Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwimba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MANSOOR S. HIRAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru umenipa nafasi hii ili na mimi nichangie hoja ambayo iko mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema nisimame mbele ya Bunge lako Tukufu kuwawakilisha wananchi wa Jimbo la Kwimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa bajeti nzuri ambayo ameiwasilisha hapa Bungeni. Mimi nitajielekeza kwenye masuala ya REA III. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa mpango kabambe wa kupeleka umeme vijijini. Mheshimiwa Waziri, amezindua miradi mingi sana vijijini. Wilaya ya Kwimba tarehe 13 Julai, 2017 alizindua mradi wa umeme vijijini, jana ndiyo kijiji cha kwanza kimewasha umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu unasuasua sana, miezi nane kijiji kimoja ndiyo kimepata umeme. Tukifuatilia kwa mkandarasi anasema Serikali bado haijasaini mkataba wa kufungua LC, mara Hazina hajasaini mkataba. Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Mheshimiwa Waziri wa Fedha, tunawaomba mtusaidie, fedha za umeme za REA III ni ring- fenced tunaomba zifike kunakotakiwa ili miradi hii ya REA III isichelewe.
Mheshimiwa MWenyekiti, pamoja na hayo, wakati wa uzinduzi wa mradi huu tulifanya maboresho, kuna vijiji vingi na taasisi mbalimbali za Serikali na za kidini zilikuwa zimerukwa wakati wa REA II. Tulikaa na Mhandisi Msofe, mkandarasi na wawakilishi wa TANESCO tukaboresha hiyo orodha, Mheshimiwa Waziri naomba mtusaidie hiyo orodha iliyoboreshwa tupatiwe ili tuweze kuiwasilisha kwa wananchi wetu ambao wanasubiri umeme huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya mwaka huu ambayo inaendelea tuna shilingi bilioni 469, bajeti ya mwaka kesho ambayo tunataka kupitisha hapa tunapitisha shilingi bilioni 375, tunapunguza shilingi bilioni 94 kwenye bajeti ya Nishati. Mimi naomba Serikali isipunguze bajeti ya REA ibaki pale pale au iongezewe zaidi kwa sababu REA ndiyo mkombozi wa wananchi kwa maendeleo. Viwanda vitapatikana kama REA imefika vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine niende kwenye hotuba ukurasa namba 93 ambapo ameongelea kuhusu Single Receiving Terminal, naomba ni-declare interest mimi ni mdau, naelewa hili suala vizuri. Hotuba hii ni tofauti na uhalisia uliopo. Wiki mbili zilizopita, TPA waliita kikao ambacho wadau wote tuliitwa mara ya kwanza, tulikuwa tunasikia fununu kwamba suala hili linakuja lakini kiliitwa kikao wiki mbili zilizopita. Kwenye kikao hicho TIPER ndiyo walifanya presentation kwamba wao ndiyo wapo tayari kupokea mafuta ya Single Receiving Terminal, wakatoa changamoto zilizopo na maandalizi yanayofanyika, lakini kwenye hotuba Mheshimiwa Waziri amesema kwamba hiyo shughuli itafanywa na TPA (Tanzania Ports Authority). Sasa ningeomba ufafanuzi kwa Mheshimiwa Waziri kwa sababu hiyo ni tofauti na uhalisia uliopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ningependa kusema kwamba katika miaka hii miwili na nusu ya kazi ya Mheshimiwa Waziri nimeona ni Waziri mzuri sana lakini nguvu nyingi ameelekeza kwenye nishati ya umeme, kwenye mafuta amewaachia wasaidizi wamsaidie. Mimi ningeshauri Waziri akae na wadau ambao wanamchangia pesa kwa ajili ya kupeleka kwenye miradi ya REA. Ni muhimu kukaa na wadau, wadau wanaunga mkono hoja hii ya Single Receiving Terminal lakini wanasema kuna ukakasi kidogo jinsi mambo yanavyoenda huko kwani hayaendi sawasawa. Kwa hiyo, naomba na kushauri Waziri akae na wadau, awasikilize, asitume watu, suala hili ni zito sana ni suala la uchumi wa nchi, ni muhimu akae na wadau awasikilize, kuna mambo mengine labda haletewi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningeshauri hata Kamati ya Nishati na Madini ikae na wadau, iwasikilize. Wadau wako tayari kukaa na Kamati ili waeleze changamoto zilizopo na tunawezaje kutoka kwenye hizo changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo napenda kuliongelea kwenye suala hilo ni kwamba Mheshimiwa Waziri kasema tunaanza biashara hiyo ya Single Receiving Terminal kwa sababu tuna ubia na TIPER kwa asilimia 50. Mimi nakubaliana kwamba kuna