Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Mlimba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii adhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na kitabu hiki cha Waziri, ukurasa wa 11 anazungumzia wastani wa pato la Taifa la kila mtu, anasema kwamba wastani wa kila mtu kwa mwaka 2017 ni sawa na dola za Kimarekani 1,021 ukilinganishana na mwaka 2016 ni dola 958 kwa mwaka, kwa hiyo anasema umekua. Sasa swali langu, mlishawahi kupandisha mishahara? Hawa watumishi katika nchi hii wastani wao wa pato la Taifa umepanda au umesimama pale pale? Kwa hiyo, hapa kipato chako kinatudanganya? Hawa watumishi ambao hamuwapandishi mishahara pamoja na sisi Wabunge mnasema wastani kwa dola ya Kimarekani 1,021 badala ya dola 958 huo ni uwongo wa mchana kweupe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, watumishi wanapata wapi hela nyingine, wanakula rushwa mpaka mnawapima wastani wao wa kipato kwa mwaka? Tusidanganyane. Yaani ninyi wataalam wa kuandika hivi vitabu, mnaandika peke yenu halafu mnatuletea hapa, mnawadanganya Watanzania, wastani haujakua, hivyo ni vitabu tu lakini hali halisi sifuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naenda sasa kwenye bajeti kuhusu kilimo maana mimi ni mtoto wa mkulima na naishi kwa kutegemea kilimo. Bajeti ya mwaka 2016/2017, Bunge hili tuliidhinisha bajeti ya kilimo shilingi bilioni 100.5 lakini hela zilizotolewa kwenye kilimo ni shilingi bilioni 2.252 halafu unasema pato limekua, limekua kwa nani? Labda kwako wewe lakini kwa Watanzania wa kawaida na wananchi wa Mlimba halijakua chochote, bado wanarudi nyuma badala ya kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Kilimo mwaka 2017/2018, Bunge hili tuliidhinisha kwenye bajeti shilingi bilioni 150.25 na sifuri sifuri huko, lakini hadi kufikia Machi mwaka huu pesa zilizotoka za miradi ya maendeleo ni shilingi bilioni 16.5 sawasawa na asilimia 11 tu, leo unasema pato la Mtanzania limeongezeka, limeongezeka wapi wakati miradi ya kilimo ni shida?
Mheshimiwa Naibu Spika, kule kwetu na karibu Tanzania nzima hivi ninavyosema ni wakati wa mavuno, wananchi sasa wanavuma pumba kwa sababu mipunga panya waliingia, mahindi panya waliingia wakahangaika wakulima mpaka sasa wakati wa mavuno watu hawavuni tena, halafu tunaambiwa ikitokea njaa Mkuu wa Wilaya, sasa kama panya wamekula halafu kilimo hamjawapa hela za kutoa wale panya hivi unadhani watu hawataomba tena msaada? Mjiandae Wizara ya Fedha kuweka fungu maalum kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania ambao wamekosa kuvuna sasa hivi mazao yao yote yaliliwa na panya. Siyo kwamba wavivu wamelima lakini uwezo wa kuvuna tena haupo, hiyo ni hali mbaya, sijui watu wengine kama wamevuna lakini kwangu hali ni mbaya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hali hii imeendelea katika miradi yote, tumepiga kelele hapa Bunge zima, Serikali ilitenga shilingi bilioni 251 kwenye Miradi ya Maendeleo Vijijini, (Local Government Development Grants, kwenye mwaka huu tunaomaliza, Wakurugenzi wote Tanzania nzima na Wenyeviti wa Halmashauri wakapuliza magari mafuta wakaharibu bajeti zao wakaja Dodoma, wakaambiwa mnapewa hela, leteni miradi ya mikakati, mkishaweka tu mkirudi pesa zinaingia. Mpaka leo hakuna senti tano iliyoingia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkurugenzi wetu na Mwenyekiti wa Halmashauri alirudi Kilombero tukakaa vikao wakatumia pesa kwa ajili ya kuidhinisha miradi ya kimkakati, wananchi wamejenga madarasa, maabara, zahanati, mmesema mtaleta hela na mvua zitaingia ile miradi itakwenda kubomoka, nguvu za wananchi zitakwenda bure, halafu leo mnasema bajeti iko sawasawa, sawasawa gani ninyi? Acheni mambo yenu bajeti hewa hizo. Kwani