Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Janeth Maurice Massaburi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. JANETH M. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru kwa kuweza kunipa fursa hii. Pia nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa zawadi ya uhai na kuweza kusimama hapa katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara kupitia jeshi la polisi itupatie taarifa ya kifo cha Chacha Wangwe, tunaomba taarifa ya kifo cha Mchungaji Mtikila, tunaomba taarifa ya watalii waliomwagiwa tindikali kule Zanzibar, tunaomba taarifa ya Makanisa yaliyochomwa moto Zanzibar. Tukumbuke nchi yetu iko hapa kwa mkono wa Mwenyezi Mungu na tangu kuhasisiwa kwake tangu enzi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, enzi ya Mzee Mwinyi, enzi ya Mzee Mkapa, enzi ya Mzee Kikwete na sasa hivi enzi ya ndugu yetu Dkt. John Pombe Magufuli. Hawa wote wamewekwa hapa kwa ruhusa na mkono wa Mwenyezi Mungu na ndiyo maana hata ukiangalia maisha yao ni ya kawaida sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba ndugu zangu tusitumie fursa ya viongozi wetu kukaa kimya na kuweza kuwatukana hovyo hovyo. Tulikuwa tukimtukana Mheshimiwa Kikwete sana, mpole tukamhujumu hata kwenye miradi yake, lakini Mwenyezi Mungu alikuwa amemsimamia alikuwa upande wake. Vilevile Rais wa Awamu ya Tano kuna mkono wa Mwenyezi Mungu na nasema watapambana lakini hawatashinda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbukeni ndugu zangu tuliapa kuitetea na kuilinda katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa maana hiyo tulisema tutalinda Muungano kwa gharama yoyote. Tarehe 26 Aprili ni siku ambayo tunakumbuka Muungano wetu ulioasisiwa na ndiyo maana yale mazoezi na parade mlizoziona ndiyo gharama za kulinda Muungano. Kwa hiyo, tumesikia watu wanasema gharama zimekuwa kubwa tungejenga shule. Ile ni sehemu ya kulinda Muungano wetu ndiyo gharama zenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nchi ni yetu sote humu ndani tuko kama mia tatu na kitu, lakini tukumbuke Watanzania wako zaidi ya milioni 60 sisi tunajiona kama tuna haki zaidi ya Watanzania walio wengi. Kuna wakulima, wavuvi, wamachinga, watu wasio na vyama, wenye dini, wapagani, kila mtu ana haki na hamasa ambazo zinatolewa kwa kutubagua sisi tunaomba zishindwe katika jina la Yesu na hazitafanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza IGP wetu na Makamanda wote wa Mikoa yote na Wakuu wa Mikoa kwa kazi nzuri sana wakiongozwa na Waziri, Naibu Waziri bila kumsahau Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama. Wamefanya kazi nzuri sana kuhakikisha nchi inakuwa salama, bila amani hatuwezi kulima, bila amani hamna kwenda shule, bila amani hakuna kustarehe, bila amani hamna kuzaliana, bila amani hamna kizazi endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tusitanie amani kwa kutumia dini, kwa ku-convince watu kwamba dini fulani inaonewa, hakuna! Mbona wewe kama dini unabaguliwa mbona uko humu ndani? Tuko dini tofauti humu ndani, kama kungekuwa kuna ubaguzi tusingekuwepo. Tusitanie amani kwa sababu tuna dhamana ya kulinda uhuru wa nchi hii tuweze kurithisha na vizazi vijavyo. Tumeikuta nchi hii ikiwa na amani, kama mnatumika na maadui wa ndani na wa nje waambieni Tanzania haitaniwi, iko imara, hakuna utani katika masuala ya amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iongeze bajeti ya kutosha katika vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, tunaomba magari yaongezwe, tunaomba mafuta yaongezwe, tunaomba makazi yao yaboreshwe na kujengwa nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba maslahi ya askari; katika nchi nyingine nimetoa mfano kadhaa kule Marekani bajeti yao ya kwanza yenye kipaumbele ni ulinzi bila ulinzi yote hayawezi kutekelezeka, mbona wewe nyumbani kwako unafunga mlango, mbona unajenga geti, mbona unaweka walinzi, tusitaniane katika mambo ya ulinzi wa nchi na wala hatutishwi, sisi Wabunge wa Chama cha Mapinduzi hatutishwi na tupo imara. Mmetushika pabaya katika masuala ya amani hatutaniwi, sisi tutatoka kwenye Bunge hili na kizazi kitaendeleza ulinzi kwa sababu Mungu yuko pamoja na sisi kwa sababu Mungu ni wa amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee Jeshi la Zimamoto, kama alivyosema Mjumbe aliyemaliza kwa kweli limekuwa lina mwamko mdogo na hasa kwenye Wizara yenye dhamana ya kupanga bajeti katika jeshi hili. Tunaomba Jeshi la Zimamoto lipewe fedha za kutosha, sisi sote hapa majanga ya moto huwa yanatokea huko mtaani na majumbani kwetu, jeshi lipewe vifaa, magari ya kutosha, majengo yako marefu sana Dar es Salam, Dodoma Makao Makuu, jengo la Bunge hivi tuna vifaa vya kisasa vya kutosha kukabiliana na janga la moto, vifaa vya uokoaji au ikitokea majanga tunaita watu kutoka South Afrika? Naomba jeshi hili liimarishwe kama vilivyo vikosi vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Idara ya Uhamiaji, naomba idara hii pia iongezewe bajeti ya kutosha kukabiliana na wahamiaji haramu, Dar es Salaam kule mkienda Kariakoo unakuta sura tofauti maana yake sisi Watanzania tunajuana. Nimwambie Mheshimiwa Waziri, wako wengi Dar es Salaam bila kutaja ni mataifa gani, mimi nakaa maeneo ya Segerea kule. Siku hizi kuna majirani wageni tunashangaa, tutumieni sisi Wajumbe wa Mabalozi wa CCM tunaweza kuwaambia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiongelee Jeshi la Magereza; Jeshi hili liongezewe bajeti ya kutosha ili wajenge makazi ya askari wapatiwe usafiri unakutana na askari magereza anaomba lifti, unakuta pale askari magereza amekaa kona anaomba lifti ni jambo la aibu mno. Anakuwa mnyonge, matokeo yake ndiyo huwa wanatukanwa hovyo hovyo. Naomba watoe pesa tuwekeze kama tunavyowekeza kwenye Stiegler’s Gorge, katika masuala ya ulinzi yapewe kipaumbele, miradi hii yote mikubwa haiwezi kutekelezwa kama hamna ulinzi wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie kusema sisi tutakuwepo, tutaondoka watakuja wengine, lakini kizazi cha Watanzania cha sasa na cha kijacho kinatutegea sisi, ulimi wetu tuutumie vizuri, tukiongozwa na roho ya Mungu, tusitumie dini kudanganyana hapa, hata mpagani anaweza kuona ufalme wa mbingu wewe ambaye unasema unadini ukapelekwa motoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante.