Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Pascal Yohana Haonga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbozi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba sasa nami niweze kuchangia Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na hoja ya kwanza ambayo wapo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wameigusia kidogo nami naomba nianze nayo hiyo, kuhusu hii bajeti ya mwaka 2018/2019 ambayo naona kwangu imepuuza sana maslahi ya watumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi wa umma katika Taifa hili tangu Serikali hii ya Awamu ya Tano imeingia madarakani bajeti zake zote, kuanzia bajeti ya mwaka 2015/2016 ambayo ilikuwa bajeti ya kwanza, bajeti ya 2016/ 2017, bajeti ya 2017/2018 ambayo ndiyo inaisha siku chache zijazo, imepuuza maslahi ya watumishi wa umma. Hakuna nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma. Mishahara ambayo watumishi wa umma wanapokea kwa mara ya mwisho iliongezwa mwaka 2014, ni mishahara ambayo Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliiacha hadi watumishi wa umma wanapokea mishahara hiyo, hapajawahi kuwa na nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunafahamu kwamba gharama za maisha zinazidi kupanda, zinazidi kuongezeka. Mwaka 2015 ukiuliza bei ya sukari ilikuwa shilingi ngapi ilikuwa bei ya chini Sh.2,000, lakini leo maeneo mengine hadi zaidi ya shilingi elfu tatu na kitu. Huku ni kuwakosea sana watumishi wa umma kwa sababu gharama za maisha zinaongezeka lakini mishahara yao ni ileile ambayo Awamu ya Nne iliiacha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti haijapunguza kodi kwa watumishi wa umma. Tulitegemea kwamba bajeti hii ingekuwa ni msaada kwa watumishi wa umma ingeweza kupunguza kodi, haijazungumza lolote lile, huku ni kuwapuuza watumishi wa umma. Ikumbukwe kwamba wakati wa kampeni viongozi mbalimbali walikuwa wanaomba kura na Viongozi wa Serikali hii ya Awamu ya Tano na wengine walikuwa wanapiga push up majukwaani wakiomba kura, leo watumishi wa umma wamepuuzwa, wamesahaulika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nasikia ilipokuwa siku ya Mei Mosi pale Iringa, Mheshimiwa Rais anasema hajawahi kuzungumzia popote pale kuhusu kuongeza mishahara kwa watumishi wa umma wakati mwaka jana Mei Mosi kule Moshi - Kilimanjaro alisema mwaka unaofuata kwa maana ya mwaka huu, angeweza kuongeza mishahara kwa watumishi wa umma lakini mwaka huu akiwa Mei Mosi amesema kwamba hakuwahi kuzungumza popote pale kuhusu kuongeza mishahara. Hii siyo sahihi, huku ni kuwapuuza watumishi wa umma...

T A A R I F A . . .

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki nibishane sana na Kiti chako, lakini ukweli unajulikana, Watanzania wanajua ukweli jinsi ulivyo au uko wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe Mosi Februari, 2016, watumishi waliandikiwa barua za kupandishwa vyeo au kupandishwa madaraja, tarehe Mosi Februari, 2016. Tarehe Mosi Novemba, 2017 barua hizi zikafutwa, yaani mwaka moja baadaye barua za watumishi kupandishwa madaraja au vyeo zikafutwa. Hili jambo ni kuwaumiza watumishi kweli, hili jambo halikubaliki hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtumishi ameandikiwa barua ya kupandishwa cheo au kupandishwa daraja, mwaka mmoja baadaye barua inaandikwa nyingine ya kufuta cheo chake. Mwaka huo 2016 kuna watumishi walistaafu na waliondoka na barua ambayo imeshaandikwa mwaka huo na tunajua kabisa kwamba pensheni ya mtumishi wa umma wanai-calculate kulingana na mshahara wake wa mwisho au daraja lake la mwisho, leo huyo mtumishi ameshastaafu yuko nyumbani inakuja kuandikwa barua nyuma kwamba tumeshafuta. Hii siyo sahihi kabisa na haikubaliki kabisa kuwafanyia Watanzania ambao ni wazalendo katika Taifa hili na wanaofanya kazi ngumu sana katika mazingira magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo watumishi ambao wamestaafu tangu mwaka 2015 hawajalipwa mafao yao hadi leo tunavyozungumza. Mwaka 2015 hawajalipwa pensheni yao, mwaka 2016 hawajalipwa, mwaka 2017 hawajalipwa, hii ni 2018 bado sioni kwenye bajeti hii kama kuna matumaini kwa watumishi hawa ambao wamelitumikia Taifa hili kwa uzalendo na kwa uadilifu wa hali ya juu sana. Namshauri Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mpango, Watumishi wa Umma ni vizuri wale waliostaafu walipwe sasa mafao yao, walipwe fedha zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu kilimo. Bajeti hii ni ndogo, lakini bajeti ya Wizara ya Kilimo imetengewa asilimia 0.52 ya bajeti yote. Tukumbuke Maputo Declaration na baadaye Malabo Declaration, viongozi wa Afrika wote walishauriwa kwamba angalau bajeti zao asilimia 10 iende kwenye bajeti ya kilimo, leo Bunge letu hili Serikali imekuja na 0.52 tunakwenda kwenye nchi ya viwanda ambayo naona haitawezekana kwa sababu bajeti ya kilimo imekuwa ni ndogo mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mazingira haya hata kufikia nchi ya uchumi wa kati na nchi ya viwanda naona ni ndoto za Alinacha, ni ndoto za mchana kweupe. Hatutaweza kufikia kwa sababu siku njema inaonekana tangu asubuhi. Kama tumetenga asilimia 0.52 maana yake viwanda itakuwa ni ndoto, tunazungumza tusiyoweza kuyatenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la masoko ya mazao, juzi nimesikia Serikali inasema sasa tumesharuhusu mazao yauzwe popote pale. Ukweli ni kwamba wananchi wetu wengi wanaolima mazao mbalimbali, kwa mfano wakulima wanaolima mahindi, Mkoa wa Songwe wananchi waliuza debe la mahindi mwaka mmoja na nusu Sh.20,000 kwa debe moja, leo wanauza Sh.3,500 na maeneo mengine na mikoa inayolima mahindi ni mingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipata soko la mahindi nchini Kenya, baada ya kufunga mipaka kuzia mahindi yasipelekwe nje, Kenya wakaenda kununua mahindi Zambia, wameenda kununua Uganda, wananchi wetu wakakosa masoko ya mahindi. Wamenunua pembejeo kwa bei kubwa sana, hali ni mbaya kwelikweli, Serikali lazima ioneshe commitment kwamba masoko ya mazao trip hii hawatazuia tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la Serikali ya Awamu hii ya Tano imetia fora kwa kuleta Bungeni bajeti isiyotekelezeka.