tunaposema bajeti hewa ni zipi? Si ndiyo hizo za kudanganyana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa leo mnatuambia tupitishe tena bajeti, haya hii bajeti tunayoipitisha mtaitekelezaje wakati hii bajeti ya mwaka huu tunaoenda kuumaliza mwezi huu hakuna kitu, hewa. Mnaharibu karatasi tu hapa hamna lolote, bora mngesema tu kwamba, hatuna hela, eti ninyi mnasema mna hela pato la Taifa limekua kwa asilimia 7.1 limekuakua vipi, mmekusanya wapi? Nini mmekusanya mpaka leo? Cash budget, mmekusanyaje hiyo bajeti, mnaishia kulipa madeni lakini kibaya zaidi mnaenda kukopa kwa biashara, halafu mnalipa madeni, nyie vipi? Nyie mnadhani hatujui siri zenu mnazofanya? Mnajikazakaza tu, mnatumbua watu kila kukicha hamtaki kusema ukweli Watanzania huku wanaumia, watu hawalipwi mishahara yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona wenzetu wa Uganda walimu tu hawakupandishwa mishahara wametangaza mgomo, hapa Tanzania, yaani sijui tumelogwa na nani? Ni haki kabisa ya kila mfanyakazi kupandishwa mshahara lakini mpaka leo hata senti tano, mnavunja sheria, kwa nini mnavunja sheria? Kama ninyi kweli mnakusanya pesa na mna pesa kwa nini mnashindwa kupandisha mishahara ya watu kwa mujibu wa sheria? Leo mnajitamba hapa tuna pesa, pesa ziko wapi? Pesa hamna, mkiambiwa ooh, mnakopa kopa tu. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wapandisheni wafanyakazi mishahara yao kwa mujibu wa sheria zilizowekwa. Hii Serikali ya Awamu ya Tano ni hatari kuliko Serikali zote zilizopita, nawaambia. Halafu leo vitabu unasema uchumi umekua, umekua kwa nani, labda umekua kwa ninyi mnaoshikashika hela huko Benki Kuu. Hela siyo zenu ni zetu halafu mnakuja hapa mnatudanganyadanganya. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii tulipofikia hali ni hatari hata wewe unajua, Waziri anajua kila mmoja anajua, lakini kwa vile mnailinda Serikali ndiyo mnasema haya hamtaki tu kusema hali mbaya. Kama hali nzuri lipeni mishahara kwa Watanzania wanaolitumikia Taifa hili, kutwa mnatumbuatumbua. Kama pato la Mtanzania limekua, wale wafanyakazi waliotumbuliwa mpaka leo hawajui hatma yao pato lao limekua au limeondoka? Watanzania gani wanaowazungumzia? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata ukiwa na kiwanja wakati wa JK utauza shilingi milioni 5 sasa hivi mpaka milioni 1 hupati mnunuzi. Ninyi nini ninyi! Eti pato limekua limekulia wapi wakati watanzania wako hoi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kitabu chake amezungumzia Tume ya Taifa ya Uchaguzi waliidhinishia hela kidogo wakafika mpaka asilimia 300, acheni ubabaishaji, kwa nini kutumia hela nyingi za uchaguzi? Kwa sababu kazi yenu Awamu ya Tano kununua Madiwani na Wabunge halafu mnaenda mnafanya uchaguzi matokeo yake Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeenda kutumia mpaka asilimia 300, acheni hizo. (Makofi)
K U H U S U U T A R A T I B U . . .
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie muda wangu kama alivyosema ndugu yangu hapa Mheshimiwa Nsanzugwanko pamoja na mipango yenu basi muangalie na sera ya nchi hii kuunganisha mikoa. Mimi natokea Mkoa wa Morogoro, kuna Mkoa wa Njombe unaunganika kwenye barabara Jimbo la Mlimba lakini tangu nilivyoanza kusema mpaka leo, okay, wamefanya upembuzi kiasi mpaka Mlimba lakini kutoka Mlimba mpaka Madeke Njombe hakuna upembuzi, hakuna kinachoendelea. Kwenye vitabu vyao vya Serikali sioni hata mafungu yanayotengwa kujenga barabara angalau waanze kidogo ili Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Njombe kupitia Mlimba ile barabara iunganishwe. Ndio maana wakati mwingine tunachangia hapa tunaona uchumi haujakuwa kwa sababu wananchi wa maeneo yale bado wanateseka na sera hazitekelezwi.