Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Temeke
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru kwa kunipa fursa niweze kuchangia machache katika bajeti hii. Kwanza, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya, nimeweza kumaliza Mfungo wa Ramadhani mimi na wapiga kura wangu wa Temeke na leo tunahitimisha siku za ziada sita katika kuukamilisha ule Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hoja iliyokuwa mbele yetu, nina mambo matatu tu ya kuyagusia endapo muda utanitosha. Kwanza, nitapenda kugusia pato la kila Mtanzania, mfumuko wa bei na mwisho nitamalizia na hujuma ya Serikali dhidi ya zao la korosho kule Mikoa ya Lindi na Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla Mheshimiwa Waziri hajawasilisha hotuba ya bajeti yake, alitangulia kutoa Taarifa ya Hali ya Uchumi hapa nchini. Katika kuizungumzia hali ya uchumi hapa nchini yako mambo ambayo yameandikwa kwenye kitabu hiki ukiyasoma kama Mtanzania kwa kweli hayaeleweki. Nadhani Mheshimiwa Waziri alikuwa analenga kuwafurahisha pengine Wazungu, World Bank au IMF ili Serikali iendelee kupata sifa za kukopa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, anasema Serikali ya Awamu ya Tano imejitahidi kupandisha pato la Mtanzania mmoja mmoja kutoka Sh.2,086,000 mpaka Sh.2,275,000. Maana yake Mtanzania mmoja sasa pato lake limepanda kutoka Sh.5,700 kwa siku mpaka Sh.6,300 kwa siku. Nikajiuliza hii ni sifa au ni kejeli? Kwa sababu kipimo cha pato la Mtanzania ni kumwezesha kupata milo mitatu. Sasa kama tunajisifu kwamba tumemuwezesha Mtanzania kupata Sh.6,300 kwa siku, hiyo itakuwa ni kejeli, haiwezi kuwa sifa, kwa sababu Sh.6,300 huwezi kupata angalau mlo mmoja uliotimilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikajaribu kuingia sokoni, nikanunua tembele la Sh.1,000 kwa maana ya mafungu mawili, nikanunua unga nusu kilo Sh.1,200, nikanunua mkaa kipimo kidogo Sh.3,000, nikachanganya na pilipili, nyanya na kitunguu Sh.6,300 imekwisha sijapata mafuta ya kula na chumvi nikaombe kwa jirani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunaleta bajeti ambayo ni ya kumwezesha Mtanzania kupata ugali na tembele la kuchemsha ndiyo uwe mlo wake mmoja wa siku nzima, nikagundua kwa nini Mheshimiwa Waziri pia alisema, akiwadhihaki tena kwamba umri wa Watanzania average ya kuishi ni miaka 64, it is obvious. Kama mlo wako wenyewe ni mmoja wa ugali na tembele la kuchemsha, utawezaje kuishi zaidi ya miaka 50? Hapo hujaumwa, yaani uombee usiumwe na hiyo familia iwe ni wewe ni mkeo au mke na mume ndiyo mtapata huo mlo mmoja wa ugali na tembele la kuchemsha.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni dharau kwa Watanzania na ndiyo maana Serikali ya Chama cha Mapinduzi mnapenda sana sifa, mkisimama majukwaani muda wote mnajisifu, tumenunua Bombardier, tunajenga standard gauge, stiegler’s gorge, hata siku moja hamjawahi kusema kwamba mmemwezesha Mtanzania sasa anaweza kupata mlo mmoja wa ugali na tembele la kuchemsha ni kwa sababu mnatambua hii siyo sifa, ni kejeli lakini kwenye kitabu hiki mmeiandika. Ndiyo maana nikasema, kitabu hiki pengine kilikusudia watu wengine nje ya nchi hii lakini siyo kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pato linakwenda sambamba sana na mfumuko wa bei. Mtanzania leo hata ukimwezesha apate Sh.20,000 kwa siku, kama haitoshi kumwezesha kupata milo mitatu, ni sawasawa na bure. Kwenye Taarifa ya Hali ya Uchumi Mheshimiwa Waziri anasema, Serikali ya Awamu ya Tano imeweza kupunguza mfumuko wa bei. Nikajiuliza, ni bei za vitu gani ambazo Serikali imedhibiti? Ni bei ya chumvi, biscuit au ya Big G?
