Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibaha Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuanza kwa kumshukuru Mungu kwa kunifikisha mahali hapa salama ili nami nichangie hotuba hii muhimu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Mwaka wa Fedha 2018/2019. Naipongeza Wizara pamoja na wataalam wake kwa kuandaa bajeti nzuri. Bajeti hii itatekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika kuhakikisha nchi yetu inaimarisha ushirikiano na mahusiano mazuri na mataifa mengine duniani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa juhudi mbalimbali inazochukua katika kuimarisha mahusiano yetu na mataifa mbalimbali duniani, ni hatua nzuri na ya kupongezwa, hatua hiyo italiwezesha Taifa kufaidika na masuala mbalimbali ya kimaendeleo na mataifa hayo. Juhudi hizo zitasaidia pia kulitangaza Taifa letu na kuvitangaza vivutio vyetu na kuvutia watalii, wawekezaji kuja nchini kuangalia fursa mbalimbali tulizokuwa nazo za kiuwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya kufungua ubalozi mpya nchini Israel ni ya kupongezwa. Taifa hilo limepiga hatua kubwa kimaendeleo, uchumi, viwanda na teknolojia. Ubalozi huo utatuweka karibu, kushirikiana katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo. Naishauri Serikali kupitia Wizara hii kuwakumbusha Mabalozi wetu wote wanaotuwakilisha katika nchi mbalimbali, kutumia fursa hiyo kuvitangaza vivutio vya kitalii tulivyo navyo na fursa mbalimbali za kiuwekezaji zilizopo nchini, hatua hiyo itasaidia sana kunufaika kama nchi kwa sekta husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Umoja wetu wa Afrika Mashariki unazidi kuimarika na kuleta taswira nzuri ya kimaendeleo. Watu wetu wanaendelea kufaidika na ushirikiano huo kwa kiasi kikubwa, wafanyabiashara wetu wanavuka mipaka na kushirikiana na wenzao katika biashara mbalimbali. Hii ndiyo dhana ya ushirikiano huu ambao una tija kwa kila Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto hazikosekani, hivyo naishauri Serikali kuziangalia kwa jicho la pekee changamoto zote na kuzipatia ufumbuzi ambao utaleta malengo chanya kwa mataifa yote wanachama.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.