Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwimba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MANSOOR S. HIRAN: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu. Kwanza kabisa, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema ili niweze kusimama mbele yako.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kuwashukuru wananchi wa Kwimba kwa kunipa ushirikiano mzuri ili niweze kutimiza wajibu wangu wa kuwatumikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri wa Fedha, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara ya Fedha kwa bajeti nzuri sana ambayo wamependekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya kusema bajeti hii ni nzuri ni kwa sababu mimi kwa mara ya kwanza kwenye historia ya bajeti yetu nimekutana na bajeti ambayo haijapandisha kodi kwenye mafuta ya dizeli na petroli. Ni busara nzuri sana ambayo Mheshimiwa Waziri ametumia kuhakikisha kwamba mafuta hayapandi bei. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema hivyo kwa sababu unapotaka kupata uchumi wa viwanda unatakiwa uhakikishe nishati ya mafuta ni bei nafuu. Nampongeza kwa hilo na kama tukienda hivi Mheshimiwa Waziri nina uhakika uchumi wa viwanda ataweza kuufikia vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwenye historia ya nchi yetu kwa mara ya kwanza mwaka huu tumekutana na riba za benki kushushwa. Riba za kukopa zimeshuka, hiyo ni mara ya kwanza imetokea kwenye historia. Pia ameweza kupambana na inflation ambayo iko tarakimu moja, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri ambayo anafanya yeye na Wizara yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kwenye mchango wa bajeti iliyowasilishwa. Naomba nijielekeze kwenye hotuba ukurasa wa 46, paragraph ya kwanza. Naipongeza Wizara kwa kuleta mapendekezo ya kupunguza Corporate Tax kwenye viwanda vipya vya dawa za binadamu na ngozi. Nachoomba kwa Mheshimiwa Waziri asibague, viwanda vyote vinavyotengeneza dawa za binadamu na ngozi ambavyo vipo na ambavyo zitakuja vyote azipe incentive ya corporate tax asilimia 20. Atakapowabagua, wale wenye viwanda sasa hivi watashindwa kushindana na viwanda vipya ambavyo vitafika. Kwa hiyo, ni vizuri kuwe na Corporate Tax ambayo inafanana kwa wote. Pia nashauri Waziri asiishie kwenye dawa za binadamu, naomba pia viwanda vya dawa za mifugo na kilimo vihusishwe kwenye hili punguzo la Corporate Tax. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingine nayopenda kuelekeza mchango wangu ni kwenye ukurasa wa 51, paragraph 12 ambayo inazungumzia Ushuru wa Bidhaa kwenye sigara zisizo na kichungi. Naomba ni-declare interest kuwa mimi ni mdau. Nimesoma hotuba vizuri, amesema kwamba sigara ambazo zinatengenezwa kwa tumbaku inayozalishwa hapa Tanzania kwa asilimia 75 na zaidi ambazo hazitumii kichungi atazichaji Excise Duty ya Sh.12,447 na zile nyingine ambazo zinatumia kichungi atazichaji Sh.29,425.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sikuelewa sababu ya kuweka tofauti hiyo kwa sababu kwanza kabisa mtu anayevuta sigara ambayo haina kichungi anapata madhara makubwa zaidi kuliko yule anayevuta sigara ambayo ina kichungi. Kwa hiyo, mimi nashauri ingekuwa opposite; kwamba zile za Sh.12,000 angeziwekea Sh.29,000 ili watu wavute sigara ambayo ina kichungi kwa sababu ile ambayo haina kichungi maana yake anaivuta tumbaku moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo ukienda sokoni sigara ambayo ina kichungi au haina kichungi zote zinauzwa kwa Sh.100 mpaka Sh.150 kwa sigara moja. Ukichukua hizi sigara ambazo hazina kichungi zinazotozwa Sh.12,447, sigara hiyo inatakiwa iuzwe kwa Sh.60 mpaka Sh.65 kwenye soko, lakini sasa hivi inauzwa kwa Sh.100 kwa sababu sisi hatuna coins za Sh.20 na Sh.30. Kwa hiyo, alichotaka Waziri ni kupunguza bei ya sigara ili mwananchi wa kawaida apate faida ya kupata sigara ya bei nafuu, hiyo faida haipo, anayefaidika ni mwenye kiwanda, mwananchi analipa ileile Sh.100. Kwa hiyo, kuna karibu Sh.40 ambayo inapotea kama kodi kwa sababu ya kutokuchaji hiyo bei. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Waziri aende kuangalia suala hili kwa undani zaidi. Asilimia 70 ya Watanzania wanavuta sigara bila kichungi. Ni vizuri ku-discourage suala hilo na ku-encourage watu waende kwenye ile yenye kichungi ili angalau madhara yapungue.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingine ambayo napenda kupeleka mchango wangu ni ukurasa wa 52, paragraph 48 inayohusiana na stempu za kodi za kielektroniki. Mimi napongeza Wizara kwa maamuzi haya mazuri sana, naunga mkono maamuzi haya mia kwa mia. Shida yangu ni moja tu, ni gharama ya hiyo huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo gharama ya kununua stempu moja ya kuweka kwenye boksi la sigara unanunua kwa Sh.13. Naomba nirudie ili Mheshimiwa Waziri anisikie vizuri, leo gharama ya kununua stempu ya sigara kwenye boksi unalipa Sh.13, huyu SCIPA ambaye mmemteua kuwa ndiye atakayetoa huduma hii ataitoa kwa Sh.29.75, mara tatu ya bei ya sasa hivi ambayo tunalipa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi sielewi hiyo hesabu imefikaje mpaka mmekubaliana na hii Sh.29.75 wakati sasa hivi tunalipa Sh.13. Ningetegemea tungepata hiyo huduma kwa bei nafuu zaidi kwa sababu ni electronic tax stamps si tena karatasi, maana yake gharama zingepungua zaidi kuliko kupanda, ningetegemea ingekuwa Sh.10 au Sh.5. Kwa hiyo, ningependa hili suala mliangalie kwa undani zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwa hesabu ya haraka haraka, mwekezaji anawekeza shilingi bilioni 44, ana mkataba wa miaka mitano, kwenye taarifa ya Kamati ya Bajeti imesema kwamba kwa mwaka atakuwa anafanya biashara ya bilioni 66. Kwa hiyo, kwa miaka mitano mtu amewekeza bilioni 44 anachukua bilioni 330 kwa nchi yetu, kweli hesabu ya wapi ndugu zangu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri pia Ofisi ya Attorney General iangalie mkataba huu kwa sababu taarifa nilizonazo ni kwamba huu mkataba alishapata huyu bwana mwaka 2016 lakini ulikuwa na matatizo ndiyo maana ulikuwa umechelewa kutoka sasa hivi ndiyo umetoka. Kwa hiyo, naomba Serikali iangalie upya hili suala kwani ni zito.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabla sijamaliza nichukue nafasi hii pia kumpongeza Commissioner General wa TRA kwa kazi nzuri wanayofanya yeye na timu yake maana bila makusanyo tusingeongea mambo ya bajeti hapa. Kwa hiyo, naomba nichukue nafasi hii pia kuwapongeza TRA na Wizara ya Fedha kwa kazi nzuri ambazo wanafanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.