Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Jesca David Kishoa

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ni bahati mbaya sana huu ni mwaka wa tatu nikiwa humu Bungeni kama Mbunge, kwenye Mabunge ya Bajeti, Bunge linakuwa linajikita zaidi kujadili ni namna gani Serikali itumie fedha badala kwa sehemu kubwa kujadili ni namna gani Serikali ikusanye fedha. Nitakwenda kujikita kwenye eneo la ukusanyaji wa fedha. Kuna eneo moja ambalo ni very strategic napenda Mheshimiwa Mpango alizingatie kwa umuhimu mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunajua kwamba Serikali inamiliki shares kwenye makampuni mbalimbali, yapo makampuni ambayo Serikali ina total ownership lakini pia yapo makampuni ambayo Serikali inamiliki asilimia fulani ya shares. Kuna changamoto kubwa sana hapa, haya makampuni ambayo Serikali inamiliki share kadhaa yamekuwa yana tabia ya kutoa taarifa ambazo siyo sahihi. Haya makampuni yanatoa taarifa ambazo siyo sahihi kwenye mitaji yake, faida inayoingiza na usahihi wa gawio ambalo linatolewa Serikalini. Sababu kubwa ya Serikali kushindwa kukagua gawio ambalo inapata kutoka kwenye makampuni haya ni kwa sababu kuna sheria ambayo ipo inambana/inamzuia CAG kufanya uchunguzi kwenye makampuni ambayo Serikali inamiliki shares chini ya asilimia 50. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Dkt. Mpango hauoni kwamba kuna haja kubwa sana ya Serikali kuchukua shares zake kuzihamisha kutoka kwenye haya makampuni na kuzipeleka kwenye Soko la Mitaji (Stock Market)? Tunajua kwamba kwenye Stock Market kuna very serious scrutiny, wanafanya ukaguzi wa kina na mahesabu yanawekwa wazi. Napenda kutumia fursa hii kumwomba sana kuchukua shares kutoka kwenye makampuni mhamishie kwenye Soko la Mitaji ili muweze kujua haya makampuni yanaingiza mtaji na faida kiasi gani na mwisho mjue usahihi wa gawio ambalo Serikali inapata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mifano mizuri sana. Makampuni yote ambayo yako listed kwenye soko la mitaji mfano NMB na TBL wanafanya vizuri sana, wanatoa gawio kubwa kwa Serikali lakini pia wanatoa kodi kubwa sana kwa Serikali. Ni kwa sababu kuna uwazi mkubwa ambao unatokana na Stock Market. Hata humu Bungeni tulipitisha sheria ya kuyataka makampuni ya mawasiliano na makampuni ya madini kuwa registered kwenye Soko la Mitaji purposely kutaka yawe wazi. Sasa unajiuliza kwa nini hamuoni umuhimu kwenye eneo ambalo mna-interest kwa sababu mna shares kwenye haya makampuni, mkachukua shares mkazipeleka kwenye Soko la Mitaji ili muwe na uhakika wa gawio ambalo Serikali inaingiza? Naomba atakapokuja ku-wind up hapa ajaribu kuligusia hili kwa umuhimu wake mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Dkt. Mpango vizuri sana; kuna eneo nimeona amefuta kodi kwa ajili ya ku-influence the investors, well and good, hilo nampongeza sana. Kuna jambo moja ambalo napenda kumshauri, kuna kodi ambayo ina utata mkubwa sana, nashauri ipitiwe upya ikiwezekana na yenyewe iondolewe kwa sababu ina-discourage sana investors.

