Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika hoja iliyoletwa mezani kuhusu Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2018/ 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeeleza vipaumbele vitatu ikiwemo kilimo, viwanda, huduma za jamii kwa maana ya maji, elimu na afya. Mimi nitachangia katika suala la kilimo na elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya CCM toka tumepata uhuru wananchi hii imekuwa na kaulimbiu na mikakati mingi kuhusiana na sekta ya kilimo. Tulikuwa na kaulimbiu na mikakati mingi ikiwemo, Siasa ni Kilimo ya mwaka 1974, Azimio la Arusha la mwaka 1967, Azimio la Iringa mwaka 1974 lakini hata mwaka 2009 tulikuja na Kilimo Kwanza na Serikali ya Awamu ya Nne pia katika Big Results Now, sekta ya kilimo na yenyewe iliongezewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna ambaye anapinga umuhimu wa sekta ya kilimo kwa Watanzania. Nilipochangia Wizara ya Kilimo hapa nilieleza umuhimu wa sekta ya kilimo kwamba inaajiri nguvu kazi asilimia 65 ya Watanzania, inachangia asilimia 30 kwenye pato la Taifa, malighafi viwandani asilimia 65 inatoka sekta ya kilimo na asilimia 100 ya chakula hapa nchini inatoka kwenye sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika malengo ya MKUKUTA ya miaka 10, ilijiwekea mkakati wa ukuaji wa sekta ya kilimo angalau kwa asilimia 6 mpaka asilimia 8. Ukuaji wa sekta ya kilimo kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2011 mpaka 2015 umekua kwa asilimia 3.4 tu. Hata hivyo, toka Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, Serikali ya Hapa Kazi, Serikali ambayo inataka kutupeleka kwenye uchumi wa Kati, Serikali inayojiita ya viwanda, ukuaji wa sekta ya kilimo pamoja na umuhimu wake wote umeshuka ukilinganisha na Serikali ya Awamu ya Nne ilivyokuwa madarakani. Ukuaji wa sekta ya kilimo umekua kwa asilimia 1.9 tu toka mwaka 2016 mpaka 2017. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, bajeti ambazo tumekuwa tukizipitisha hapa Bungeni kwenye sekta ya kilimo imekuwa haifiki kwenye Wizara, hazitolewi kwa wakati. Mwaka 2016/2017 tulipitisha Bungeni hapa shilingi bilioni 100 zilizotolewa ni shilingi bilioni 2 tu fedha za maendeleo ni sawasawa na asilimia 2.2. Mwaka 2017/2018 sekta ya kilimo ilitengewa shilingi bilioni 150 zilizotolewa ni shilingi bilioni 16.5 sawasawa na asilimia 11 na mwaka huu fedha zilizoombwa kwenye sekta ya kilimo kwa maana ya Wizara ya Kilimo zitakazotekeleza miradi ya maendeleo ni shilingi bilioni 98.1. Tunawashangaa sana kila siku Serikali iliyoko madarakani, pamoja na kaulimbiu zenu na mikakati yenu mnayosema kwenye vitabu lakini sekta ya kilimo ambayo tunaitegemea sisi Watanzania tulio wengi, mmeendelea kutoipa kipaumbele na kutoona umuhimu wa sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukifanya uwiano kati ya bajeti kuu ya Serikali na sekta ya kilimo, mwaka 2016/2017 uwiano kati ya bajeti kuu na sekta ya kilimo kama ambavyo mmesaini Maazimio mbalimbali ya Kimataifa ni asilimia 0.93, mwaka 2017/2018 ni asilimia 0.85, mwaka 2018/2019 ni asilimia 0.52 na mwaka huu imeshuka zaidi ukilinganisha na miaka mingine. Sasa tunajiuliza mmesema mtaweka kipaumbele chenu cha kwanza ni sekta ya kilimo lakini sekta hiyo hiyo ya kilimo hamuipi fedha, mmewasahau Watanzania wakulima walio wengi, tutawaaminije? Mbona mmetudanganya miaka mingi sana? Mmekuwa wazuri kwenye maandishi, kwenye vitabu lakini kuja kwenye utekelezaji mmekuwa tofauti kabisa. Kwa kweli nirudie