T A A R I F A . . .
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa yake kwa sababu anakiri kwamba kweli kwenye huo huo wastani, Watanzania hawapati milo mitatu, mpaka tusubiri mwaka 2025 tutapata milo mitatu. Kwa hiyo, yupo sahihi, ananiunga mkono kwa hiki nachokisema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nikasema pato la mtu mmoja mmoja kama halimwezeshi kupata milo mitatu kwa kesi yetu hapa Tanzania, hata kama atakuwa anapata Sh.20,000 haiwezi kumsaidia. Ndiyo maana nikasema huo mfumuko wa bei wanaosema wanau-control ni upi? Kwa sababu kama mfumuko wa bei ungekuwa controlled vizuri, Mtanzania hata angepata Sh.2,000 kwa siku, angeweza kumudu milo mitatu. Sisi kesi yetu ni milo mitatu tu hapa, wala siyo kiasi gani kinaingia mfukoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, wamesema wamepunguza mfumuko wa bei mwaka 2017, Serikali ya Awamu ya Tano wakati inaingia madarakani bei ya kilo moja ya sukari ilikuwa Sh.1,200, mwaka 2017 bei ya sukari ika-shoot kutoka kilo Sh.1,200 mpaka Sh.2,500/=. Wakalieleza Bunge hili na Taifa hili kwamba hiyo ni hujuma ya wafanyabiashara wameficha sukari kwenye godown na kwamba wataitafuta kwa gharama yoyote ili bei ya sukari irudi kwenye bei yake ya kawaida. Leo ni mwaka 2018 hawajarudi kutuambia walipata sukari kiasi gani kwenye godown na wameipeleka wapi? Cha ajabu zaidi, bei sasa imekwenda mbali zaidi, kilo ya sukari leo ni zaidi ya Sh.3,000. Sasa unajiuliza, bei ambayo wanai-control ni ya vitu gani, mbona hatuioni? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi tu hapa ikatoea tena crisis ya mafuta ya kula na Mheshimiwa Waziri Mkuu akaahidi hapa ametoa siku tatu. Utakumbuka maelezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu yalikuja baada ya Waziri wa Viwanda na Biashara kutoa tamko hapa Bungeni kwamba malighafi ya mafuta iliyopo nchini haiwezi kusababisha bei ya mafuta ipande, hata kama ile meli itachelewa kupakua mafuta. Ndiyo maana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kupitia maelezo hayo akasema hapa, natoa siku tatu, mafuta yaliyofichwa yatoke. Mpaka leo bei ya mafuta ipo juu, haijashuka na hatujapewa taarifa yoyote. Tukisema tuna- control mfumuko wa bei, ni bei za vitu vipi? Hivi vitu ndiyo vinagusa maisha ya Mtanzania ya kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge lililopita hapa lilipandisha bei ya mafuta ya taa kwa sababu ya kukomesha uchakachuaji. Walisema kabisa kwamba wanafanya hivyo kama temporary solution ya ku-control uchakachuaji wa mafuta, kwa hiyo, bei ya mafuta ya mafuta ya taa ifanane na bei ya diesel. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, EWURA sasa hivi inatumia mbinu za kisasa na teknolojia za kisasa, lakini bado eti tunaacha bei ya mafuta ya taa iwe sawa na ya diesel kwa ajili ya ku-control uchakachuaji. Kwa nini tumtese Mtanzania asiyekuwa na gari kwa sababu ya kulinda maslahi ya wenye magari? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kengele ya kwanza. Naomba dakika tatu basi nimalizie hujuma ya Kusini.