ubia lakini ni vizuri sana kwa sababu kuna gharama ambazo zinahusika kwenye kutoa hiyo huduma, TIPER hawatoi huduma bure, kuna gharama kubwa sana ambazo zipo ambazo hajazitaja kwenye hotuba yake, mimi nitaziweka mezani hapa ili Waziri azielewe na awaulize hizo gharama kama zipo ni lazima zishindaniwe, lazima ieleweke wamefikia vipi hiyo gharama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mafuta yanayoingia ndani ya nchi leo asubuhi Mheshimiwa Waziri kasema kwa mwezi tunapokea karibu takriban milioni 450 ya mafuta. Kwa mwezi ukipokea milioni 450 ya mafuta kwa gharama waliyopanga kwenye kabrasha ya TIPER ambayo ninayo hapa wanasema watatoza dola 2.35 kwa siku 10. Kwa hiyo, haya mafuta yote yakipita kwa TIPER takriban utakuwa unalipa kwa mwezi bilioni mbili na milioni mia nane na lazima ulipe ili mafuta yapite pale na hiyo ni kwa siku 10. Mafuta hayo yakikaa zaidi ya siku 10, kuna mkataba ambao Serikali haijahusishwa ambao unaingiza sasa gharama inakuwa shilingi 30 kwa lita moja. Kwa hiyo, ukisema ndani ya milioni 450, kama nusu ya mafuta hayo yamebaki pale kwa siku 11 au 12, utakuwa unalipa karibu bilioni saba zingine kwa mwezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachoomba kwa Mheshimiwa Waziri, huyo mbia wake ni mfanyabiashara, anafanya biashara ya mafuta, ana-supply mafuta kwenye tender, sasa anapewa nafasi ya kusimamia mafuta katikati na kuingiza ndani ya nchi na kusambaza pia anapewa kazi hiyo yeye na huku chini pia tunashindana naye kwenye biashara. Mheshimwa Waziri, huyo mtu utashindana naye vipi kwenye biashara? Wengine wote sisi tutashindwa kufanya biashara hiyo kwa sababu huyo mtu mmoja ana-advantage ya kushinda kwenye tenda, anasimamia katikati pale na huku chini pia yumo, unampa undue advantage. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri ashirikishe hata Fair Competition Commission ili waangalie kama utaratibu huu unaendana na sheria zetu. Ningeshauri pia Attorney General atusaidie suala hili na aliangalie kwa undani zaidi. Mheshimiwa Waziri ana sifa nzuri sana kwa kazi anazofanya lakini hii inatukumbusha mwaka 2005 wakati nchi ilikuwa ina giza, Serikali ikaagiza kwamba tunataka tupate umeme kwa haraka sana, Wizara ya Nishati ikaenda, ikaleta kampuni ya mfukoni inaitwa Richmond, wakaingia mikataba mibovu, imetugharimu mpaka leo, tunarudi huko tulikotoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkataba huu haueleweki umepita vipi kwa sababu wakati wamefanya presentation tukasema tunaomba kujua makubaliano kati ya Serikali na TIPER, hakuna makubaliano. Tukaomba makubaliano kati ya TPA na TIPER, hakuna makubaliano. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, ningeomba hili suala aliangalie kwa ndani sana, nampenda sana na pia Serikali ya Awamu ya Tano haipendi kabisa ihusishwe na mambo ya ufisadi, rushwa na mambo ya hovyo hovyo. Kwa hiyo, ningeshauri Mheshimiwa Waziri, aliangalie hili suala kwa ndani, tusimharibie Rais wetu sifa zake nzuri ambazo anazo za kupambana na ufisadi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nalopenda kulisema hapa, kwenye hotuba Mheshimiwa Waziri amezungumzia ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta safi, kwenye ukurasa wa 87. Naomba ni-declare interest, mwaka 2014, Wizara ya Nishati na Madini mliletewa andiko, mwekezaji kampuni ya Kitanzania, Petroleum Logistics Tanzania Limited akasema atajenga bomba kutoka Dar es Salaam mpaka Zambia, gharama iliwekwa pale, akafanya presentation, Wizara ikamuita Katibu Mkuu kutoka Zambia akafika hapa, mwekezaji akafanya presentation mbele ya Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Maji ya Zambia na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati alikuwepo, wataalam walikuwepo na taasisi mbalimbali zilikuwepo. Wamechukua huo mradi, wameugeuza kuwa mradi wa Serikali, sasa wanasema Serikali inaanza mchakato wa kutengeneza mradi. Hiyo kampuni ya Kitanzania, haikuomba mkopo wa Serikali wala haikuomba guarantee yoyote ilisema itafanya kwa gharama zake. Naomba Mheshimiwa Waziri aliangalie hilo pia anasema anaanza mchakato wakati mchakato uko tayari kwenye ofisi zake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana.