Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Korogwe Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijachangia, nataka nirudie suala langu la jana naomba nishukuru watu wafuatao. Nimshukuru Mheshimiwa Spika, Katibu wa Bunge, Ofisi ya Uhasibu, Wabunge wote wa Mkoa wa Tanga kwa msaada walionipatia, Wizara ya Afya chini ya Mheshimiwa Waziri Ummy, pamoja na Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na rafiki yangu Ndassa kila wakati alikuwa anakuja kumuona mgonjwa pale Muhimbili. Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kazi kubwa ambayo wanayoifanya. Leo ilikuwa nichangie makubwa sana lakini kufuatana na hotuba na gawiwo walilokuwa wamelipata, Wabunge wenzangu tujaribu kuwaunga mkono hawa mabwana. Kwa sababu tulikuwa tunatarajia kwamba Serikali au Hazina ingetupatia fedha nyingi ili itusaidie katika suala la umeme lakini cha kushangaza ni kwamba hela zile nyingi hazikupatikana na Waziri anafanya kazi katika mazingira magumu na amekuja kwangu mara nyingi na amesema yale aliyokuwa anataka kuyafanya hayafanyiki kwa sababu hana fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuwashukuru sana wenzetu wa REA wanafanya kazi katika mazingira magumu. Hata hivyo, tuna mtihani Wabunge wote tuliokuwa hapa ndani, bila kukaa vizuri na Hazina wakatupa fedha hawa Wabunge hapa wameweka Ubunge wao rehani. Wakati wa mwanzo tulipewa orodha ya vijiji ambavyo vitapata umeme wa REA na Wabunge wakafurahia wakapeleka katika majimbo yao na kuonyesha kwamba umeme huu utafika kwa wakati fulani. Cha kusikitisha vijiji ambavyo vilipewa majina na Wabunge tukaenda tukavisemea na Madiwani wakaenda wakavisemea vimekatwa vyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, nina kata ishirini na tisa, kuna kata saba ambazo toka Uhuru hazijapata umeme. Mwaka huu ziliingizwa kwenye mpangilio wa kupata umeme, leo hii naambiwa zile kata hazina umeme, nina kwenda kuwaambia nini wapiga kura? Inasikitisha sana, nina Kata za Kizara, Kalalani, Mpale, Mswaha, Mkalamo na Folofolo toka Uhuru umeme wanausikia. Ukizingatia Wilaya ya Korogwe ina viongozi wakuu wanatoka pale. Kwa mfano, kata ambayo anatoka Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu, Kata ya Mkomazi haina umeme. Huyo Assad ambaye anawakagua hapa anatoka kwenye jimbo langu lakini kwake hakuna umeme. Ukienda Kata ya Mtindiro, Kijiji cha Mtindiro hakina umeme, ukienda vijiji vingine zilivyoko pale havina umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Askofu Mkuu wa Anglikana anatoka kwenye Jimbo langu, Mheshimiwa Mndolwa lakini leo hii umeme umepita nyumbani kwake, wameruka, wanakwenda kuangalia sehemu nyingine, mnatuweka wapi? Wabunge tutasema nini kwa wapiga kura? Keshokutwa mnataka tuwachague Wenyeviti wa Serikali za Vijiji watakwenda kusema nini kwa wananchi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi simlaumu kabisa Mheshimiwa Waziri, wala siwalaumu watu wa REA, wanafanya kazi katika mazingira magumu lakini huko Hazina kuna nini kibaya? Leo mnatuandikia hapa kwamba tunapokwenda kulipa bili TANESCO, REA wanakata asilimia 3, Ewura wanakata asilimia 1, nani anachukua hela hii? Leo hii kila tukisema hela, makandarasi wanasema hela hawajapewa, unaangalia ukienda kwenye mafuta tunakatwa hela, ukienda kwenye kulipia umeme tunakatwa hela, maji tunakatwa hela ya umeme leo hii tukikulaumu Mheshimiwa Waziri tunafanya makosa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Wabunge wenzangu tuungane tumsaidie hizi fedha ambazo zilikuwa zinazungushwa apatiwe tumaliziwe miradi yetu. Mheshimiwa umezunguka nchi nzima hii unawasha umeme lakini cha kushangaza katika vijiji vyote watu wamerundika nguzo tu ukiuliza wanasema hatujapewa fedha. Sasa tunaipeleka wapi hii nchi, tunapeleka wapi wapiga kura wetu? Mheshimiwa Waziri wa Fedha kama hizi hela zilikuwa haziendi REA au TANESCO, basi naomba tuondoeni hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wananchi wanatulalamikia wanasema Wabunge wanakwenda kulala, Wabunge wanaonyesha nia kwamba tunatetea umeme, umeme huo tunautetea ni upi? Kama umeme haupatikani, umeme haufiki, Waziri amekuja kwenye Jimbo langu wakati wa kampeni akasema sehemu ambazo zilikuwa hazina umeme upatikane. Kinachoshangaza sana Mheshimiwa Waziri, vile vijiji ambavyo ulisema vipate umeme havipati tena umeme kinapata kijiji kimoja eti hela hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kwenye Jimbo langu kuna mradi wa maji, kuna nguzo zimewekwa na TANESCO toka 2004 mpaka leo waya hazijawekwa. Tumekwenda na viongozi wa TANESCO wa Mkoa, viongozi wamekwenda pale wamenisemea, wananchi wamesikia leo wanakwambia umeme haufiki, mimi mnaniweka wapi na Wabunge wengine tunawaweka wapi? Hii ipo ndani ya Ilani ya Uchaguzi, kwa nini tusitekeleze haya mambo? Mheshimiwa Dkt. Kalemani ni mchapakazi wa hali ya juu sana, hebu tujaribu Bunge hili kuhakikisha pale mahali ambapo fedha za EWURA na REA, zilipokwamia zijaziwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mweyekiti, suala la pili ni la bomba la mafuta. Tuna kawaida mabomba ya mafuta au kitu chochote kizuri kinapokuja wananchi wanakuwa hawatengewi sehemu badala yake wanachukuliwa watu kutoka nje Watanzania tunabaki hivihivi. Mheshimiwa Waziri bomba la mafuta umekuja, umeliona, umetathmini, umetupa hamasa, watu hawa wote wanaopitiwa na bomba la mafuta naomba Watanzania wawe wa kwanza kupewa kazi. Kuna taratibu watu wanakuja na watu wao, Watanzania ambao watalilinda bomba lile hawapati kazi. Naomba Mheshimiwa Waziri, wewe ni msikivu sana na ni rafiki yangu sana lakini kwa leo naomba uhakikishe kwamba bomba la mafuta linalopita katika ile Mikoa yote Watanzania wa nchi hii wapate kazi kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nisisitize katika vijiji ambavyo mlikuwa mna-support kwamba vipate umeme Tanzania nzima, kwa kupitia mpango wa REA naomba virudishwe kwenye orodha. Mkurugenzi wa REA Maganga anakaimu, unafikiri atatoa maamuzi gani? Huyo Bwana Msofe ni mtu mmoja mzuri ukimpigia simu hata saa nane za usiku anakupokea, ukienda Mwenyekiti wa Bodi wa REA ni watu wasikivu, wapewe fedha ili hii kazi iishe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya machache, kwa sababu naumwa niliomba tu niwe mtu wa kwanza, naomba niwahi Muhimbili lakini naunga mkono asilimia mia kwa mia Waziri apatiwe fedha afanye kazi. Mungu awabariki sana, ahsanteni sana.