Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kasulu Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa namna ya pekee niunge mkono hoja hii na mapendekezo ya Waziri wa Fedha. Hata hivyo, naomba niwape hongera nyingi sana Waziri wa Fedha na timu yake kwa kazi nzuri wanayoifanya na hasa sera hizi za kodi za kuja na mkakati wa kulinda viwanda vya ndani na kuchochea uwekezaji katika Taifa letu, hilo ni jambo jema, hongereni sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba pia kuwapa hongera sana wenzetu wa TRA kwa kubadilisha mtazamo (attitudes), wameanza kuwa tax friendly kwa walipa kodi. Ni kitu chema sana na Ndugu Kichere na wenzake hongereni kwa kazi nzuri, songeni mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na hili la mfumo mpya wa stempu za kodi za kielektroniki. Kwanza ni jambo jema, kama alivyosema ndugu yangu yule wa Kwimba na Mheshimiwa Waziri nadhani cha msingi hapa hebu rudini kwenye meza tena muangalie hizo economics zake, haya yanayozungumzwa yana ukweli kiasi gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ni vyema Watanzania tusiogope mambo mapya. Mzee Dkt. Kikwete aliwahi kutueleza hapa kwamba ili ule lazima uliwe. Kwa hiyo, utaratibu huo wa stempu za kielectroniki uendelee lakini nimwombe tu Waziri wa Fedha na wenzake, warudi kwenye meza ya mazungumzo (drawing board) waangalie economics zake hizo. Hicho kinachosemwa kwamba watatupiga sana ni kitu cha kweli ili wajiridhishe na jambo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina ushauri katika suala hili la mifumo ya kutoza kodi. Wakati kampuni hiyo inafanya kazi hizi mngeifungamanisha na kampuni ya Kitanzania, hii Kampuni ya Maxicom Africa, hawa ni Watanzania, ni Waafrika wanaofanya kazi nzuri. Wamekubalika Uganda, Zambia, Rwanda na Kenya kwa washindani wetu wakubwa wa kibiashara. Kwa hiyo, ingekuwa jambo jema kwa miaka hii mitano muwafungamanishe na hii local company ili baadaye kazi hii iweze kufanywa na kampuni ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nitakuwa na machache tu. Jambo ambalo napenda niliseme ni nidhamu ya kibajeti. Pamoja na mambo mazuri haya ambayo yamekuja kwenye bajeti hii ambayo ameyaainisha na mengine akayazungumza hata kwenye hali ya uchumi, nizungumzie nidhamu ya utekelezaji wa bajeti, hili ni jambo kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 29 Mheshimiwa Waziri mwenyewe amebainisha kwamba kipaumbele kitakuwa ni ukamilishaji wa miradi inayoendelea. Sasa nimwombe sana miradi mipya isimame kwanza tukamilishe miradi ya kielelezo ambayo imekwama ili tuwe na
consistency.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini siyo hilo tu, kwenye hotuba pia ameainisha juu ya Waraka wa Hazina Na. 01 wa mwaka 2018/2019 ambapo anawaagiza Maafisa Masuuli wote watenge fedha za kutosha kwenye miradi inayoendelea. Narudia tena, miradi inayoendelea kabla ya kuanza mingine mipya. Sasa ipo miradi tunaijua ya kielelezo, miradi ya kipaumbele tangu bajeti ya mwaka jana, hiyo miradi haijakamilika. Moja ya miradi hiyo muhimu ni miradi hii ya barabara ya kuunganisha mkoa na mkoa mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi yetu mikoa ambayo haijaunganishwa kati ya mkoa mmoja na mwingine ni pamoja na Mkoa wa Kigoma. Mkoa wa Kigoma haujaunganishwa na Tabora, Katavi, Mwanza wala Shinyanga. Niombe sana kupitia Waraka Na. 01 aliouainisha Waziri kwenye hotuba yake katika ukurasa wa 29 basi miradi hii ambayo ina wakandarasi tayari kwenye maeneo mbalimbali ipewe kipaumbele na fedha ili ikamilike. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimkumbushe Mheshimiwa Waziri barabara muhimu sana katika nchi hii inayoitwa ya Kigoma – Kidahwe – Nyakanazi, hiyo ni barabara ya kielelezo imekaa miaka 20, bajeti zinakuja zinatoka barabara hii haijakamilika. Nimwombe Mheshimiwa Waziri naye aache legacy sasa kwamba barabara hii muhimu na kubwa katika nchi yetu inayotoka Kigoma - Nyakanazi haijakamilika. Nashauri Waziri akae na TANROADS na Katibu Mkuu wa Hazina, barabara hii ipewe fedha kwa sababu ni muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda nilizungumze ni umeme. Umeme ni muhimu sana kwa maendeleo ya viwanda na hata hizi juhudi zinazofanywa za kujenga Stiegler’s Gorge maana yake umeme huu utaingizwa kwenye Gridi ya Taifa. Mimi nataka nimkumbushe Waziri kuna mikoa iko off grid na inahitaji kuendelea kiviwanda na moja ya mikoa hiyo ni pamoja na Mikoa wa Kigoma na Katavi. Napenda sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja atueleze ule mkakati ambao Waziri wa Fedha mwenyewe alikwenda Korea kusaini pesa kwa ajili ya kitu kinachoitwa North West Grid, umeishia wapi? Kwa mradi ule Mikoa ya Geita, Kigoma, Katavi na Rukwa ingeunganishwa kwa Gridi ya Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya hayo, sisi ambao tuko off grid kuna Mradi mkubwa wa Kielelezo wa Malagarasi Hydro Power ambao una uwezo wa kuzalisha megawati 45. Naomba nimueleze Mheshimiwa Waziri wa Fedha, mradi huu ni muhimu sana na hii mikoa ambayo sisi tuko off grid lazima tupate treatment sawasawa kama mikoa ambayo ipo kwenye Gridi ya Taifa. Haiingii akilini mikoa ambayo ipo kwenye Gridi ya Taifa inanufaika na umeme mwingi wa kiviwanda lakini kuna mikoa ipo off grid. Bahati nzuri sana sisi Mkoa wa Kigoma tuna umeme wetu huu wa Malagarasi wa megawati 45.4, nina uhakika umeme huu utasaidia sana pia kuchochea maendeleo ya viwanda katika Mkoa wa Kigoma na maeneo ya jirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naomba nizungumzie uimarishaji wa ushirikiano na washirika wa maendeleo. Liko jambo ambalo ningependa Mheshimiwa Waziri atueleze, washirika wa maendeleo, Jumuiya ya Nchi za Ulaya, USAID na World Bank wana malalamiko makubwa na wamekuja kwenye Kamati zetu kutueleza kwamba Serikali mpaka tarehe 12 Juni kulikuwa na fedha shilingi bilioni 700 ambazo ni sawa na USD milioni 300, Serikali imeshindwa kusaini MoU. Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ni kitu gani hiki? Naomba aje atueleze tatizo liko wapi? Mfumo wa majadiliano ni wa kimkakati, kisera na kisiasa, zungumzeni na watu hawa tupate fedha hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naunga mkono hoja lakini Waziri aje atueleze juu ya jambo hili muhimu sana, ahsante sana.