Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Kwanza nianze na kumshukuru Mwenyezi Mungu vilevile nianze kutoa pole nyingi sana kwa wananchi wa Iringa kwa msiba mzito ambao tumepata kuondokewa na watoto wetu wapenzi Maria na Consolatha ni watoto ambao wametupa elimu kubwa sana na wametufundisha funzo kubwa sana, tunaomba Mwenyezi Mungu awapokee na awalaze mahali pema peponi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze na kumpongeza Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mpango vilevile nimpongeze Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Kijaji na ni wapongeze Wakurugenzi wote au watendaji wote wa taasisi za fedha kwa kazi nzuri wanazozifanya.

Nianze mchango wangu kwanza kuongelea kuhusu ucheleweshaji wa fedha katika Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli ucheleweshaji wa fedha katika halmashauri zetu za maendeleo umefanya miradi mingi sana kutokamilika kwa wakati hivyo ningeiomba Serikali ingejaribu kuangalia ile miradi ambayo ina tija pesa ingeletwa kwa wakati. Kwa mfano nikitoa tu mfano katika Halmashauri yangu Manispaa ya Iringa Mjini kuna mradi ambao ni wa machinjio wa Ngerewala huu mradi umeanza toka mwaka 2008 na huu mradi tulikuwa tunaimani kabisa kama ungeletewa fedha kwa wakati ungeweza kusaidia hata miradi mingine na ni chanzo kizuri sana cha mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile ungeweza ukatoa ajira kubwa sana katika Manispaa yetu hivyo ningeomba Serikali ingekuwa inajaribu kuangalia kufanya upembuzi yakinifu wa miradi ile ambayo unajua ina tija ambayo inaweza ikasaidia ikaweza kuletewa pesa nzuri zaidi huwa sielewi kama Serikali huwa inatumia vigezo gani kutenga hizi fedha katika hii miradi ya maendeleo. Sasa ni vizuri sana Serikali ingetenga fedha kukamilisha miradi kama hii ili tuweze kupata chanzo kikubwa cha Halmashauri zetu na vile tungeweza kukusanya pesa nyingi katika kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia ninaomba nizungumzie kuhusiana na madeni ya wazabuni. Kuna wazabuni wanaidai Serikali hii kwa mda mrefu sana toka mwaka 2012 wako wengi sana wanadai Serikali yetu. Nakumbuka Mheshimiwa Rais pia aliwahi kuagiza kwamba wazabuni wote walipwe pesa zao sasa sijajua kama walilipwa na utaratibu gani ulitumika kwasababu bado kuna malalamiko mengi sana kwa wazabuni kutolipwa pesa zao. Na kumbuka kwamba kuna wazabuni wengi sana walikuwa wamekopa benki na kuna wazabuni wengine wameuziwa mali zao kutokana na riba kubwa ambazo walikuwa wanadaiwa na benki. Kwa hiyo, ni vizuri labda Serikali ingealia na vilevile tunaona kwamba hawa wazabuni pia bado walikuwa wanatozwa na TRA kwamba wanahesabika kama wamefanya biashara na wakati bado hawajalipwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa labda kungekuwa na utaratibu mzuri wa kuangalia kudai hata hizi VAT ambazo wazabuni wanadai Serikali, wangeangalia hata sheria iwalinde kwa sababu bado wanakuwa wanadaiwa na Serikali, bado wao wanaidai Serikali sasa ningeomba labda uangalie utaratibu hata ile Sheria ya VAT. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie kuhusu sekta ya mazao ya misitu kama mbao, mirunda, nguzo ambazo kwa kweli ndio biashara kubwa ambayo inafanyika katika Mkoa wetu wa Iringa na hata Njombe na sehemu nyingine. Huu utaratibu wa kudai risiti za EFD wakati wa kusafirisha mazao haya kwenye maroli umekuwa ni kero kubwa sana kwa wafanyabiashara kumbuka mazao haya mkulima anakuwa anasafirisha anapeleka sokoni ndipo alipwe lakini sasa anapodaiwa hizi risiti hata wale wasafirishaji wale wa maroli wanakuwa wanakata kubeba mizigo yao. Kwa hiyo, inasababisha sasa mfanyabiashara wa roli hapati pesa hafanyi biashara, mfanyabiashara wa mbao hafanyi biashara hata kuna vijana wanasaidia kupakia hizi mbao hawapati pesa. Kwa hiyo, pengine ningomba sasa ingetafutwa utaratibu mzuri wakusanye hizi pesa za mazao ya mbao ambayo wafanyabiashara imekuwa ni kero kubwa sana katika Mkoa wetu wa Iringa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze sana Kamishna Mkuu wa TRA Mr. Kichele tumemuona katika vyombo vya habari anazunguka nchi nzima, anapita kwenye maduka, anakagua, sasa huwa najiuliza na anakuta kuna madudu mengi sana. Sasa hawa maafisa walio katika hii mikoa ina maana hawapiti kuona haya madudu ambayo Kamishna anayaona labda ni vizuri sasa na wao wakajaribu sasa kupita na kuangalia kuliko wamsubiri Kamshina Mkuu ndio anakuja kugundua madudu ambayo yapo.

