Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Mtwara Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MAFTAH A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Mwenyezi Mungu, Subhanahu wa taala, Mwenyezi Mungu ambaye ameendelea kunipa afya njema. Asiyeshukuru kidogo basi hata akipewa kingi hawezi kushukuru. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tulikuwa Mtwara na Lindi tukiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa Dkt. Kalemani tumeenda kuzindua umeme, sasa hivi Mtwara na Lindi tumeunganishwa kwenye Gridi ya Taifa, tunashukuru sana. Tunashukuru sana kwa sababu na sisi sasa tumewekwa miongoni mwa Watanzania maana kwa miaka mingi tumekuwa tukililia suala la Mikoa ya Kusini kuunganishwa na Gridi ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru kwamba Mtwara Mjini hivi sasa tumezindua pia mashine mbili mpya ambazo zitaenda kutoa megawati nne za umeme lakini bado mpaka leo hazijaunganishwa sawasawa, tumeenda kuzindua tu. Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri kwamba zile mashine sasa zianze kufanya kazi kwa sababu ile juzi tukiwa pale Mtwara bado umeme usiku ulikatika kwa sababu zile mashine bado hazijaanza kufanya kazi. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri Dkt. Kalemani mashine hizi sasa ziunganishwe na mashine zingine zile tisa tuweze kuondoa tatizo la kukatika kwa umeme mikoa hii ya Mtwara na Lindi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze suala hili ambalo nimekuwa nazungumza kwa muda mrefu ndani ya Bunge hili na huu ni mwaka wangu wa tatu nazungumza haya. Kumekuwa na eneo ambalo tunasema ni mkuza wa gesi ambapo bomba la gesi limepita na ikumbukwe Mikoa ya Mtwara na Lindi na hasa Jimbo la Mtwara Mjini, wananchi waliandamana wakapigwa risasi wengine wakauwawa wakidai kujua namna gani hii gesi itaweza kuwanufaisha, tukawa tumeahidiwa sana. Miongoni mwa ahadi za Serikali zilikuwa ni kupewa umeme wa uhakika. Kwa hiyo, tunashukuru sasa hivi hili linakuja kutekelezwa lakini tunaomba kuwe na kasi ya kusimika zile mashine umeme usikatikekatike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwenye haya maeneo ni ule mpango wa Serikali, waliambiwa wawapelekee wananchi nguzo za umeme lakini walichofanya ni kupeleka nguzo chache sana kwenye huo mkuza wa gesi kwa maana ya maeneo lilipopita bomba la gesi ambapo Serikali ilisema lazima wale wananchi wapate umeme. Maeneo ya Mtwara Mjini, Lindi na maeneo mengine lakini kilichofanyika Serikali imepeleka nguzo chache sana, wananchi wengi katika maeneo yale hawajapata umeme. Wakitaka kulipia umeme wanalipa kwa bei kubwa sana, nguzo wanunue kwa Sh.500,000, kitu ambacho Serikali ilishasema kwamba wale watu watapelekewa nguzo kwa sababu bomba la gesi limepita mule waweze kuunganisha umeme kwa Sh.27,000 lakini kinachotokea ni kinyume kabisa nguzo zimeenda chache sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo ya Jimbo la Mtwara Mjini, kwa mfano, Mtawanya bomba la gesi limepita mule nguzo za umeme hazijaenda kabisa, maeneo ya Magomeni, pale pale Mtwara Mjini baadhi ya maeneo nguzo hazipo. Kuna maeneo ya Chipuputa hakuna nguzo za umeme, kuna maeneo ya Kiholo, Komoro pale Mtwara Mjini, Mbaye na Mitengo, kote huko bomba la gesi limepita na Serikali iliahidi itapeleka umeme maeneo yale lakini nguzo zimeenda chache sana na wananchi wa wakienda kuomba TANESCO wanaambiwa hapa nyie ni mjini, kwa hiyo, mnalipia Sh.500,000 nguzo na ukilipa hiyo Sh.500,000 ndiyo tutakupelekea umeme. Sasa tunaenda kinyume kidogo na ahadi na nia ya Serikali. Yawezekana wakati mwingine Mheshimiwa Waziri hayajui haya lakini watendaji kule wanafanya haya, wananchi wananiagiza mimi kila siku na ndani ya Bunge hili nimekuwa nazungumza sana. Naomba sana Wizara iangalie maeneo haya ambayo yalikuwa ni ahadi ya Serikali kupeleka umeme kutokana na kupatikana kwa gesi hasa katika maeneo ya ule mkuza wa gesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna maeneo pia ya pembezoni kwenye miji hii iliyopo Mtwara na Lindi, maeneo yale ambayo mwanzo kabla mji haujatangazwa kuwa Manispaa yalikuwa ni maeneo ya vijijini lakini yale maeneo yakaingizwa kwenye Manispaa lakini kumekuwa na tatizo sana la umeme na tumekuwa tunaongea sana. Ndani ya Bunge hili nimeongea sana yale maeneo ya pembezoni ambayo sasa hivi ni mitaa mwanzoni yalikuwa ni vijiji wapelekewe huu mpango wa umeme ambao Serikali inasema imeweka mkakati wa kusambaza umeme, tunasema diversification of electricity yaani yale maeneo yapelekewe isije ikawa tunatumia sana vyombo vya habari kuzungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwenye hii hotuba leo imetaja sana Mtwara na Kusini, nimekusikia sana Mheshimiwa Waziri Kalemani lakini sasa tunaomba haya maeneo umeme upelekwe kwa sababu unaambiwa na watendaji kwamba huku tunafanya kila nikikuuliza Waziri unaitikia sana unasema bwana nimepewa taarifa kwamba tunapeleka na mwaka jana uliniahidi Mheshimiwa Waziri kwamba utakuja Mtwara nikupeleke kwenye maeneo niende kukuonesha haya ninayozungumza lakini haujafika. Nikuombe mwaka huu baada ya bajeti mguu kwa mguu wewe na Naibu Waziri wako Mheshimiwa Subira anaijua sana Mtwara, kakaa sana Mtwara huyo, tunatembea mguu kwa mguu, niite mkutano wa hadhara wananchi wakupe kero hizi ambazo wananiagiza kila siku wananchi wa jimbo la Mtwara Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, safari hii kama Waziri hautaniahidi kwamba utapeleka umeme nang’ang’ania shilingi yako. Maeneo haya ni maeneo ya Mbawala Chini narudia tena Bunge hili limekuwa linanisikia sana nikiyataja, Mbawala Chini uende umeme, mfanye diversification kwenye maeneo haya. Kuna maeneo ya Kijiji Naulongo au Mtaa wa Naulongo pelekeni umeme, kuna eneo la Mkunjanguo mpaka watu sasa wananitania ndani ya Bunge wananiita Mkunjanguo kwa sababu nilikuwa nazungumza sana . (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri haya maeneo yazingatie peleka nguzo za umeme wananchi wanataka umeme, ndio manufaa yenyewe ambayo mmetuambia wananchi wa Mtwara. Kuna maeneo ya Namayanga, Dimbuzi, Mkangala tunaomba umeme muupeleke kwenye maeneo haya. Nimekuwa nalia sana, naagizwa sana, kila siku nikifanya mkutano wa hadhara wananchi wanalia sana kwenye haya maeneo. Kwa hiyo, niombe sana mlishughulikie suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala hili la punguzo la umeme. Tuliahidiwa kwamba pamoja na mambo mengine manufaa ya umeme Mikoa hii ya Kusini Mtwara na Lindi kwamba kuna gesi tutapunguziwa umeme, wananchi wakaacha kuandamana. Wananchi wamenituma kwa mara nyingine nije kuzungumza ndani ya Bunge, kwa kuwa gesi bado ipo Mtwara na Lindi, lile punguzo tunaomba liendelee kuwepo msiliondoe. Kwa sababu sasa hivi wananchi wanavyoenda kuomba kuunganishiwa umeme wanaambiwa walipe Sh.390,000 wakati pale gesi bado ipo na punguzo lilikuwepo. Naomba hili punguzo wananchi wapewe, walikuwa wanaunganisha umeme kwa Sh.97,000 kwenye yale maeneo ambayo sio mkuza wa gesi tunaomba liendelee kwa sababu gesi bado Mtwara na Lindi ipo haijaondolewa katika mikoa hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuunganisha gesi majumbani tunashukuru kwamba Serikali imezungumza kwenye hotuba hapa kwamba Mtwara nayo ipo. Majaribio ya kuunganisha gesi majumbani yameanza Masaki Dar es Salaam wakati gesi yenyewe iko Mtwara, tunashangaa sana gesi imetokea Mtwara kwa nini wasingeanza pale kwanza au sisi wana Mtwara hatuna majumba ya kutumia gesi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana isije ikawa inazungumzwa sana kwa sababu nilishaliona suala hili kwenye Kamati wakati tunapitia taarifa ya TPDC mwaka juzi ndiyo nikaliibua nikawaambia Mikoa ya Kusini ambako inatoka gesi yenyewe kumesahaulika kabisa, ilikuwa haipo kabisa. Tunashukuru safari hii mmeweka na unatuambia kwamba tunaenda kupewa hii gesi tuweze kutumia kama nishati. Hii itapunguza matumizi ya mkaa na ukataji wa misitu kule. Kwa hiyo, tunaomba suala hili Mtwara Mjini, Lindi Mheshimiwa Waziri alizingatie kwamba wananchi wanahitaji gesi majumbani isiwe inazungumzwa tu halafu mnaanza Dar es Salaam, kule kwenyewe inapotoka gesi kunakuwa ni kizungumkuti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba kuzungumzia suala la viwanda. Serikali ya Awamu ya Tano inasema kwamba ni Serikali ya viwanda. Kusini kuna wawekezaji wanahitaji kujenga viwanda vya mbolea, Petrochemical, wanataka kujenga viwanda vya mbolea Mtwara na Lindi mpaka leo bado wanapigwa danadana tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri mwaka huu hawa watu wape gesi waweze kujenga viwanda vya mbolea kwa sababu viwanda vitatoa ajira kwa wananchi wa Mtwara na Lindi na sisi tutaondokana na umaskini kwa sababu gesi hii Mwenyezi Mungu ametupatia imeanzia pale. Wenzetu maeneo mengi ya Tanzania viwanda vimejengwa siku nyingi sisi tuna kiwanda kimoja tu cha Dangote nacho kinasuasua.
Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri safari hii unitekelezee mambo haya, ahsante sana.