Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Amina Saleh Athuman Mollel

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru kwa kunipa nafasi nichangie bajeti ya Serikali kwa mwaka huu wa fedha 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naipongeza Serikali kwa kazi nzuri wanayoifanya na nampongeza Mheshimiwa Rais na Waziri mwenye dhamana. Vilevile nampongeza sana Spika wa Bunge pamoja na Katibu wa Bunge Bwana Kagaigai, kwa sababu wamekuwa ni mfano wa kuigwa kwa kuzingatia haki za msingi na kufuata Sheria za Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mwaka 2006 juu ya haki za watu wenye ulemavu. Nampongeza sana Mheshimiwa Spika na Katibu wa Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu, katika suala zima la elimu bure kwa watu wenye ulemavu limekuwa na faida kubwa sana. Nasema hivyo kwa sababu siku za nyuma katika suala zima la elimu katika jamii zetu, hasa wazazi walikuwa wanaangalia kwamba kipaumbele apewe nani. Kipaumbele hiki apewe mtu mwenye ulemavu. Kwa hiyo, kama kuna watoto wawili katika familia, mzazi yuko tayari kumpeleka mtoto asiye na ulemavu na mtoto mwenye ulemavu anaachwa nyumbani na wengi wao walikuwa wanafichwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba haki ya kupata elimu ni ya msingi na ni haki pia kwa watu wenye ulemavu. Katika Bajeti ya Serikali Mheshimiwa Waziri sijaona, bado sijaridhika hasa katika kundi hili la watu wenye ulemavu kuzungumzia ni kwa jinsi gani. Kwa maana hiyo naiomba tu Serikali na Mheshimiwa Rais, kwa sababu pamoja na kwamba jitihada nzuri na kazi nzuri imefanyika katika kuhakikisha kwamba elimu ni bure mpaka kidato cha nne, lakini bado naomba elimu kwa watu wenye ulemavu iwe ni bure kuanzia elimu ya msingi mpaka elimu ya chuo cha Kikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu gani nasema hivyo? Kama nilivyosema hapo awali, mtu mwenye ulemavu tegemeo lake kubwa liko katika elimu, hana namna nyingine yoyote ambayo inaweza kumwezesha huyu mtu akaweza kujitegemea mbali ya elimu. Kwa sababu ukimpa elimu umemkomboa na elimu hii ndiyo itakayomsaidia aweze kupata ajira. Vile vile bila ajira kwa mtu mwenye ulemavu na hasa hata wale ambao wamesoma, asipopata ajira bado inakuwa ni shida. Kwa hiyo, ile elimu aliyopata itamsaidia aweze kuona ni kwa jinsi gani anaweza akajiajiri kwa namna moja au nyingine. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali kuhakikisha kwamba inatoa elimu bure kwa watu wenye ulemavu kuanzia elimu ya msingi, sekondari na vilevile elimu ya chuo kikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mzuri tu, nawaombea mapumziko mema mapacha wawili ambao walifariki hivi karibuni, Maria na Consolata. Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika suala zima la mkopo, aliwapa watoto hawa ruzuku ambayo siyo mkopo, kwa sababu aliona umuhimu wa watoto hawa kwa jitihada zao mpaka wakafika elimu ya chuo cha kikuu. Kwa hiyo, akaona ni namna bora kabisa kuhakikisha kwamba anawapa ruzuku ili waweze kusoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mtu mwenye ulemavu mpaka anapofika chuo kikuu au anapobahatika kumaliza elimu ya sekondari akaenda kidato cha nne, cha tano na cha sita na baadaye kwenda chuo kikuu ni sawa na usemi wa Kiswahili unaosema: “Ukimwona nyani mzee, ujue amekwepa mishale mingi.” Kwa hiyo, changamoto wanayopata watoto wenye ulemavu na watu wenye ulemavu ni kubwa na ni mara mbili ya wenzetu wasio na ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sana Serikali kuona umuhimu wa kuwapa elimu bure watu wenye ulemavu kuanzia elimu ya awali mpaka chuo kikuu. Siyo hayo tu, tuone ni kwa jinsi gani tunawawezesha kwa kupata vifaa. Nafurahi sana Waziri mwenye dhamana ni mama, wanasema: “Uchungu wa mwana aujuae mzazi.” Tuone sasa ni kwa jinsi gani tunawezesha vifaa vipatikane katika shule zote. Pia hawa Walimu ambao wanasoma katika Vyuo, tuone ni kwa jinsi gani tutawawezesha wapate vifaa vya kuwasaidia pia katika kufundishia ili basi tutatue zile changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba sana na namwomba sana Mheshimiwa Rais aone ni kwa jinsi gani atalikomboa hili kundi la watu wenye ulemavu. Natambua jitihada zake, tumeona ni kwa jinsi gani katika Wizara mbalimbali wapo watu wenye ulemavu na hawajamwangusha. Hata katika Bunge lako, katika Baraza tumeona Mheshimiwa Ikupa anavyofanya kazi vizuri na hii imetuonesha kwamba watu wenye ulemavu ukiwapa nafasi wanaweza. Sasa usipowapa elimu itakuwa ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu. Naomba sana katika hilo ili basi tuweze kuwasaidia watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Ukurasa wa 15 wa Bajeti ya Mheshimiwa Waziri, ameeleza kuwa asilimia 10.4 ya Watanzania hawana ajira na vijana 800,000 wanaohitimu Elimu ya Chuo Kikuu ni vijana 40,000 tu wanaopata ajira. Kwa miaka mitatu ina maana kwamba tutazalisha watu 2,280 wasio na ajira. Kwa sababu kati ya hao 40,000 ukiondoa katika hiyo 800,000 wanabaki watu 760,000. Kwa hiyo, utaona ni kwa jinsi gani tatizo la ajira lilivyo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Waziri aliendelea kwa kusema kwamba Sekta ya Kilimo ambayo ni tegemeo, inaajiri asilimia 66 ya Watanzania. Pamoja na kwamba kuajiri asilimia hiyo bado inachangia pato lake kwa wastani wa asilimia 30, lakini pato hili linakua kwa kasi ndogo sana ya 3% mpaka 7%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa sababu hivi karibuni tumeona jitihada zake, ambapo amezindua mpango mkakati wa kilimo. Katika suala hili sasa tuone ni kwa jinsi gani kilimo chetu tunakifanya kuwa cha kisasa. Nchi ya Misri ambayo inategemea maji kutoka Mto Nile, wameweza kwa kiasi kikubwa sana kufanikiwa katika suala zima la kilimo. Siyo hao tu, ukienda nchi ya Israel mapinduzi ya kilimo ni makubwa sana na hata Mheshimiwa Mama Mbene siku akichangia bajeti hii alielezea pia nchi ya Vietnam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sasa nchini Tanzania mvua ni shida na hii ni kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, je, tunajipangaje kuhakikisha kwamba kilimo chetu, mbali ya kuajiri asilimia hiyo 66, lakini vijana hawa 800,000 ambao wanahitimu vyuo vikuu, tuone kwamba wale wanaobaki ni kwa jinsi gani wanaweza kujiajiri katika suala zima la kilimo. Vile vile katika kilimo tuone kuna mpango mkakati gani wa kuwawezesha vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa tumeona kwamba vijana wengi wameingia katika kilimo cha kisasa ambacho ni kilimo cha kibiashara kwa kulima hasa kwa kutumia hizi green house. Je, Serikali sasa inawawezesha vipi hawa vijana na hasa ukizingatia kwamba nchi ya Tanzania tuna maeneo makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika haya maeneo makubwa tunawawezesha vipi vijana ili waweze kujiajiri wao kwa kulima kilimo chenye tija ambacho kitaweza kuwasaidia wao na familia zao? Hili ni jukumu ambalo Serikali inapaswa kuhakikisha kwamba inajipanga na itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la ajira. Kwa sababu vijana tukianza kuwawezesha na kuwafundisha tangu chuo kikuu; na tumeshaona kwamba sasa hivi Mheshimiwa Rais ana dhamira ya dhati kabisa kuwakomboa vijana na hasa katika mapinduzi haya ya kilimo, sasa basi twende kuwawezesha vijana waingie katika hicho kilimo cha biashara ambacho kitawasaidia kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona baadhi ya vijana ambao wamefanya vizuri na wanasafirisha bidhaa za shambani ambazo wanalima mpaka nje ya nchi. Mmoja wa vijana hao ni Khadija Jabir ambaye amekuwa ni mfano wa kuigwa. Sasa tunawaandaaje vijana wengine, tuwapate kama akina Khadija Jabir ili nao waweze kujiingiza katika mapinduzi haya ya kilimo? Kwa sababu pia tunakwenda katika viwanda rasilimali nyingine hasa malighafi nyingine…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nimalizie kwa kusema kwamba napongeza pia kwa kuona umuhimu wa kufuta kodi katika baadhi ya vifaa ambavyo vinachanganywa katika vyakula vya kuku. Kuku hivi sasa ni tegemeo kubwa sana la wajasiriamali. Kwa hiyo, kwa kuondoa kodi hizi zitawasaidia sana wanawake ambao ndiyo wajasiriamali wakubwa na jamii yote kwa ujumla ili waweze kuwekeza katika ujasiriamali wa kufuga kuku. Siyo hilo tu, hili pia litawasaidia waweze kuendeleza na kuwasomesha watoto wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushuru sana na naunga hoja mkono.