Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye hoja iliyo mbele yetu. Naanza kwa kumpa pongezi Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote Wakuu kwa kuandaa bajeti nzuri. Kwa kweli, bajeti hii ni nzuri, nasema ni nzuri kwa sababu bajeti hii imewalenga watu wa kawaida na ukiangalia mipango iliyopo unaona kabisa kwamba, bajeti yetu hii inawalenga watu wa kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiangalia bajeti hii imelenga kupunguza matumizi na gharama za maisha, lakini imelenga kuhusianisha ukuaji wa uchumi pamoja na maendeleo ya mtu mmoja mmoja. Bajeti hii imelenga kuendeleza viwanda na wakishaendeleza viwanda ina maana kwamba, wakulima watatoa hizo malighafi, watapata mahali pa kuuza bidhaa zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasema bajeti hii ni nzuri kwa sababu unakuta kwamba, inalinda viwanda vyetu vya ndani. Sasa hivi tunasema tuko katika era ya kukuza viwanda katika Tanzania kwa hiyo, lazima tuvilinde viwanda vyetu vya ndani, ndiyo maana nimefurahishwa niliupoona kwamba, katika bajeti hii wanaondoa kodi ya ongezeko la thamani kwenye vifungashio vya dawa za binadamu, kwa hiyo mtu wa kawaida atapata dawa kwa bei nafuu. Vilevile virutubisho vya vyakula vya mifugo, kama vyakula vya kuku vinaondolewa VAT kwa hiyo, vitazalishwa kwa bei nafuu, mkulima atafuga na kuweza kupata faida kwa sababu gharama za uzalishaji zitakuwa ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile bidhaa zinazozalishwa humu nchini kama juice, bia, maji, mvinyo, vinywaji baridi, ushuru haukupanda kwa hiyo, gharama za uzalishaji zitakuwa ndogo, therefore wataweza kuzalisha kwa faida. Mheshimiwa Mpango hongera sana pamoja na Naibu Waziri kwa kutuletea bajeti nzuri ambyo inalenga watu wa kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata ukiangalia kwenye Ibara ya 43 kwenye bajeti hii ambayo inazungumzia vipaumbele, kipaumbele cha kwanza kilichozungumzwa ni kilimo, kilimo ndiyo sekta ambayo inaajiri Watanzania walio wengi. Hongereni sana ni bajeti ya watu ni bajeti ambayo inawalenga Watanzania wa kawaida.
Mheshimiwa Spika, watoto wa kike wanashindwa kwenda shule kati ya siku mbili mpaka nne kila mwezi kwa sababu ya maumbile. Kwa kipindi kirefu sana Wabunge Wanawake mnatuona huwa tunakwenda pale Pius Msekwa kwenye Ukumbi tunafanya mikutano mbalimbali, baadaye tukawaomba na wanaume wakatuunga mkono, tunapanga mipango, tukaunda Kamati mbalimbali zikaenda kuongea na Serikali, hatimaye Serikali ya Chama cha Mapinduzi imekubali ikaliona hili na kuondoa kodi ya VAT kwenye taulo za kike ili kusudi watoto wa kike waweze kuzipata kwa bei nafuu na wakishazipata kwa bei nafuu ina maana sasa hata wataweza kwenda shule kila siku kwa sababu wataweza kujisitiri, nawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali kwa kupanga kuleta mabadiliko ya Sheria ya Serikali za Mitaa ambayo inasema sasa asilimia 10 zitengwe, kwa ajili ya asilimia tano kwa wanawake na vijana asilimia tano. Pamoja na kwamba, viongozi mbalimbali hasa Mawaziri walikuwa wanakaa hapa wanatuambia hizo asilimia zitengwe, lakini Halmashauri nyingi walikuwa wanakwepa, hawatengi asilimia 10, wakitenga ni asilimia mbili au tatu. Sasa sheria ikishakuja itawabana itabidi wazitenge hizo asilimia.
Mheshimiwa Spika, nataka kuwaambia mimi najishughulisha sana na vikundi vya vijana na vikundi vya wanawake kwa kweli, hizi hela zinasaidia. Hizi hela zikienda kwenye vikundi vya vijana wataweza kufanya shughuli zao, watakuwa wamejiajiri, akinamama watafanya biashara zao, watafanya ujasiriamali, wataweza kulisha hizo familia.
