Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Tanga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema. Pia nawatakia Waislam wote Tanzania na duniani kwa ujumla Heri na Baraka ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mahusiano ya Kimataifa; Tanzania bado ni nchi inayotambulika kuwa bado amani na utulivu unapatikana, lakini kadri siku zinavyokwenda mbele Tanzania inapoteza heshima na umuhimu tunaopewa na dunia. Mfano, moja, demokrasia inaminywa kwa kutoruhusiwa mikutano ya hadhara ya Vyama vya Siasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mbili, maiti zinazookotwa katika mito na fukwe za bahari na mito na Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani, Waziri Mwigulu Nchemba anajibu bila shaka hao maiti ni wahamiaji haramu. Napata shaka dunia itatuelewaje Watanzania? Je, wahamiaji hawatakiwi au tumepitisha sheria ya kuwaua hao wahamiaji haramu?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Waziri Mheshimiwa Dkt. Mahiga alijibu Bunge na kutoa tafsiri sahihi kwa kuwa badala yake Watanzania waishio nje ya nchi (Diasporas) wanaweza kudhuriwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania waliofungwa nje; katika nchi nyingi duniani, Watanzania katika kutafuta maisha, wanapatikana na hatia mbalimbali kama vile:-
(a) Kuishi bila ya “Permit” au “overstay” baada ya VISA kuisha na kufungwa magerezani.
(b) Wanaotuhumiwa kujihusisha/kushirikiana na wafanyabiashara wa dawa za kulevya. Mfano, familia ya Tanga iliyokamatwa China na mtoto wao wa miaka mitatu kurudishwa nchini kutokana na tuhuma za dawa za kulevya.
(c) Wanaokwenda kutafuta ajira za viwandani, mashambani na majumbani.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali, je, Serikali ina mpango gani wa Kidiplomasia wa kubadilishana wafungwa ili warejeshwe Tanzania kuhukumiwa kwa Sheria zetu?
Mheshimiwa Naibu Spika, viwanja vya Ubalozi tunavyovitelekeza; kwa masikitiko makubwa, natoa hoja hii nikiwa bado nashangaa kuwa Serikali ya Kifalme ya Oman imetupa Kiwanja “Low Density” huko Muscat, lakini mpaka leo tumeshindwa kukijenga. Nashauri Serikali itafute fedha na kujenga na kuondoa aibu hii inayochafua Taifa letu.