Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Hawa Abdulrahiman Ghasia

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mtwara Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa fursa hii niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Fedha. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwigi wa rehema ambaye ameniwezesha afya njema na kuweza kusimama mbele ya Bunge lako tukufu kuweza kuichangia bajeti hii.

Mheshimiwa Spika, napenda nianze kwa kumpongeza Waziri wa Fedha na Naibu wake pamoja na taasisi zilizo chini yao. Pamoja na pongezi hizo ningependa kushauri katika maeneo yafuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, eneo la kwanza ni suala la Tume ya Mipango. Tume ya Mipango ipo kisheria na ni chombo pekee ambacho katika nchi mbalimbali ndio kimekuwa tegemeo la kuishauri Serikali katika mipango yake ya nchi. Na nchi nyingi zilizofanikiwa zimepitia chombo hiki ambacho aidha ni Tume ya Mipango au ni vyovyote wanavyoita, lakini ambacho kinahusika na masuala ya mipango na wengine wanaitwa think tank. Tume ya Mipango inapaswa kuwa chombo huru ambacho kinakuwa juu ya Mawaziri wote akiwemo na Waziri wa Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na ndio maana tuliwahi kuwa na Wizara ya Fedha na Wizara ya Mipango. Na pia tumewahi kuwa na Waziri wa Nchi ndani ya Ofisi ya Rais, anayeshughulikia Mipango; na ndio maana tukapata Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Taifa, ambao ulikuwa na lengo la kuondoa vikwazo vya maendeleo na tukawa na Mpango wa Pili ambao wenyewe unajielekeza katika Uchumi wa viwanda. Na tulikuwa na Mipango miradi ya kielelezo ambayo ilikuwa inasimamiwa na Tume ya Mpango. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia katika bajeti ya mwaka huu iliyotoka, hata lile jina miradi ya kielelezo limepotea, miradi ya kimkakati imetoweka kwa sababu Tume iliyokuwa inashughulikia masuala hayo haipo. Niombe Serikali yangu, chombo kile au tume ile irudi na ikiwezekana ili iwe huru iwe Tume ndani ya Ofisi ya Rais. Iwajibike moja kwa moja kwa Mheshimiwa Rais na iwe inatoa maelekezo kwa Wizara zote ikiwemo na Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia sasa hivi Wizara ya Fedha inaangalia zaidi kukusanya kuliko kuanzisha miradi au mipango ambayo itakuza uchumi na kuiwezesha Wizara ya Fedha kuweza kukusanya. Kwa sababu suala la mapato au revenue ni function ya price times quantity. Sasa badala ya kuongeza tu hiki kiwango cha tozo kwamba mwaka huu umetoza shilingi 10, mwakani shilingi 20, mwakani shilingi 30 ongeza uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuongeze viwanda viwe vya vinywaji, viwe vya saruji unaweza ukabaki na tozo yako ile ile lakini ukakusanya zaidi na ndio hapo ambapo tunaitaka Tume ya Mipango ili iweze kutushauri kama ni viwanda, ni viwanda vya aina gani ambavyo vitachangamisha uchumi wetu kwa haraka zaidi na hivyo kuiwezesha Serikali kuweza kupata makusanyo mengi zaidi na kwa haraka zaidi. Tukiendelea tu kupandisha kodi, kodi, kodi kila siku tunakula mitaji, tunaua biashara, makusanyo yanashuka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo nilipenda nichangie ni suala la ubia wa Serikali na sekta binafsi. Tumezungumzia madeni ya Serikali, madeni ya Serikali hakuna ubishi kwamba mpaka sasa hivi ni himilivu kwa vigezo vyote, lakini tunataka yaendelee kuwa himilivu kwa vipindi vyote. Kitu ambacho kitatusaidia deni letu liendelee kuwa himilivu ni kwa kuangalia miradi ile ambayo iko kimtizamo wa kibiashara, basi Serikali iingie ubia na sekta binafsi ili tupunguza kukopa. Tukiingia ubia na sekta binafsi kama Serikali tutachangia sehemu yetu lakini pia tutaweza kupitia ubia wetu kuongeza uzalishaji na pia kuongeza mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, tangu tulivyopitisha Sheria ya PPP mpaka sasa hivi ukiacha Mradi wa DART ambao miundombinu imejengwa na Serikali kwa asilimia 100 lakini tumeingia ubia kwenye uendeshaji. Hakuna mradi mwingine ambao unaonesha tayari Sheria ya PPP imefanikiwa.

Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri Wa Fedha tuharakishe mchakato, tunayo miradi mingi hata ukipitia kwenye hotuba mingi ambayo imeorodheshwa, lakini yote hiyo iko kwenye upembuzi yakinifu. Nimuombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha huo upembuzi yakinifu basi uharakishe ili ile miradi itekelezwe na hiyo ndio itakayotusaidia. Pesa ndogo tulizonazo zipelekwe kwenye sekta ya afya, zipelekwe kwenye elimu, zipelekwe kwenye miradi ile ambayo sekta binafsi wanaiona haivutii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo pia nilitaka nilichangie ni suala la michezo ya kubahatisha. Ukiangalia kwenye kitabu hiki cha Waziri wa Fedha mwaka huu kumekuwa na mafanikio makubwa sana yamepatikana mapato mengi sana kutokana na michezo ya kubahatisha, lakini mafanikio haya tulipata shida sana mwaka jana Bodi ya Michezo ya Kubahatisha kutukubalia kwanza kodi hii kukusanywa na TRA, lakini pia kuongeza tozo ambazo zilikuwa zinatozwa mpaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali alivyowauliza mimi mbona ninawashangaa kwamba Kamati inataka muongeze kutoza ninyi mnakataa ndipo walipokubali, lakini leo wote tunasherehekea mapato kwamba hii michezo ya kubahatisha imeongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado kwenye michezo ya kubahatisha Serikali inaweza ikakusanya pesa nyingi zaidi kuliko inavyokusanya sasa hivi, kuna makampuni zaidi ya 46 yanayojishirikisha katika hii michezo, lakini ukiziangalia makusanyo hayo yote yanatoka katika makampuni matatu tu, yapo makampuni yanayocheza michezo inayofanana lakini kila mtu anatozwa kiasi chake.

Katika baadhi ya maeneo watoto wetu wadogo wanaenda kwenye ku-bet huko kwenye vibanda lakini Serikali pale inapata shilingi 32 tu kwa mwezi tungependa iongezwe kiasi hiki. Waswahili wanasema ukitaka kula nguruwe basi mle aliyenona, si wengine hii ni kamari, lakini kwa vile Serikali imetaka iende basi kamari hiyo inufaishe zipatikane pesa za kutosha watu wapate maji, wapate barabara, wapate kingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna watu wanapata kwa mwezi zaidi shilingi bilioni tano wanatoa shilingi milioni 200 tu kwa Serikali. Tunaomba eneo hili bado Serikali ifanyie kazi tulishapeleka mapendekezo muda mrefu ya kuitaka Serikali iongeze kwa baadhi ya watu wanakuwa-charged asilimia
12; asilimia sita tukasema waongezewe lakini mpaka sasa hivi hatuoni kama Serikali ina nia ya kuongeza katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja.