Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia kidogo kuhusu hoja iliyo mbele yetu ya bajeti ya Serikali mwaka 2018/2019.
Mheshimiwa Naibu Spika, navyoelewa mimi ni kwamba hapa tunachojadili ni mipango yetu ya maendeleo tunaitafsiri kwa minajili ya pesa. Tunapanga bajeti, tunatoa pesa au sisi kama Bunge tunaidhinisha ili Serikali iweze kutekeleza ile mipango ambayo imeletwa hapa na imepitishwa na Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachonisikitisha ni kwamba Bunge hapa linakaa linapanga bajeti lakini Serikali hii iliyoko madarakani kusema ukweli haina nidhamu ya kusimamia matumizi jinsi bajeti ilivyopitishwa. Tunapitisha bajeti Serikali inakwenda kutumia pesa bila hata kulishirikisha Bunge. Si makosa Serikali kuomba bajeti au supplementary budget pale ambapo kumelazimika kuwa na matumizi ya lazima na hayakuwepo kwenye bajeti lakini Serikali haileti inatumia inavyoona kitu ambacho nakiona ni dharau kwa Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye uhalisia wa bajeti. Nchi yoyote inapanga bajeti kulingana na uwezo na makusanyo yake. Ukiangalia mwaka jana, tulipitisha bajeti zaidi ya shilingi trilioni 31 lakini haikutekelezeka kwa sababu makusanyo hayakuweza kutosheleza. Mwaka huu pia tunakwenda kwenye bajeti ya shilingi trilion 32, je, tuna uhakika wa kukusanya ili bajeti iweze kutekelezeka? Nachoshauri Serikali wala isione aibu, pale ambapo wanaona makusanyo hayatoshelezi na hayatapatikana leteni bajeti ambayo inalingana na uwezo wa nchi yetu ili tusifanye kwa kuonesha wananchi kwamba Serikali inaweza kukusanya mapato makubwa na hatuwezi kufanya jinsi wananchi wanavyotegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kuhusu Halmashauri. Wengi sana wamesema kuhusu D by D, lakini mara nyingi nikisimama huwa nairejesha Serikali hii katika kitu kilichotendeka mwaka 1972 – 1982, kile kilichokuwa kinaitwa madaraka mikoani, walikuwa wanasema decentralization, sijui kama ilikuwa D by D. Zoezi hili lilishindwa kwa sababu naona Serikali hii inapenda kuongoza nchi hii kwa trial and error. Tunajaribu tunashindwa halafu sijui tuna- retreat halafu tunaenda kuanza upya. Kwa hiyo, nchi inakaa katika kupanga na kupangua tu, ni kama tunafanya experiment kwamba tujaribu hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali sasa inarudi kwenye centralization kwa sababu inachukua pesa yote inaweka katika mfuko mmoja. Dhana ya kuanzisha halmashauri hizi ni ipi? Kama zilianzishwa kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi na kwa kuzingatia kwamba nchi hii ni kubwa, huwezi kuiendesha ukisimama Dar es Salaam peke yake, haiwezekani. Kama tulijaribu tukashindwa ni kwa nini sasa Serikali inataka kuturudisha kule. Hizi halmashauri kama Serikali iliyoko madarakani haizitaki leteni sheria hapa tubadilishe, tubaki na madaraka kule makao makuu ya Serikali halafu pesa zote ziwe zinatoka huko zinakuja kule chini, kitu ambacho hakitawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vyanzo vyote vya halmashauri, kama walivyosema wengine na wewe unavijua vimekwenda Serikali Kuu. Kitu ambacho kimenisikitisha ni hata ardhi, maana halmashauri nyingi zinategemea ardhi le ya wilaya lakini hata ile asilimia 30 ambayo ilikuwa inabaki au inapaswa irudishwe kule katika halmashauri kusaidia kwa sababu inatokana na ushuru au tozo mbalimbali ambazo zinatokana ardhi na yenyewe mmebeba mmepeleka Wizarani sijui Hazina na pesa hizi hazirudishwi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hebu tutazame ile Local Government Development Grant mpaka sasa hivi hakujatolewa hata senti tano. Kibaya zaidi hata kipindi hiki Serikali haijaweka bajeti ya pesa hizo kurudi katika halmashauri. Kama pesa hizo hazirudi miradi yote ambayo ilikuwa imepangwa kufanywa na halmashauri madarasa, zahanati, imekwama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali imeshindwa kurudisha hicho kidogo tu, je, ikiwa na mfuko mkubwa maana yake ni nini? Labda Serikali inachotaka kutuonesha ni kwamba imeweza kukusanya, siyo hivyo, la hasha, haijakusanya ni kwamba wamepora vyanzo vya halmashauri na halmashauri ziko mahututi na hatutegemei kwamba kweli wananchi wa Tanzania wataweza kupata huduma wanazostahili kama barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, mnaona barabara wanazotengeneza TARURA hata hapa Dodoma nendeni huku tunakokaa mitaani, wanatengeneza barabara ambazo hata ma-engineer hawafiki. Mmechukua ma-engineer wote wa halmashauri wameenda TARURA, halmashauri zimebaki hivi hivi zina wayawaya, ni kwamba hata barabara zinazotengenezwa hazipo. TARURA haiwezi kutengeneza barabara nzuri kwa sababu haipati pesa, watafanya grading tu lakini hawawezi kutengeneza barabara ambazo zitaweza kupitika ili wananchi waweze kusafirisha mazao yao. Hata huduma nyingine za afya, elimu hazitaweza kutekelezeka kama halmashauri hazipati pesa na Serikali Kuu inazikalia haipeleki pesa katika halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye kilimo. Ni jambo jema kwamba Serikali imeleta bajeti ambayo kipaumbele chake ni kilimo. Ila mimi ninajiuliza kipaumbele hiki mmeweka katika makaratasi, je, utekelezaji wake ukoje?
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi ambao tuna umri kidogo unawazidi walio wengi hapa, hebu turudi nyuma tuangalie ile Awamu ya Kwanza ya Hayati Mwalimu Nyerere aliwezaje kufanikiwa kutengeneza kilimo kikasaidia nchi yetu. Si vibaya na wala si dhambi kuangalia kule nyuma huyu bwana alifanyaje kwani makaratasi hayapo, mafaili hayapo, mipango haipo? Naiomba Serikali irudi nyuma ione ni kitu gani ambacho Awamu ile ilifanya (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza walikuwa na extension officers, sasa hivi kilimo kinasemwa lakini hakuna elimu inayotolewa kwa wakulima. Hata yale mashamba darasa mnayoyasema hayapo na kama yapo yametelekezwa. Sisi tunakaa vijijini huko, mimi nikienda nakaa kijiji sijawahi kumwona extension officer wa kata na hata hao waliopo hawana huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niko kwenye kamati ya LAAC kuna siku moja tumemwambia CAG hebu nenda kafanye performance auditing ya hawa ma-extension officers, kwa kweli wanapata mishahara ya bure, atuoneshe wanalipwa nini na wanafanya nini. Kama hawastahili kuwepo basi waondoke wakulima wajitegemee wenyewe wanavyoona yaani bora liende kila mkulima anafanya anavyoona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi nchi yetu ina vijiji zaidi ya 19,000, je, wako ma-extension officer kiasi gani ambao wanaweza kusaidia kuongoza wakulima? Mimi nakumbuka baba yangu alikuwa analima kahama na kwenye kilimo cha kahawa walikuwa wanakuja extension officers wiki mara mbili na pikipiki sasa hivi hawana hata usafiri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye kahawa. Niongezee kwa mchango wa Benardetha Mushashu jana …
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)