kusema, wakulima wa nchi hii adui yenu namba moja ni Serikai iliyopo madarakani kwa mikakati na sera mbovu ambazo hazitekelezeki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kutuambia kwamba kwenye bajeti hii kipaumbele ni kilimo lakini miaka iliyopita, mavuno ya mwaka juzi, wakulima mbaazi tu imewasumbua mpaka leo, kupata masoko ya wakulima wetu mbaazi ni mtihani, korosho ni mtihani, pamba ni mtihani yaani hakuna ambako afadhali, tumbaku ni mtihani, mahindi imewasumbua mwaka mzima yanawahangaisha mnakataza vibali, mnageuka kwa nyuma mnaruhusu vibali. Kahawa imewasumbua, pamba, mkonge, mazao mchanganyiko hakuna mkulima wa nchi anayelima zao lolote ambaye ana uhakika wa soko. Sasa mnasema kipaumbele ni kilimo mnawahakikishiaje Watanzania wakulima kuwa na uhakika wa masoko? Nini mkakati kwenye bajeti hii kuhakikisha wakulima wana masoko ya kutosha? Tunaomba majibu Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu sekta ya elimu. Serikali ya Awamu ya Tano mmesema mnatoa elimu bure na Serikali ya Awamu ya Nne iliona kutoa elimu bure ni changamoto, ikaona namna bora ni kusaidiana na wazazi kuhakikisha wanakabiliana na upungufu mbalimbali kwenye sekta ya elimu ikiwemo miundombinu na changamoto nyingi katika shule zetu za msingi na sekondari hapa nchini. Ninyi mmekuja, mmefuta michango, mnasema elimu ni bure, Mheshimiwa Waziri kwenye mambo yako 10 uliyoyataja hapa ya kumsifia Rais Magufuli umeelezea suala la elimu bure, nataka nikwambie elimu bure imekuwa na changamoto kubwa, mnaua sekta ya elimu kuliko hata Serikali ya Awamu ya Nne ilivyokuwa madarakani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe takwimu, upungufu wa walimu, shule za msingi, mwaka 2016 upungufu ulikuwa 191,772 mwaka 2017 upungufu umeongezeka umefika 179,291; shule za awali, upungufu wa walimu umekuwa 1,948; shule za sekondari masomo ya hisabati upungufu wa walimu ni 7,000, baiolojia 5,000, kemia 5,000, na fizikia 6,000. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu wa miundombinu; upungufu wa maktaba…

T A A R I F A . . .

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei hiyo taarifa na kitu ambacho nafikiri Serikali mnakosea sana, mnapima mafanikio ya elimu bora na idadi ya uandikishwaji siyo quality na hiki kitu mmekuwa mnakisema siku nyingi. Pia idadi ya wanafunzi wanaondikishwa inawezekana ikaongezeka kwa sababu ya uzao, birth rate nayo inawezekana ikawa inaongezeka, population inaongezeka, sasa mnapimaje hayo? Mheshimiwa Naibu Waziri utapata nafasi baadaye na wewe utasema ya kwako.
(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu wa maktaba; mwaka 2016 upungufu ulikuwa ni asilimia 88, mwaka 2017 upungufu umekuwa ni asilimia 91. Maana yake badala ya kwenda mbele kupunguza changamoto mbalimbali za kimiundombinu tunarudi nyuma hatua kadhaa haya matatizo yanazidi kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maabara; upungufu wa maabara ya baiolojia ni asilimia 51, fizikia 54 na kemia 53. Upungufu wa madawati ni milioni 1,170,000 na upungufu wa walimu ni 186,000. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajiuliza, mnatuambia elimu bure, elimu hii siyo bure, mnakwenda kuua Taifa la kesho. Badala tuliandae Taifa la kesho, mnajua umuhimu wa elimu ni kuandaa rasilimali watu, kuliandaa Taifa, tuwe na wataalam na wajuzi wa kutosha, tuandae mazingira ya kufikia haya, tunatengeneza mazingira mabovu ya kuwa na elimu mbovu ya kuiangamiza nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.