Mheshimiwa Mwenyekiti, investor anaweza akaja aka- invest kupitia viwanda moja kwa moja na yupo mwingine anaweza akaja aka-invest kupitia kununua shares kwenye Soko la Mitaji. Sasa unakuta mwekezaji ameweka shares zake kwenye Soko la Mitaji, zimekaa kule labda takribani miaka mitatu akaona hakuna kinachoongezeka akaamua kutaka kuziuza, anapokwenda kuziuza muda aliotumia kununua labda ni miaka mitatu iliyopita, let’s say labda alinunua dola 1,000 kwa miaka mitatu iliyopita wakati huo exchange rate ikiwa ni Sh.2,000 akaja labda akauza baada ya miaka mitatu shares zile zile dola 1,000 kwa exchange rate ya Sh.2,200, mnakuja kumtoza Capital Gain Tax kwenye ongezeko la exchange rate. Hii kodi ina-discourage sana investors, nashauri hii kodi iondolewe kwa sababu mnapokuja kukata Capital Gain Tax kwenye ongezeko la exchange rate mnakuwa hamuwatendei haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine ambalo napenda pia kuligusia kwenye sekta ya mifugo. Haya ni maajabu ya dunia, Tanzania tunazalisha maziwa kwa mwaka takribani lita bilioni 2.4, Kenya hapo majirani zetu wanazalisha kwa mwaka lita takribani bilioni 5.4, tuna difference karibu ya lita bilioni 3. Kinachonishangaza zaidi ni kwamba wakati Kenya wanazalisha lita za maziwa bilioni 5.4 Tanzania tunazalisha lita bilioni 2.4 wakati tuna ardhi kubwa sana, mito mingi sana, maziwa na mifugo mingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo, Mheshimiwa Mpina na nashukuru yupo hapa, hakuna sehemu yoyote nimeona amegusia suala hili na ameeleza ana mkakati gani kuifanya Tanzania kuwa champion kwenye uzalishaji wa maziwa. Kama Taifa tuna kila sababu ya kuwa maridadi kwenye uzalishaji wa maziwa kutokana na namna ambavyo tumebarikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na suala la LNG. Hili suala la LNG nililizungumza toka mwaka 2015 naingia humu Bungeni. Limekuwa ni suala ambalo limepigwa danadana miaka nenda miaka rudi. Nilipitia jarida moja la Reuters mwezi Machi, 2018, TPDC wananukuliwa wanasema kwamba makubaliano ya LNG pamoja na haya makampuni mjadala wake kwa sababu umeshakuwa mzito na wameushindwa, Serikali imetangaza sasa apatikane Mshauri Mwelekezi aweze kutoa mawazo yake aisaidie Serikali kuweza kuingia makubaliano sahihi na haya makampuni. Mkurugenzi wa TPDC akanukuliwa akisema kwamba toka mwezi Machi mpaka kufikia mwezi wa Mei, suala hili litakuwa
limekwishatekelezeka, lakini mpaka sasa hivi tunaenda mwezi Agosti hakuna kunachoeleweka wala kinachofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya sana kwa sababu huu ni mradi ambao unakwenda kutengeneza historia mpya ya Taifa letu katika ukanda wa Afrika Mashariki, hakuna mradi mkubwa kama huu Ukanda wa Afrika Mashariki nzima. Ni mradi mkubwa sana. Ni investment kubwa sana ambapo kama Serikali nilitegemea hata kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri angeielezea kwa mapana yake, kwa uzuri na kwa kuifafanua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyoendelea kuchelewa hivi Msumbiji wameshateka soko lote la East Africa. Ni vema tukatumia nafasi hii vizuri, kama huyo mtaalam mnamtafuta wa kuja kusaidia ku-negotiate kwenye masuala ya kisheria na kuhakikisha kwamba kunakuwa na win-win situation do that, kwa nini mnachelewa? Kwa nini suala hili mnakuwa mnalipiga danadana miaka nenda miaka rudi? Inasikitisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nigusie Deni la Taifa. Deni la Taifa linazidi kukua kwa kasi ya ajabu na linazidi kukua kwa sababu kuna mambo mengine ambayo tunayaona kama ni madogo lakini yanachangia kwa kiwango kikubwa sana ukuaji wa deni hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kumsikia Mheshimiwa Rais hata Mheshimiwa Waziri kipindi fulani akisema kwamba Serikali iko pia busy kulipa madeni ya kipindi cha nyuma sana. Kwa kufanya hivyo, tafsiri yake ni kwamba kuna fedha ambazo Serikali inalipa madeni ya nyuma ambayo yalikopwa kwa exchange rate ya kiwango hicho kwa wakati huo. Mnapokuwa mnalipa wakati huu mnalipa kwa exchange rate ya wakati huu kwa maana hiyo mnakuwa mnalipa fedha nyingi zaidi ukilinganisha na kama madeni hayo yangelipwa wakati huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna njia ambayo niliisoma ambayo Uganda wanai-apply katika kukopa na kulipa. Kuna mfumo ambao…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)