Mheshimiwa Spika, leo hii naleta kero kubwa ya wakulima wa Mkoa wa Kagera na kero yenyewe ni bei ndogo sana ya kahawa. Unakuta mtu analima kahawa, anautunza mbuni kwa miaka miwili mpaka minne katika miaka hiyo analima, anapalilia, anaweka mbolea, anaweka viua- wadudu, lakini anakuja kuuza kilo moja ya kahawa kwa Sh.1,000. Hii ni bei ndogo sana, pamoja na kwamba Serikali ilitangaza kati ya tozo zile 26 zilizokuwa kwenye mazao mbalimbali zilipunguzwa, lakini bei ya kahawa haikupanda.
Mheshimiwa Spika, hata leo hii msimu wa kahawa umefunguliwa, lakini bei bado ni ndogo. Ni ndogo kwa sababu, hadi leo mtu akiuza kahawa kilo moja unakuta kuna ushuru wa Halmashauri ya Mji Sh.84, kuna ushuru wa Chama cha Msingi Sh.200, kuna ushuru wa Chama Kikuu, kuna ushuru wa sijui uboreshaji, usafirishaji, ukaushaji shilingi Sh.330, kuna gharama za mikopo, yaani wao wanakopa, riba wanaiweka kwenye kila kilo ya kahawa inayouzwa Sh. 367 na gharama nyingine zinakuja mpaka Sh.1,600.
Mheshimiwa Spika, unakuta mtu labda kahawa kwenye World Market imeuzwa kwenye Sh.3,000, lakini Sh.1,600 zote zinakatwa, lakini na mwenyewe akienda kuuza anapewa malipo ya awali labda kama Sh.1,000/=, wanasema wakishauza kule watakuja kumpa malipo ya pili na malipo ya pili na yenyewe huwa hawapati.
Mheshimiwa Spika, nimeangalia kwenye kitabu kinachozungumzia hali ya uchumi hapa naona kwamba, uzalishaji wa kahawa umepungua kwa 20.7% wakati uzalishaji wa korosho umepanda kwa 70.7%. Hakuna muujiza hapa, muujiza ni bei, bei ya kahawa ikipanda watu wenyewe watalima, watakata ile mibuni ya zamani, watalima mipya. Tunaomba vituo vya utafiti kama TACRI wapewe fedha watengeneze miche bora, wasambaze kwa wakulima walime kwa tija waweze kuuza mazao kwa bei zinazoeleweka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimeshangaa kwenye hiki kitabu cha hali ya uchumi wanazungumza kwamba, kwa mwaka 2017 kahawa ya robusta na arabika iliweza kuuzwa kati ya Sh.4,200 mpaka Sh.5,900 sasa inakuwaje mkulima anapata Sh.1,000 jamani? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu ndiye jembe letu na ndiye tegemeo letu. Tunaona amefanya kazi nzuri sana kwenye mazao mengine kama korosho, tumbaku na pamba. Wote hapa Wabunge wanaotoka kwenye mikoa inayolima kahawa tunaomba na kwetu aje atusaidie, bei ya kahawa ipande ili kusudi watu wa kwetu waweze kuondokana na umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali kwa kazi nzuri sana waliyoifanya kwa kujenga upya shule ya Ihungo na Nyakato Secondary School ukaifanyia ukarabati wa kina baada ya kuwa shule hizi zimeharibiwa sana kwa tetemeko. Sasa hivi shule zimekamilika lakini hakuna samani, kwa sababu baada ya tetemeko wanafunzi walisambazwa kwenye shule mbalimbali katika Mkoa. Sasa zile samani walihama nazo na katika hamisha hamisha samani zikaharibika.
Mheshimiwa Spika, watoto wanapaswa kuingia form five mwezi wa Julai/Agosti, lakini hakuna samani. Mkoa umeshaleta mahitaji ya samani katika Wizara zinazohusika, tunaomba samani zipelekwe ili kusudi hizi shule ziwe tayari kuwapokea, hata itapunguza ile backload niliyosikia asubuhi wanasema kwamba, watoto 20,000 wamekosa kwenda form five kwa sababu, hakuna miundombinu. Pale miundombinu ipo, kinachohitajika ni samani.
Mheshimiwa Spika, Madiwani ni watu wa muhimu sana. Madiwani ni viongozi wenzetu ambao ndiyo wako karibu na wananchi. Wale kila siku wanazunguka kwenye Kata, wanapanga mambo ya maendeleo, wanaibua miradi, wanachangia maendeleo, wao wanatoa huduma za jamii, wao magari yao na pikipiki zao ndiyo zinasomba.
Mheshimiwa Spika, tunaomba kwa sababu ya hali ya maisha, posho ya Madiwani ipandishwe au ikiwezekana walipwe mishahara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namalizia kwa kusema hii bajeti ni nzuri, inawalenga Watanzania walio wengi na hasa Watanzania wenye kipato cha kawaida.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.