Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kigoma Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nami nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake kwa kuwasilisha bajeti yenye matumaini kwa Watanzania. Hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri kwa sababu mimi niko kwenye Kamati ya Bajeti kwa kusikiliza Wajumbe wa Kamati na kuweza kufanyia marekebisho mambo mbalimbali. Hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na ukurasa wa mapendekezo ya bajeti, ukurasa wa 29 unaosema kwamba, kutoa kipaumbele kwa ukamilishaji wa miradi iliyoanzishwa na wananchi. Nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, tulikuwa tupokee shilingi bilioni 251 kwa ajili ya miradi ya afya na elimu, lakini kwa bahati mbaya mpaka sasa pesa zile bado hazijafika kwenye maeneo yetu. Waziri anafahamu kwamba Waziri wa TAMISEMI aliwaita Wakurugenzi wakakubaliana kwamba ni miradi gani ya kimkakati ambayo wanapendekeza kwenye Halmashauri zao na wakataja ile miradi. Kwa hiyo, tumuombe sana Mheshimiwa Waziri suala la afya na elimu ya msingi na sekondari ni muhimu sana katika majimbo yetu.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu wananchi tumewahamasisha, wamejenga madarasa, wamejenga zahanati, wamejenga vituo vya afya, wanategemea Serikali watakwenda kumalizia kupaua na taratibu zingine ili madarasa haya yaweze kutumika. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba ajitahidi kama anaweza atupatie ile shilingi bilioni 251 ili Waheshimiwa Wabunge wote wakitoka humu waweze kuwa na jambo la kuzungumza kwa wananchi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ni uhai, sisi wote tunafahamu bila maji hakuna uhai. Waislamu huwa tunafunga na leo bado watu wanaendelea kwenye sita, akifungua kitu cha kwanza anakimbilia maji. Sasa tunazungumzia miradi ya maji, hali ya miradi hiyo siyo nzuri. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri atukubalie kwenye mapendekezo ya Finance Bill tuone ni jinsi gani tunaweza tukapenyeza hapo ile Sh.50 kwa ajili ya kwenda kwenye Mfuko wa Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linawezekana, hata kama Wabunge wengi waliosimama hapa hawakusema lakini kila mmoja ukimuuliza hapa ni wangapi wanapendekeza ile Sh.50 iongezwe ili iende kwenye Mfuko wa Maji, wote watasema ndiyo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tunaomba kwenye Finance Bill aweze kuliangalia hili na sisi tuko kwenye Kamati ya Bajeti tunaendelea kutoa mapendekezo nadhani na hili tutalileta kwako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie kilimo. Uvinza ni wakulima wa tumbaku lakini zao hili wakulima wamefika mahala wamelikatia kabisa tamaa na chanzo kikuu wanachokitegemea halmashauri ni zao hili. Tunaomba sana Wizara ya Kilimo iangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wa Mikoa ya Kusini wanaomba zile shilingi bilioni 81, lakini na mimi pia nazisemea zile shilingi bilioni 81 kwa sababu asilimia 65 kwa mujibu wa sheria inatakiwa iende kwa wakulima wa korosho, tunaomba ziende. Kwa nini nasema hivi Mheshimiwa Waziri? Waziri ni mzaliwa wa Kigoma, Naliendele wametuletea miche ya mikorosho, tumepokea miche ya mikorosho, tumehamasisha, wananchi wa Uvinza wamepanda korosho kwa mara ya kwanza. Sasa wakisikia korosho imekufa Ukanda wa Kusini na wenyewe watakata tamaa. Kwa hiyo, tunaomba ile asilimia 65 ipelekwe ili na mikoa mingine kama Tabora, Kigoma, Dodoma ambao tumeitikia kulima hili zao la korosho basi tuweze kupata motisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie miundombinu. Tunapitisha bajeti za Wizara hapa lakini hatimaye inafika tarehe 30 Juni, utekelezaji hakuna. Natambua kwamba sisi tumepata pesa ya Daraja la Ilagala, nimwombe Mheshimiwa Waziri atuletee hiyo pesa ya kujenga Daraja la Ilagala. Wananchi watakuwa wameokoka na vifo vya wamama wajawazito na watoto vitapungua. Wanapopata uchungu wakifika kwenye ferry, SUMATRA wametuambia saa 12.00 jioni ndiyo mwisho wa kivuko kutumika. Daraja la Ilagala likijengwa wale wanawake wa kata sita watakuwa wanavuka wanaenda kwenye Kituo cha Afya cha Ilagala wanajifungua kwa wakati bila madhara yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia hili suala la Electronic Tax. Hili suala siyo baya, tunachosema sisi tunaomba yale mapendekezo ya Mwenyekiti waKamati ya Bajeti yapokelewe na yazingatiwe. Kwa sababu huyu mtu kwa muda wa mwaka mmoja atakuwa amerudisha hela yake na faida juu. Tunapompa mkataba wa miaka mitano tunaonesha ni jinsi gani ataondoka ametajirika kwa pesa za walalahoi. Kwa nini nasema za walalahoi? Tukitumia huu mfumo kwa kampuni hiyo tuliyoipendekeza wanaokwenda kuathirika ni walaji, mfano, wanywaji wa soda, bia na maji na wavutaji sigara. Kwa hiyo, hatulikatai hili lakini kwa nini basi tusitoe kipaumbele kwenye kampuni za wazawa? Kwa hiyo, hili suala liangaliwe tusilirukie sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumzie ukurasa wa 72. Wilaya ya Uvinza ni wadau wa chumvi. Tunashukuru kwamba Mheshimiwa Waziri ameona umuhimu wa kutoa tozo mbalimbali. Kwenye hii tozo ya kwanza ukurasa wa 73(a), kufuta ushuru wa mazao ya chumvi unaotozwa na halmashauri, Mheshimiwa Waziri ametuua. Halmashauri ya Uvinza tunategemea tumbaku na chumvi, hii 0.03 tunaomba atuachie. Leo tulikuwa na mmiliki wa kile kiwanda yeye mwenyewe ameona kwamba hii 0.03 isifutwe, iendelee kuwepo ili na sisi halmashauri tuweze kupata hapo kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Waziri, tunayo madini ya chokaa. Madini haya hapa Tanzania hatuna viwanda vikubwa tuna viwanda...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba suala hili la kwenye chumvi liende pia na kwenye chokaa ili wanaochimba chokaa waweze kunufaika na mimi pia ni mdau wa suala hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.