Mheshimiwa Spika, pia nizungumzie kuhusiana na wafanyabiashara wadogo na kodi, ningeomba labda Serikali ingekuwa na utaratibu wa kila mwaka unapoanza TRA kupitia idara yao ya elimu kwa mlipa kodi wangekuwa kuna elimu wanawapatia na pia wawasilikilize kero au wasikilize hoja zao na lugha pia iwe rafiki kwa wafanyabiashara kwa sababu naona lugha sio nzuri sana maafisa wetu wa TRA wanapokwenda kukusanya hizo kodi wanatishiwa wanawekewa kodi ambazo siyo, kwa hiyo mfanyabiashara anakuwa anakata tamaa sana na biashara anapoanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia ningeomba Serikali kuwepo na utaratibu wa kuwasaidia hawa wafanyabiashara wadogo hata ikiwezekana wanapoanza hizi biashara basi angalau kodi wasianze na kodi kubwa kwa sababu unakuta wanatozwa kodi hata biashara hawajafanya. Lakini kungekuwa na utaratibu mzuri kama nchi za wenzetu, kwamba wanawasaidia wanaanza kuwapa pesa wanaanza kuwatoza kodi kidogo hata asilimia 10 halafu baadae inapanda kidogo kidogo watakuwa wanawajengea utaratibu mzuri kwanza wigo mpana wa kodi utaonekana kwa sababu wafanyabiashara wengi sana watasajili, watalipa kodi na vilevile itasaidia Serikali kukusanya kodi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nizungumzie kuhusu tariff ya East Africa Community. Tanzania na wenyewe wawe wepesi kubadilika kutokana na tozo ambazo zimekuwa zikibadilika badilika. Kwa sababu tunaona nchi nyingine kwa mfano Kenya au Uganda kuna tariff ambazo wanakuwa wanazitoa yaani kodi zile zinaondolewa tozo. Lakini unaona Tanzania kutotoa zile tozo mapema sasa hata biashara zinaondoka, watu badala ya kwenda kupitisha hata biashara kwenye bandari yetu unakuta wanapitisha kwenye bandari nyingine kwa sababu tayari tozo zinakuwa zimeondolewa pengine kwa sababu ni biashara ya East Africa basi kuwepo na utaratibu mzuri wenzetu wakiondoa na sisi tuondoe ili na sisi tuweze kupata biashara nzuri zaidi kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie kuhusu wafanyabiashara wanaodaiwa madeni na TRA kwa miaka ya nyuma. Kumekuwa na utaratibu sasa hivi wa maduka mengi sana yamefungwa hasa pale Iringa, kwamba kuna madeni wanadaiwa ya nyuma na utakuta pengine walikuwa wamekisiwa tofauti yaani hawakukisiwa inavyotakiwa. Sasa unaona miaka 10/miaka mitano bado mfanyabiashara yule anashindwa kulipa madeni, labda kungekuwepo na utaratibu kwamba badala ya kuwafungia maduka basi wawaachie wawe wawalipa kidogo kidogo kwa sababu wakifungia bado Serikali inakosa kodi. Lakini wakiwaachia wakalipa kidogo basi angalau inasaidia wao wanapata biashara zinaendelea na Serikali inaendelea kupata zile kodi.

Mheshimiwa Spika, tungefanya labda utaratibu kama tulivyofanya zile tozo za magari kwamba walizifuta zile za nyuma zote tukaanza upya pengine ipo haja kwa sababu utakuta hawa wafanyabiashara wengi wao walikadiriwa kodi ambayo haikuwa ya ukweli kwa hiyo bado wanaendelea kuteswa wanafunga maduka yao. Sasa Serikali iangalie na itoe uzito kwasababu maduka yote yakifungwa maana yake sawa sawa na ng’ombe sasa kama tukimchinja hatupati tena maziwa lakini kama ng’ombe wako ukimpa mashudu unaweza kuendelea kukamua vizuri zaidi. Kwa hiyo, tukiendelea kuwasaidia wafanyabiashara wetu wakafanya biashara zao vizuri, wakawapa elimu nzuri, tutaendelea kukusanya kodi nyingi zaidi na wafanyabiashara wengi sana watafungua biashara, kwa hiyo Serikali itaendelea kupata kodi kwa wingi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.