanya mapambano ya infantry na ya air wing.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la heshima kwa viongozi hawa wawili tulioweza kupata ni vile wameahidi kwamba watatumia lugha ya Kiswahili katika kuendesha shughuli katika Bunge la Afrika. Hii ni turufu kubwa na heshima kwa Tanzania yetu. Tanzania hoyee.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante nakubali. Katika hotuba Waziri amezungumza sana kuhusu diaspora na vile wanavyoweza kuchangia. Ni kweli wana-diaspora wameongezeka na uchumi wao huko waliko ni mzuri, hivyo wana nafasi kubwa kuchangia hapa kwetu. Sasa Serikali irahisishe mazingira ya wao kuweza kuwekeza hapa nchini Tanzania, kwa hili bado halijawa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, iko mifano kadhaa ya nchi ambazo zimeweza kuwatumia diaspora na kuendeleza na kunyanyua uchumi wa nchi hizo na kipato cha familia zao. Hasa kwa kuzingatia kama watu hawa wana uchumi mzuri na wanapata experience na exposure za kutoka katika nchi zile.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo linanikereketa na naomba Serikali inisaidie na tuweze kupata ufumbuzi ni hili suala la uraia pacha (dual citizenship). Suala hili tuiombe Serikali ilifanyie tafakari upya na kulipatia utekelezaji japo kwa masharti. Ikiwezekana basi kama wasiwasi wa kiusalama basi tuweke vipengele ambavyo vitazuia watu hawa wasiingie katika mistari ya kupiga kura au kuhatarisha usalama wa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nafikiria na napendekeza kwamba, basi tutazame uwezekano wa kufanya kama ule mfano ambao wanatumia India. India wao hawana duals citizenship lakini wanao utaratibu unaotiwa Person of India Origin, Wahindi hao wanapewa utambuzi ambao unawapa haki sawa isipokuwa hawawezi kupata uraia.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa jambo kama hili kwa kutumia watalaam wao watafute namna kama kuwa na timu kabambe kama zile za makinikia ili tuweze kuwasaidia hawa vijana wetu ambao wako nje huko na wanapoteza nguvu kazi nyingi sana, ambao wana nia hasa ya kuendeleza rasilimali katika Tanzania yetu na hasa hivi tunavyotaka Tanzania ya viwanda hawa watu naamini wanao uwezo sana wa kutengeneza viwanda hata vidogo vidogo. Mbona hamnipigii makofi, hamtaki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya ombi hilo la kuiomba Serikali, sasa naomba tena suala la pass ya diplomatic. Diplomatic Pass imetoka agizo kwamba wasipewe wenza. Sasa naomba Serikali ifikirie jambo hilo kwa sababu inakuwa haipendezi unasafiri na mkeo au na mumeo japo mimi sina mume l akini nawasemea wenzangu wenye waume. Wewe mke unakwenda huku, mume anakwenda kwingine inakuwa haipendezi na haijengi heshima ya nchi. Hata hivyo, tutazame kwa wale watu ambao wanaongeza wake wengi waliozidi, waliozidi wanne au ishirini, basi waambiwe awekewe wake zake wawili tu. Kwa sababu tukisema apewe mke mmoja hapa nitaingilia utaratibu hata Mzee Ally Hassan nitakuwa nimemwingilia kwa hivyo atakuwa haweze kuwachukulia wake zake wote wawili.
Sasa nasema kwa sababu ukisema apewe mke mmoja tu au mume mmoja inaweza kuleta tatizo kwa sababu mzee wetu wa heshima baba yetu Rais wetu Ali Hassan anao wake wawili. Sasa utakuwa upendeleo ukisema mmoja aende. Kwa hivyo wakae watazame namna gani wata-sort out jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kuzungumzia ni kuhusu viwanja vya ubalozi. Nchi yetu tulipata heshima kubwa na viwanja vingi tulipata kwa heshima ya mwenyewe hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, lakini viwanja vingi mpaka hivi sasa hivi bado havijaendelezwa. Sasa tubadilike tutafute namna hata kushirikiana na investors wengine sio tu haya majengo yawe kwa ajili ya ubalozi lakini tuweze kufanya shughuli nyingine kwenye majumba yale kujenga ofisi, kupangisha na kufanya ubalozi. Maana yake hiyo tunu tuliyopewa mwisho itapotea, nyota ile tuliondoka nayo itapotea, majengo yetu mengi hayako katika hali nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutumie hii nafasi ya kidemokrasia ya kiuchumi kushawishi ili tuweze kuviendeleza viwanja hivyo, lazima kuwe na uwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko makubwa fedha zilitengwa kwa mfano wa kujenga jengo la Oman lakini hazikuweza kupatikana. Sasa nataka nishauri kwa vile Oman ni rafiki zetu sana na nimeona hapa kwenye hili ripoti wanasaidia kukarabati Bete la Jaibu basi tutafute namna kwa kushirikiana kwa mazungumzo kama vile wafalme wengine wanaweza kuja kutujengea uwanja au kama marehemu Gadafi alivyojijengea misikiti na hao watusaidie kujenga hili jengo la ubalozi pale Oman itatusaidia sana.
Naomba kuunga mkono hoja.